Chelsea yaweka rekodi Ulaya, ikitwaa UEFA Conference League

Muktasari:
- Kwa ushindi huu, Chelsea wamefikisha jumla ya mataji saba ya UEFA, hatua inayoiweka klabu hiyo kuwa miongoni mwa vilabu vyenye mafanikio Ulaya.
Chelsea imeweka historia mpya usiku wa kuamkia leo kwa kutwaa taji la UEFA Conference League baada ya kuifunga Real Betis ya Hispania kwa kichapo cha mabao 4-1 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Wrocław, Poland.
Kwa ushindi huo, Chelsea imekuwa timu ya kwanza katika historia ya soka barani Ulaya kutwaa mataji yote makuu manne ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), ambayo ni Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League), Kombe la Washindi (Cup Winners’ Cup), UEFA Europa League, na sasa UEFA Conference League.
Real Betis ndiyo walitangulia kwa bao la mapema lililofungwa na Abde Ezzalzouli katika dakika ya tisa, lakini Chelsea walirejea kipindi cha pili kwa nguvu, wakifunga mabao manne kupitia kwa Enzo Fernández, Nicolas Jackson, Jadon Sancho na Moisés Caicedo.
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, ambaye ni raia wa Italia, ameweka jina lake kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kutwaa taji lake la kwanza akiwa na timu hiyo tangu alipojiunga Julai 2024.
Baada ya kuiwezesha Chelsea kubeba taji hilo Maresca amesema ushindi huo ni matokeo ya mshikamano na kazi kubwa ya kikosi chake.
"Hii ni siku ya kipekee kwa klabu, mashabiki, na kila mmoja aliyekuwa sehemu ya safari hii. Tumeweka historia ambayo haijawahi kufikiwa na timu yoyote Ulaya," amesema Maresca baada ya mechi.
Licha ya kupoteza, Real Betis walicheza kwa kujituma na kuonyesha kiwango cha juu. Walitengeneza nafasi kadhaa, hasa kupitia Lo Celso na Isco, lakini walikosa umakini wa kumalizia mbele ya lango la Chelsea.
Kocha wa Betis, Manuel Pellegrini alikiri kuwa Chelsea walikuwa bora, lakini akaeleza kuwa timu yake imejifunza mengi na itarejea imara msimu ujao ambapo watakuwa kwenye mashindano ya Europa League.
"Tumefika mbali. Hii ni historia kwa Betis. Hatujawahi kufika hapa na tunajivunia mafanikio haya licha ya matokeo ya leo," amesema Pellegrini.
Kwa ushindi huu, Chelsea wamefikisha jumla ya mataji saba ya UEFA, hatua inayoiweka klabu hiyo kuwa miongoni mwa vilabu vyenye mafanikio makubwa Ulaya.
Chelsea inashikilia mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) waliyoyatwaa mwaka 2012 na 2021, mataji mawili ya Europa League, ambayo ni mashindano ya pili kwa ukubwa barani Ulaya, waliyoshinda mwaka 2013 na 2019, mataji mawili ya Kombe la Washindi la UEFA (UEFA Cup Winners’ Cup), ambayo walipata mwaka 1971 na 1998.
Na sasa, taji lao la kwanza la UEFA Europa Conference League, linakamilisha jumla ya mataji saba ya UEFA.
Katika mitaa ya London, usiku wa jana mashabiki wa Chelsea walimiminika barabarani kusherehekea, huku timu hiyo ikitarajiwa kufanya paredi la ushindi wikiendi hii.
Hili ni taji la pili la Ulaya linakwenda England msimu huu baada ya Tottenham kufanya hivyo kwenye michuano ya Europa League ilipoifunga Manchester United bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa San Mames, Bilbao, Hispania.