Njooni muone Shoo, Yanga kwa Mkapa

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amewaita mashabiki wa klabu hiyo kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam wakati timu hiyo itakapovaana na USM Alger ya Algeria katika pambano la kwanza la fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha Nabi amesema anajua mechi hiyo ni ngumu kwa kuwajua wapinzani wao kutoka Afrikas Kaskazini ambao huwa na desturi ya kucheza kwa kupoteza muda na kutafuta bao japo moja na kuambulia sare, lakini ametamba wamejiandaa kupata matokeo ili kazi iwe rahisi ugenini.

Yanga ina dakika 90 za mchezo huo utakaoanza Saa 10:00 jioni kabla ya kusubiri dakika nyingine kama hizo ugenini ili kupatikana kwa bingwa wa msimu huu wa michuano hiyo baada ya taji kutemwa mapema na waliokuwa watetezi, RS Berkane Morocco.

Matokeo ya ushindi ni kitu kikubwa na cha muhimu kwa Yanga kukipata katika mechi hiyo ya leo ili ijiweke katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa katika mechi ya marudiano itakayochezwa Juni 3 huko Algeria.
Kinyume na hapo, wawakilishi hao wa Tanzania watakuwa na kibarua kizito katika mchezo wa marudiano ambao watakuwa ugenini, ili waweze kuchukua kwa mara ya kwanza ubingwa wa mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), baada ya kushindwa kufanya hivyo tangu timu hiyo ilipoanzishwa mwaka 1935.

Kazi ipo hapa
Uwezo ulioonyeshwa na timu hizo mbili katika kufumania nyavu katika kila kipindi cha mchezo, unalazimisha kila upande kucheza kwa tahadhari kubwa kwa dakika zote 90 ili usitoe mwanya kwa mwingine kupata mabao yanayoweza kuamua mchezo.
Kipindi cha pili ndicho kinaonekana kuwa cha hatari zaidi kwani idadi kubwa ya mabao kwa kila timu, imefungwa katika muda huo ingawa pia zimekuwa zikifunga katika dakika 45 za mwanzoni.
Katika mabao 17 iliyofunga USM Alger kuanzia hatua ya makundi hadi nusu fainali, tisa kati ya hayo imeyapata kipindi cha kwanza huku nane ikipachika kipindi cha pili, ilihali Yanga katika mabao 15 iliyofunga, matano imepata kipindi cha kwanza na mengine 10 katika kipindi cha pili.
Muda wa hatari zaidi ni ule wa dakika 30 za mwisho za mchezo, kwani Yanga imefunga mabao nane ndani ya muda huo wakati USM Alger katika dakika 30 za mwisho wamefumania nyavu mara tisa.


Miamba hii hapa

Kikosi cha nyota 11 wa Yanga katika mchezo wa leo kinaweza kuundwa na Djigui Diarra, Dickson Job, Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca, Bakar Mwamnyeto, Yannick Bangala, Jesus Moloko, Mudathir Yahya, Fiston Mayele, Aziz Ki Stephane na Kennedy Musonda.
Kwa upande wa wageni USM Alger, kikosi chao kinaweza kuundwa na Oussama Benbot,  Saâdi Redouani,  Haithem Loucif,  Adem Alilet,  Zineddine Belaid,  Oussama Chita,  Abderrahmane Meziane,  Brahim Benzaza, Abdelkarim Zouari,  Aymen Mahious  na  Tumisang Orebonye.


Macho kwa Mkapa

Ni mchezo ambao utavuta kundi kubwa la watu hapa nchini kwa lengo la kuja kuutazama lakini pia umechangia Tanzania itangazwe vilivyo katika nchi mbalimbali hasa barani Afrika, jambo ambalo linasaidia kwa namna moja au nyingine kuhamasisha utalii na kuongeza pato la nchi.
Taarifa za uhakika ambazo gazeti hili limezinasa ni kutakuwa na ugeni wa maofisa zaidi ya 100 kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambao watakuja kusimamia mchezo huo katika nyanja tofauti, huku ikieleza tiketi zote zilizokadiriwa kwenye mchezo huo zikiwa zimeisha tangu mapema jana asubuhi.
Kadhalika wageni USM Alger wamekuja na msafara wa watu wasiopungua 250 miongoni mwao ni wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi, maofisa wa serikali na chama cha soka Algeria, viongozi pamoja na mashabiki wa timu hiyo.


Ubingwa wa heshima

Fainali hii inakutanisha timu mbili ambazo hazijawahi kuonja ladha ya ubingwa wa mashindano ya klabu Afrika hivyo itakayobeba itakuwa inafanya hivyo kwa mara ya kwanza.
Hii ni fainali ya kwanza kwa Yanga katika mashindano ya klabu Afrika tangu ilipoanzishwa mwaka 1935.
USM Alger ambayo ilianzishwa mwaka 1937, iliwahi kuingia fainali moja ambayo ilikuwa ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015, lakini ikapoteza kwa mabao 4-1 katika mechi mbili baina yao, ikifungwa 2-1 nyumbani na kisha ikapoteza kwa mabao 2-0 ugenini.


Tanzania na Yanga

Kujitosa moja kwa moja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kusapoti maandalizi na hamasa ya Yanga kwa ajili ya mchezo huo kunatoa ishara ya wazi kuwa nchi nzima iko nyuma ya wawakilishi hao pekee waliobakia katika mashindano ya kimataifa kuhakikisha wanapata ushindi leo na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.

Rais Samia kwanza ametoa sapoti kwa kununua tiketi 5,000 ili zigawiwe kwa mashabiki waende kuishangilia Yanga katika mechi hiyo ya leo lakini pia ameahidi kutoa zawadi ya Sh 20 milioni kwa kila bao ambalo Yanga itafunga katika hatua ya fainali.

Jambo kubwa zaidi lingine ambalo Rais Samia amelifanya kwa Yanga ni kuwapatia ndege ambayo itawapeleka moja kwa moja Algeria kwa ajili ya mechi ya marudiano, kuwasubiri na kisha kuwarudisha jambo ambalo halikuwa kufanyika kwa klabu nyingine yoyote hapa nchini.

Hesabu zinaonyesha tangu Rais Samia alipoanza kununua mabao kwenye mechi za makundi kwa timu za Simba iliyoishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Yanga iliyotinga fainali, Vijana wa Nabi wameshavuta jumla ya Sh 155 Milioni na kama leo watashinda wataendelea kutunisha mfuko.


Tambo kila kona

Kocha Nabi alisema mchezo huo utakuwa ni wa kiufundi kwa sababu wapinzani wao wana mpango wa kuja kupata bao la ugenini hata moja, huku upande wao Yanga, lengo lao  ni kuhakikisha kufunga mabao mengi na kujiweka sehemu nzuri.

"Tunajua kabisa namna ambavyo watakavyokuja kucheza hapa, tunataka tufunge lakini tutashambulia huku tukiwa tunajilinda na nimeshaongea na wachezaji kuhakikisha tunafanya vizuri.

"Ilishawahi kutokea kwenye mechi na Al Hilal ile tulishambulia na tukasahau kujilinda, hii nayo ni timu kubwa na ndio maana imefika hapa kwenye fainali," alisema Nab.

Kocha wa USM Alger, Abdelhak Benchikha alisema kwenye mchezo wa leo hawatocheza kwa kujilinda kwa kucheza nyuma bali watashambulia kama vile wapo nyumbani kwao Algeria.

"Hatuna sababu ya kujilinda kwenye mchezo huu kwa sababu tunatafuta matokeo, hatutokaa nyuma kabisa kwenye mechi hii, tutashambulia kwa sababu sisi ni timu ya mpira,"alisema Benchikha.

Mbali na vita ya makocha hao, pambano la leo ni nafasi nyingine ya straika Fiston Mayele wa Yanga na Khaled Bousseliou wa USM Alger kujiweka pazuri kwenye mbio za Mfungaji Bora wa msimu.

Mayele ndiye kinara akiwa na mabao sita na asisti tatu akifuatiwa na Ranga Chivaviro wa Marumo Gallants iliyotolewa nusu fainali, wakifuatiwa na Khaled aliyefunga manne, huku Zineddine Belaïd wa USMA na Kennedy Musonda wa Yanga wakiwa nyuma yao kila mmoja akifunga mabao matatu.

Mechi ya leo na ile ya marudiano ya wiki ijayo ni sehemu ya wakali hao kuonyeshana umwamba wa kutupia nyavuni ili kutwaa tuzo hiyo ambayo msimu uliopita kwenye michuano hiyo ya Shirikisho ilibebwa na Victorien Adebayor wa US Gendarmerie Nationale ya Niger aliyemaliza na mabao sita.


Sh 155 Milioni

Kiasi cha fedha ambazo Yanga imevuna hadi sasa kupitia ahadi ya Rais Samia kununua mabao CAF

09 Mabao aliyohusika nayo Mayele wa Yanga kati ya 15 iliyofunga tmu hiyio katika Shirikisho Afrika.

05 Idadi ya mabao iliyoruhusu Yanga katika michuano ya Shirikisho Afrika hadi kufika fainali.