Rais Samia akutana na wanamichezo Dar
Muktasari:
- Katika hafla hiyo ya kuzipongeza timu za taifa zilizofanya vizuri kwa mwaka 2025, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo wa Serikali, viongozi wa klabu, wachezaji wa sasa na wa zamani, wanariadhaa, mabondia na Waandishi wa Habari.
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Saluhu Hassan, ameipongeza timu ya taifa ya Taifa Stars kwa kufika hatua ya 16 Bora ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), inayoendelea kurindima huko Morocco.
Stars iliyokuwa inashiriki mashindano hayo kwa mara ya nne, ilitolewa na wenyeji, Morocco kwa kuchapwa bao 1-0, ingawa imeweka rekodi ya kipekee, ikiwa ni mara ya kwanza inafikia hatua hiyo, kwani mara tatu zote ilikuwa ikiishia makundi.
Samia amezungumza hayo alipowaalika wanamichezo, wadau wa michezo viongozi wa serikali na wachezaji wa zamani Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam, katika hafla ya chakula cha mchana kwa lengo la kuwapongeza kwa kazi kubwa walioifanya kwenye mashindano hayo.
"Mafanikio haya ni makubwa na ni fahari kwa taifa letu na ni ushahidi kwamba soka letu linaendelea kupanda viwango vya ubora Barani Afrika, kwa mara ya kwanza nilikaa kwenye televisheni mwanzo hadi mwisho," alisema Samia na kuongeza;
"Siku hiyo nilikuwa nimefunga nimekaa kufutari, wakati naendelea na futari yangu tayari mechi inataka kuanza, nikakaa na kuangalia watoto wangu kazi wanayoifanya, lakini nikaondoka pale mwili wote unaniuma mlipokuwa mkipigwa na kuzuiwa."
Aidha, Rais Samia alisema anajua ni kwa nini mambo yote yaliyotokea kwa sababu tuliocheza nao ni wenyeji wa mashindano hayo, taifa lenye fedha na taifa lenye ushawishi pia, ingawa dunia nzima imeona wazi kwamba Tanzania ni wapambanaji.
"Nalipongeza pia benchi la ufundi, viongozi wa timu na wanamichezo wengine wote mliopo hapa, ni ukweli kama walivyosema walionitangulia michezo yetu imepanda, naipongeza pia timu ya kriketi kwa kufuzu Kombe la Dunia Namibia," alisema Samia.
Pia, Rais Samia aliipongeza timu ya Mpira wa Miguu ya Wanawake Futsal kwa kushiriki Kombe la Dunia Ufilipino na mabondia waliotwaa mikanda ya kimataifa, ikiwemo timu ya taifa ya ridhaa iliyopata medali 18, ikiwemo moja ya dhahabu, medali za fedha nne na 13 za shaba katika mashindano ya kanda ya tatu ya Afrika yaliyofanyika Nairobi Kenya.
"Tunakwenda ndugu zangu, tulikotoka sio tulipo leo, walau jina la Tanzania linasikika na kuonekana kwenye kila fani, pia nawapongeza mabondia kwa ushiriki wa mashindano ya dunia yaliyofanyika Dubai, ambapo bondia wetu mmoja alifika hatua ya 16 bora."
Katika hatua nyingine, Rais Samia alizipongeza timu za taifa zilizofanya vizuri kwa ukanda wa CECAFA, zikiwemo timu za vijana, timu za shule, timu za kuogelea na timu za watu wenye ulemavu, kwa kuipeperusha vyema bendera nje ya Tanzania.
Pia, Rais Samia alimpongeza mwanariadha, Alphonce Felix Simbu, kwa kushinda medali ya dhahabu ya Tokyo Marathon 2025, akiwa ni Mtanzania wa kwanza kutwaa dhahabu ya kimataifa na Sisilia Ginoka Panga kwa kutwaa dhahabu ya mbio za kilomita 15 zilizofanyika Sao Paulo, Brazil.
"Jitihada na nidhamu mlizozionyesha ni alama ya uzalendo wa kweli, mmeipeperusha vyema bendera yetu ya taifa la Tanzania na mmeandika historia mpya kwa taifa letu katika ulimwengu wa michezo," alisema Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alisema Tanzania ina kazi kubwa ya kuandaa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, hivyo, maandalizi yanahitajika mapema, mshikamano wa kitaifa na ushirikiano wa karibu kati ya wadau wa michezo nchini na Serikali.
"Ni wajibu wetu sote kuhakikisha AFCON 2027, inafanyika kwa ufanisi mkubwa, kwa heshima na manufaa ya taifa letu, ni dhahiri ili tufanye vizuri hatuna budi kuwekeza katika maendeleo ya wachezaji wetu wanaohitaji mechi nyingi za ndani ili kupata uzoefu," alisema na kuongeza;
"Nitoe rai ya ushirikiano baina ya klabu na wadau wa soka kuhakikisha Ligi zetu zinaendelea kuwa imara, shindani na pia zinawapa nafasi wachezaji wazawa kukua, tusiwarudishe nyuma ili wakue, kwani uzoefu utawaandaa vyema kushindana katika nyanja za kimataifa."
Aidha, Rais Samia alisema atahakikisha anaendelea kuboresha maslahi na posho mbalimbali kwa timu za taifa, baada ya hivi karibuni kupata taarifa kutoka vyombo vya Serikali Taifa Stars kugoma ikiwa Misri kabla ya kwenda Morocco kwenye mechi za AFCON.
"Kwa wachezaji tunajua mnachohitaji lakini kuhusu suala la posho zenu niwahakikishie hilo tutalifanyia kazi," alisema Samia.
Pia, Rais Samia alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Shirikisho la Soka Barani Africa (CAF), Patrice Motsepe, kwa kumtunuku Tuzo Maalum, ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wake mkubwa anaoendelea kuuonyesha katika mchezo wa soka.
Katika hafla hiyo ya kuzipongeza timu za taifa zilizofanya vizuri kwa mwaka 2025, zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo wa Serikali, viongozi wa klabu, wachezaji wa sasa na wa zamani, wanariadhaa, mabondia na Waandishi wa Habari.