Serikali yafafanua kuingia bure uwanjani mechi ya Simba dhidi ya Berkane

Kamishna Idara ya Michezo, Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo Zanzibar, Ameir Mohammed Makame (kulia) akifafanua taarifa za kuingia bure uwanjani katika mechi ya marudio ya Simba na Berkane ya Morocco kushoto ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Kauli hiyo imekuja baada ya kusambaa taarifa tangu jana Mei 22, 2025 na leo zikidai Rais Hussein Mwinyi amelipia gharama zote hivyo wananchi wataingia bure kutazama mechi hiyo.
Unguja. Baada ya kuibuka taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikidai Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amelipia gharama zote za mechi ya marudio ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Simba na RS Berkane ya Morocco, serikali imesema viingilio vipo pale pale.
Mechi hiyo ya marudio inatarajiwa kuchezwa Jumapili Mei 25, 2025 saa 10: 00 jioni katika uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Jana Mei 22, 2025 zilianza kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwani tayari Rais mwinyi amelipia gharama zote na wananchi wote wataingia bure kushuhudia mchezo huo wa marudio.
Akitolea ufafanuzi jambo hilo wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Mei 23, 2025, Kamishna Idara ya Michezo Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo Zanzibar, Ameir Mohammed Makame amesema alicholipia Rais Mwinyi ni gharama za uwanja asilimia 15 pekee na sio viingilio vya wananchi.
“Hizi taarifa jamani sio za kweli kwamba mheshimiwa Rais amelipia gharama zote na viingilio, tunaomba ieleweke kwamba alichosaidia kwa mapenzi makubwa aliyonayo amelipia asilimia 15 tu za uwanja, kwa hiyo viingilio vipo pale pale,” amesema
Kuna aina tatu za viingilio katika mchezo huo: Daraja la kwanza (VIP) ni Sh50, 000, darala la pili Sh30,000 na Sh10,000 kwa daraja la tatu.
Naye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema kupitia Kamisheni ya Utalii wameona watumie fursa hiyo kuitangaza Zanzibar ikizingatiwa michezo kwa sasa ni moja ya bidhaa inayotumika kuitangaza Zanzibar na watatumia bidhaa yao mpya ya Visit Zanzibar kuinadi zaidi.
“Hii ni sehemu ya kuitangaza Zanzibar kitaifa, kikanda na kimataifa na tutatumia fursa hiyo kujitangaza na maana mechi hii itakuwa inatazamwa na zaidi ya mataifa 27 ya Afrika,” amesema
Kwa mujibu wa Soraga, watalii wengi wanaokwenda kutembelea kisiwa hicho wanatoka bara la Ulaya lakini huo ni mpango mpya kuongeza watalii kutoka Afrika.
“Nasema hivi kwa sababu Morocco wamekuja na watu wengi sio wachezaji pekee wakiwa hapa wataona na watakuwa mabalozi watakaporudi kwenye taifa lao nao watashajiisha wengine kuja kutembelea Zanzibar.
“Huu ni mwelekeo mzuri mashindano kama haya kufanyika hapa Zanzibar kwa mara ya kwanza inaonesha namna gani tunavyozidi kuchanja mbuga kusonga mbele kimataifa,” amesema
Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni Utalii, Arif Abbas Manj amesema sekta ya utalii ndio inachangia asilimia kubwa ya uchumi wa Zanzibar na kwamba wamejipanga kuhakikisha wananchi wote wanaofika wanapata sehemu nzuri za kulala bila wasiwasi.
“Hii ndio dhana halisi ya utalii tumejipanga wananchi wajitokeze kwa wingi kuhshuhdia mechi hii zipo hoteli za kutosha wasihofu tunwakaribisha,” amesema