Namba za Dube zamfunika Depu, mastaa Simba wakomaliwa
Muktasari:
- Feisal Salum ndiye mchezaji aliyehusika na idadi kubwa ya mabao katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu akiwa na mabao sita ya kufunga na pasi nne za mwisho.
Kuna eneo moja ambalo Prince Dube na Laurindo Dilson ‘Depu’ wanapigana vikumbo kwenye Ligi hivi sasa lakini Dube ameonekana kutamba dhidi ya Depu katika maeneo mengine mawili.
Wawili hao wapo sawa katika mbio za kuwania Ufungaji Bora wa Ligi Kuu msimu huu ambapo hadi sasa, kila mmoja ameshapachika mabao sita kwa mechi ambazo wameichezea Yanga kwenye ligi.
Hata hivyo, Dube ameonekana kuibuka kidedea katika upigaji pasi za mwisho na idadi ya tuzo za mchezaji bora wa mechi kulinganisha na Depu.
Dube ameshapiga pasi tatu za mabao kwenye Ligi Kuu hadi sasa wakati Yanga ikiwa imeshacheza mechi 14 huku Depu akifanya hivyo mara moja.
Ukiondoa takwimu hizo, Dube ameibuka kidedea mbelenya Depu kwa kutwaa idadi kubwa ya tuzo za mchezaji bora wa mechi.
Katika mechi 14 ambazo Yanga imeshacheza hadi sasa, Dube ameshapata tuzo hizo katika mechi tatu huku Depu akichukua mara mbili.
Michezo ambayo Dube ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi ni dhidi ya Singida Black Stars, JKT Tanzania na dhidi ya Coastal Union.
Kwa upande wa Depu yeye ametwaa tuzo hiyo ya Mchezaji Bora wa mechi ni dhidi ya Tanzania Prisons na Namungo.
Ukiondoa hao, wachezaji wengine wa Yanga ambao wametwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi ni Maxi Nzengeli aliyefanya hivyo mara mbili na Djigui Diarra, Mudathir Yahya, Duke Abuya na Mohamed Hussein ambao kila mmoja amaechukua mara moja.
Kwa mara tatu ambazo Dube ameshinda tuzo hiyo ya Mchezaji Bora wa mechi, mshambuliaji huyo anaongoza chati ya wachezaji waliotwaa mara nyingi tuzo hiyo.
Kileleni Dube anaungana na Fabrice Ngoy wa Namungo, Paul Peter (JKT Tanzania) na Kelvin Nashoni wa Pamba Jiji ambao kila mmoja amechukua mara tatu.
Ambao wamechukua tuzo hiyo mara mbili kila mmoja ni Nzengeli, Depu, Peter Lwasa, Libasse Gueye, Salehe Karabaka, Abdulmarick Zakaria, Feisal Salum na Rushine De Reuck.