PSG mabingwa UEFA wakiweka rekodi

Muktasari:
- PSG imeweka rekodi ya ushindi mkubwa zaidi wa fainali ya UEFA Champions League na wa kwanza kwa tofauti ya mabao matano.
Munich, Ujerumani. Hatimaye PSG imevunja laana ya miaka mingi kwa kutwaa kwa mara ya kwanza katika historia yao taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League), baada ya kuichapa Inter Milan ya Italia mabao 5-0 katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena, Munich, Ujerumani.

Mabao ya ushindi wa PSG yalifungwa na Achraf Hakimi aliyeanza kufungua karamu ya mabao katika dakika ya 12, akimalizia kwa pasi ya Désiré Doué ambaye aliiongezea PSG bao la pili katika dakika ya 20 akipiga shuti la mbali lililomshinda kipa, Yann Sommer kabla ya kurejea tena dakika ya 63 na kufunga bao la tatu, akionyesha ubora wake mkubwa katika mchezo huo.

Khvicha Kvaratskhelia alipachika bao la nne katika dakika ya 73 akipiga mkwaju mkali ndani ya boksi, kabla ya Senny Mayulu kufunga bao la tano na la mwisho katika dakika ya 86, akiweka historia kwa bao lake la kwanza kwenye fainali ya UEFA, na kuhitimisha kipigo kizito dhidi ya mabingwa wa zamani, Inter Milan.
Ushindi huu umeweka rekodi ya ushindi mkubwa zaidi wa fainali ya UEFA Champions League na wa kwanza kwa tofauti ya mabao matano tangu mwaka 1994, wakati AC Milan walipoifunga Barcelona mabao 4-0 mjini Athens, Ugiriki.

Kocha wa PSG, Luis Enrique, ameweka historia baada ya kutwaa taji hili mara mbili na vilabu viwili tofauti. Alicheza fainali yake ya kwanza mwaka 2015 na kutwaa ubingwa akiwa na FC Barcelona, na sasa ameongoza PSG kutwaa taji lao la kihistoria msimu wa 2024/2025.
Pia, kocha huyo ameiongoza PSG kutwaa mataji matatu ndani ya msimu mmoja yaani ‘Treble’ ambapo walitwaa taji la Ligi Kuu Ufaransa, Coupe de France na sasa UEFA Champions League.
Kwa upande wa Inter Milan, hii ilikuwa ni fainali yao ya sita katika historia ya mashindano haya, ambapo walishinda mara tatu (1964, 1965 na 2010), lakini sasa wamepoteza mara ya nne.
Inter Milan wametoka kapa msimu huu baada ya kunyang’anywa taji la Ligi Kuu Italia ‘Seria A’ ambalo lilibebwa na Napol kwa tofauti ya pointi moja dhidi yao huku katika michuano ya Copa Italia waliondolewa katika hatua ya nusu fainali na wapinzani wao AC Milan ambao nao walipoteza fainali kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Bologna.