Profesa Pius Mbawala afariki dunia Muhimbili
Muktasari:
- Profesa Mbawala alifariki jana mchana Juni 23, 2026 baada ya kulazwa hospitalini hapo kwa siku 10 kutokana na matatizo ya presha na kisukari yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Ushirika na Mbunge wa Namtumbo, Profesa Pius Mbawala amefariki dunia wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam.
Profesa Mbawala alifariki jana mchana Juni 23, 2026 baada ya kulazwa hospitalini hapo kwa siku 10 kutokana na matatizo ya presha na kisukari yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwananchi leo, Juni 24, 2026, mtoto wa marehemu, Priscila Mbawala, amesema baba yake alikuwa akiendelea kupatiwa matibabu kabla ya umauti kumkuta.
“Alifariki jana mchana katika Hospitali ya Muhimbili ambako alikuwa amelazwa kwa siku 10. Kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la presha na kisukari,” amesema Priscila.
Amesema msiba unaendelea nyumbani kwa familia eneo la Banana, Dar es Salaam, huku mwili wa marehemu ukitarajiwa kusafirishwa kwenda Namtumbo, mkoani Ruvuma, siku ya Jumamosi kwa ajili ya mazishi.
Priscila ambaye ni mtoto wa nne kati ya watano wa marehemu huyo, amesema mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu katika Wilaya ya Namtumbo baada ya kukamilika kwa taratibu za kuusafirisha mwili kutoka Dar es Salaam kwenda Ruvuma.
“Safari ya kuusafirisha mwili itaanza Jumamosi kuelekea Namtumbo, Ruvuma, na mazishi yatafanyika Jumatatu, kwa sasa maombolezo yanaendelea hapa Banana,” amesema Priscila.
Priscila amesema marehemu ameacha mjane na watoto wa nne, wawili wakike na wanaobakia wakiume.