CAF yaipa uhakika Simba kwa Al Masry

Muktasari:
- Mechi ya mwisho kwa Simba kucheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ilikuwa ni ya Ligi Kuu dhidi ya Azam FC ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Azam FC, iliyochezwa Februari 24, 2025.
Dar es Salaam. Simba imetamba kuwa imehakikishiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi yake ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, Aprili 9, 2024 baada ya wakaguzi wa shirikisho hilo kuukagua uwanja huo juzi.
Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa mashabiki wa Simba na Watanzania kiujumla hawapaswi kuwa na wasiwasi kwani mchezo huo dhidi ya Al Masry utapigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa vile wakaguzi wa CAF wameridhishwa na maboresho ambayo yalipendekezwa kufanyika katika uwanja huo.
“Niwatoe hofu kwamba Uwanja wa Benjamin Mkapa umeshafanyiwa ukaguzi. Bado majibu hayajatoka lakini katika mazungumzo wanasema kuna maboresho makubwa kwenye uwanja ukilinganisha na mara ya mwisho walipofanya ukaguzi.
"Hivyo kuna nafasi kubwa ya kucheza kwenye uwanja huo. Na wote mnakumbuka kauli ya Msemaji Mkuu wa Serikali alivyosema kwamba uwanja upo tayari. Hatuna muda wa kusubiri, sisi tunafanya maandalizi yote kuelekea Benjamin Mkapa kwa sababu tuna uhakikisho kutoka serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Ally.
Ahmed Ally amesema kuwa bei ya chini ya kiingilio katika mchezo huo ni Sh5,000 na ya juu itakuwa ni Sh 250,000.
“Mechi hii tunataka kuingiza mashabiki kati ya 50,000 hadi 60,000 hivyo tutafanya hamasa kubwa, mtaa kwa mtaa ili kuwahamasisha Wanasimba kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo muhimu. Safari hii tutatembelea matawi mengi sababu tunataka watu wengi waje uwanjani.
“Wale wote ambao walinunua tiketi dhidi ya Constantine watatumia tiketi zao kwenye mchezo dhidi ya Al Masry," amesema Ally.
Katika hatua nyingine, Ahmed Ally ametoa taarifa ya safari ya timu hiyo kuelekea Misri ambako itacheza mechi ya kwanza dhidi ya Al Masry, Aprili 2, 2025.
“Kikosi kitaondoka nchini alfajiri ya tarehe 28 kuelekea Misri kwa kutumia ndege ya Egypt Air. Wachezaji wetu waliokuwa Taifa Stars wataungana na timu nchini Misri. Camara na Mukwala tayari wamewasili nchini kujiunga na wachezaji wenzao kwa ajili ya maandalizi ya safari.
“Kila Mwanasimba atambue kwamba pamoja na mipango tuliyonayo lakini lazima tujipange, lazima tujiandae na hasa kama timu yenyewe inatokea Misri. Ukiangalia michuano ya Afrika ilivyo utaona kwamba Misri ndio nchi iliyoingiza timu nne kwenye robo fainali,” amesema Ally.