Prime
Simba kimkakati zaidi Misri, yatanguliza sita juu kwa juu

Muktasari:
- Baada ya kucheza na Bigman FC, Simba itasafiri kwenda Misri kupambana na Al Masry katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika hatua ya robo fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Suez Canal Aprili 2, huku mikakati kabambe ikiundwa mapema.
Dar es Salaam. Simba inashuka kwenye Uwanja wa KMC Complex Alhamisi kwa ajili ya mchezo wa hatua ya 16, bora wa Kombe la Shirikisho (FA), dhidi ya timu changa ya Bigman FC. Lakini mabosi wa kikosi hicho hesabu zao zipo Al Masry na mastaa sita watatangulizwa juu kwa juu.
Baada ya kucheza na Bigman FC, Simba itasafiri kwenda Misri kupambana na Al Masry katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika hatua ya robo fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa New Suez Canal Aprili 2, huku mikakati kabambe ikiundwa mapema.
Moja ya mikakati ni kuhakikisha wachezaji sita waliokuwa katika majukumu ya timu ya taifa ya Tanzania iliyofungwa mabao 2-0 na Morocco Jumanne usiku, wanaunganisha moja kwa moja kwenda Misri wakitokea Morocco, kwa lengo la kuwapunguzia safari zitakazowachosha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema wachezaji wote waliokuwa Morocco wataunganisha moja kwa moja na watawahi Misri.
Wachezaji wa Simba waliofanyiwa utaratibu huo wa kwenda Misri ni Ally Salim, Abdulrazack Hamza, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yusuph Kagoma, Kibu Denis na Shomari Kapombe.
Nyota hao walishuhudia ndoto ya Stars kucheza Kombe la Dunia mwaka 2026, ikififia baada ya kuchapwa mabao 2-0, dhidi ya Morocco iliyojikatia tiketi tayari, na sasa hesabu ni za mchezo wa kwanza wa Simba wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema kwa sasa mawazo yake ni kumalizana na Bigman FC, kisha; “Hatuwezi kuangalia mchezo wa mbele zaidi ya huu tulionao kwa sasa, inaweza kututoa katika malengo yetu kwa sababu tunaweza kumpa mpinzani wetu nguvu, hatutaki kuingia kwenye mtego huo isipokuwa tutapambana na kilichopo mbele.”
Fadlu alisema wapinzani wao wana timu nzuri na inayobadilika mara kwa mara na hilo wamelionyesha kwa mechi walizocheza kuanzia kwao Misri na ile ya kimataifa, hivyo watapambana ili kujitengenezea mazingira mazuri mechi ya marudiano Aprili 9.
Simba iliyomaliza kinara wa kundi A na pointi 13, imepangiwa na Al Masry iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kundi D na pointi tisa, nyuma ya wapinzani wao kutoka Misri, Zamalek ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo 2023-24.
Pambano hilo la Aprili 2 la Al Masry na Simba litakuwa ni la tatu kwao kukutana kwa miaka ya hivi karibuni baada ya mwaka 2018.
Timu hizo zilikutana raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo mechi ya jijini Dar es Salaam zilitoka sare ya mabao 2-2, Machi 7, 2018, kisha marudiano Misri zikatoka suluhu (0-0), Machi 17, 2018, na Simba kutolewa kwa mabao ya ugenini.
Wakati Simba ikitarajia kuondoka nchini keshokutwa, rekodi zinaibeba zaidi kutokana na uwiano mzuri wa kufunga bao kwenye kila kipindi Ligi Kuu, ukilinganisha na Masry.