Maofisa 16 CAF kusimamia Fainali Simba, RS Berkane

Muktasari:
- Mchezo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Simba na RS Berkane utachezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Jumapili Mei 25, 2015 kuanzia saa 10:00 jioni:
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua maofisa 16 kwa ajili ya kusimamia mchezo wa marudiano wa hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Simba na RS Berkane Jumapili wiki hii katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa kuanzia saa 10:00 ambapo Simba inahitajika kupata ushindi wa tofauti ya angalau mabao matatu ili iweze kutwaa ubingwa baada ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini kwa mabao 2-0.
Orodha hiyo ndefu ya maofisa wa CAF itaongozwa na refa wa mchezo Beida Dahane kutoka Mauritania ambaye atasaidiwa na marefa wasaidizi, Jerson Dos Santos kutoka Angola na Adou Desirw N’goh kutoka Ivory Coast.
Waamuzi hao watatu watapata sapoti ya refa wa akiba wa mchezo, Abdel Aziz Bouh ambaye naye anatoka Mauriatania.
Kutakuwa na marefa watatu ambao watakuwa kwenye chumba cha teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) ambao wataongozwa na Issa SY kutoka Senegal.
Marefa wasaidizi wa VAR ni Akhona Makalima wa Afrika Kusini na Arsenio Maringule kutoka Msumbiji.
Kamishina wa mechi ni Mohamed Yonis, Mratibu ni Helly Zafinimanga kutoka Madagascar na Djamel Halmoudi wa Algeria ndio mtathmini wa marefa.
Kutakuwa na Maofisa Habari wawili kwenye mechi hiyo ambao ni Ahmed Hussein wa Uganda na Clifford Ndimbo wa Tanzania.
Maofisa wa Usalama ni wawili ambao ni Amr Salman wa Misri na Joe Sakaumba wa Zambia huku Mratibu Msaidizi wa mechi ni Rasha Elghorour na Gift Macha wa Tanzania ameteuliwa kuwa Meneja wa Urushaji Matangazo uwanjani.