Huu hapa mfumo mpya Klabu Bingwa Dunia

Muktasari:
- Timu zilizofuzu kucheza mashindano haya ni zile ambazo zilifanya vizuri kwenye mashindano ya Klabu Bingwa misimu minne iliyopita ambayo hufanyika kila Bara.
FIFA iko mbioni kuandika historia mpya katika soka kwa ngazi ya vilabu, kupitia mashindano ya Klabu Bingwa Dunia yatakayofanyika kwa mara ya kwanza kwa mfumo mpya kuanzia mwezi ujao nchini Marekani.
Mashindano hayo, yatakayohusisha jumla ya klabu 32 kutoka mabara mbalimbali, yatafikia tamati Julai 13 mwaka huu na yanatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa, si tu kwenye uwanja wa michezo bali pia kwenye sekta ya uchumi.
Michuano hii, ambayo hapo awali ilihusisha vilabu saba pekee, sasa itakuwa kama ile ya Kombe la Dunia la timu za taifa, ambapo timu zitapangwa katika makundi, kisha kuingia hatua ya mtoano, robo fainali, nusu fainali, hadi fainali.
Kutakuwa pia na mechi ya mshindi wa tatu. Ambapo timu 32 zitagawanywa kwenye makundi manane ya timu nne kila moja, na mbili zitakazo maliza katika nafasi za juu kutoka kila kundi zitatinga hatua ya 16 bora. Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuongeza ushindani, kuvutia mashabiki zaidi, na kuonyesha utofauti wa kandanda kutoka kila kona ya dunia.
Mgawanyo wa timu shiriki
Timu zilizofuzu kucheza mashindano haya ni zile ambazo zilifanya vizuri kwenye mashindano ya Klabu Bingwa misimu minne iliyopita ambayo hufanyika kila Bara ambapo Bara la Ulaya (UEFA) limeongoza kwa kutoa timu 12, Afrika (CAF), Asia (AFC) na Amerika ya Kaskazini (Concacaf), zitatoa timu nne kila mmoja wakati Amerika ya Kusini (Conmebol) yenyewe itatoa timu sita huku Bara la Oceania (OFC) litatoa timu moja.
Mgawanyo wa timu katika makundi
Katika hatua ya makundi, vilabu kutoka nchi au mabara yanayofanana hayatapangwa pamoja, ili kuongeza utofauti. Katika hatua ya mtoano hadi robo fainali, mechi zikimalizika kwa sare zitaamuliwa kwa mikwaju ya penalti moja kwa moja bila muda wa ziada. Muda wa ziada utatumika tu kuanzia nusu fainali.
FIFA itagharamia huduma zote muhimu kwa timu shiriki, zikiwemo usafiri wa ndege, hoteli, chakula, na kambi za mazoezi. Zaidi ya mashabiki milioni 2 wanatarajiwa kuhudhuria michuano hiyo moja kwa moja, kutoka Marekani na duniani kote.
Makundi ya Klabu Bingwa Dunia 2025
Kundi A: Palmeiras, FC Porto, Al Ahly, Inter Miami
Kundi B: Paris St-Germain, Atletico Madrid, Botafogo, Seattle Sounders
Kundi C: Bayern Munich, Auckland City, Boca Juniors, Benfica
Kundi D: Flamengo, Esperance Sportive de Tunisie, Chelsea, Club Leon
Kundi E: River Plate, Urawa Red Diamonds, Monterrey, Inter Milan
Kundi F: Fluminense, Borussia Dortmund, Ulsan, Mamelodi Sundowns
Kundi G: Manchester City, Wydad, Al Ain, Juventus
Kundi H: Real Madrid, Al Hilal, Pachuca, Salzburg