Refa Inter, Barca hana masihara

Muktasari:
- Szymon Marciniak mwenye umri wa miaka 44, amechezesha mechi tisa za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Refa asiye na mzaha kwa wachezaji wanaocheza faulo na watovu wa nidhamu, Syzmon Marciniak kutoka Poland atachezesha mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Inter Milan na Barcelona leo, Mei 6, 2025 katika Uwanja wa San Siro.

Marciniak raia wa Poland mwenye umri wa miaka 44, anasifika kwa kumwaga kadi kwa wachezaji ambao wanafanya makosa ndani ya uwanja.
Katika mechi 10 za mashindano tofauti ambazo Marciniak amechezesha hivi karibuni, ametoa idadi ya kadi 55 ikiwa ni wastani wa kadi 5.5 kwa mchezo ingawa kadi hizo zote ni za njano.
Marciniak atasaidiwa na Tomasz Listkiewicz na Adam Kupsik huku refa wa akiba akiwa ni Pawel Raczkowski ambao wote wanatoka Poland.
Katika mchezo kila timu inahitaji ushindi ili iweze kusonga mbele baada ya mchezo wa kwanza baina yao ambao Barcelona ilikuwa nyumbani wiki iliyopita, ulimalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi 13 ambazo timu hizo zimekutana, Barcelona imeibuka na ushindi mara sita, Inter Milan imeshinda mbili na zimetoka sare mara tano.
Katika mechi hizo 13 zilizopita baina ya timu hizo, Inter Milan imefunga mabao 13 na Barcelona imefumania nyavu mara 20.

Kocha wa Barcelona, Hans Flick amesema kuwa timu yake inahitaji matokeo mazuri katika mechi hiyo.
“Tayari tumepata mataji mawili msimu huu. Wachezaji wote wameimarika kadri mechi zinavyoongezeka. Sasa tupo katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na tunatakiwa kufurahia hilo. Kufurahia kucheza na kila mmoja na kuonyesha kila mmoja jinsi tulivyo wazuri,” amesema Flick.

Kocha wa Inter Milan, Simone Inzaghi ametamba kuwa timu yake haina presha na mechi hiyo.
“Tunajua umuhimu wa mechi hii. Tunahitaji kuwa na kiwango bora dhidi ya timu imara ambayo tumeiona. Kundi lina wachezaji wanaojiamini na wanaitaka mechi na wanaisubiria kwa hamu mechi hii,” amesema Inzaghi.