Kifo cha Mchungaji Msuya kilivyoibua kumbukumbu maisha yake
Muktasari:
- Mchungaji Kiongozi wa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kijitonyama, Eliona Kimaro amesema Mchungaji Sylvanus Msuya alikuwa ushuhuda wa maisha yaliyobadilishwa na imani, elimu na malezi ya kiroho.
Dar/Kilimanjaro. Kifo cha Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga, Sylvanus Msuya, kimeacha simanzi miongoni mwa waumini, viongozi wa dini na watu wengi walioguswa na ushuhuda wa maisha yake.
Baadhi wamekumbuka safari yake ya kutoka kwenye changamoto za maisha hadi kuwa mtumishi wa Mungu aliyegusa maisha ya wengi.
Mchungaji Msuya alifariki dunia jioni ya Jumapili, Julai 26, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rabininsia jijini Dar es Salaam.
Akithibitisha taarifa hizo, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mwanga, Dk Daniel Mono alisema kanisa limepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo hicho na kwamba ratiba ya mazishi itatangazwa baada ya taratibu za kifamilia na za kanisa kukamilika.
"Kwa masikitiko makubwa nawajulisha kwamba mpendwa wetu Mchungaji Sylvanus Abel Msuya ameitwa mbinguni jioni ya leo akiwa anapatiwa matibabu Dar es Salaam. Tupeane pole sote tukiwa na tumaini la ufufuko. Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe," alisema Askofu Mono katika taarifa yake.
Simulizi ya Mchungaji Eliona
Kwa mujibu wa Kanisa la KKKT mwili wa Mchungaji Sylvanus Msuya, utazikwa Alhamisi Julai 30, 2026, Usharika wa Shighatini, KKKT Dayosisi ya Mwanga.
Kifo chake kimeibua tena simulizi ya maisha yake iliyowahi kusimuliwa hadharani Novemba 7, 2024 na Mchungaji wa KKKT, Dayosisi ya Kijitonyama, Eliona Kimaro, ambaye alikuwa mlezi wake kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wa Mchungaji Kimaro, Msuya aliyebarikiwa kuwa Mchungaji rasmi Jumapili Novemba 3, 2024 Dayosisi ya Mwanga, alipitia changamoto nyingi akiwa kijana kabla ya kukabidhiwa kwake na baba yake Mchungaji Abel Msuya na mama yake kwa ajili ya malezi ya kiroho na kimwili, hatua iliyomfungulia ukurasa mpya wa maisha.
Baada ya kuona uwezo wake kitaaluma, Kimaro alimsaidia kuendelea na masomo ya Diploma ya Uandishi wa Habari kati ya mwaka 2011 na 2013, kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Iringa alikohitimu Shahada ya Kwanza ya Uandishi wa Habari mwaka 2016.
Aliendelea na Shahada ya Uzamili ya Mawasiliano ya Umma (Master of Arts in Mass Communication) katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) kati ya mwaka 2017 na 2019, kabla ya kufanya uamuzi wa kuingia katika huduma ya kichungaji.
Baadaye alisoma Shahada ya Theolojia katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, akahitimu na kuwekwa wakfu kuwa mchungaji wa KKKT Dayosisi ya Mwanga.
“Amehitimu na kubarikiwa kuwa mchungaji macho yangu yakiona, namshukuru sana Mungu,” aliandika Mchungaji Kimaro katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook.
Akizungumza kuhusu msiba huo, Mchungaji Kimaro amesema kifo hicho kimemuumiza kwa sababu alimlea kwa miaka mingi na kushuhudia hatua zote za ukuaji wake.
"Kwa masikitiko makubwa sana ninatoa pole nyingi kwetu sote kufuatia kutwaliwa kwa Mchungaji Sylvanus Abel Msuya kutoka katika maisha haya. Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha yake hapa duniani. Ninawaombea faraja ya Roho Mtakatifu mke wake, watoto, familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu," amesema.
Ameeleza kuwa Msuya alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa nimonia kwa takribani miezi mitatu na alikuwa amelazwa hospitalini mara kadhaa huku hali yake ikionekana kuimarika kabla ya kuzidiwa ghafla wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa Kimaro, baada ya hali yake kubadilika alipelekwa katika hospitali moja kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rabininsia, ambako alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), lakini alifariki dunia akiwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Waumini wamlilia
Mbali na huduma yake madhabahuni, Msuya alijulikana kwa kushiriki mahubiri, mafundisho na ushuhuda wa maisha yake, hususan jinsi alivyoondokana na changamoto mbalimbali na kuanza maisha mapya kupitia imani ya Kikristo.
Baada ya taarifa za kifo chake kusambaa, mamia ya waumini na watu waliowahi kukutana naye walitumia mitandao ya kijamii kutoa salamu za rambirambi, wakieleza namna walivyoguswa na huduma na maisha yake.
Abad Beatrice amesema ingawa hakuwahi kumfahamu binafsi, ushuhuda wa Msuya kuhusu changamoto alizopitia ulimgusa sana.
"Clip yake ya ushuhuda kuhusu matumizi ya dawa za kulevya ilinitoa machozi. Alikuwa hazina kubwa kwa watoto na vijana wenye changamoto za uraibu. Tumepoteza mtu muhimu," amesema.
Kwa upande wake, Alfred Rick amesema anamkumbuka Msuya tangu akiwa kijana alipofikishwa kwa Mchungaji Kimaro kutokana na changamoto za maisha.
"Uliamua kuwa mlezi wake mpaka akawa mchungaji. Hakika duniani hatuna mji udumuo," amesema.
Waumini wengine, akiwemo Daniel Mritines, Emanuel Laabdi, Casey Mtei na Fredrick Nwaka, walikumbuka mahubiri yake, huduma katika usharika mbalimbali wa KKKT pamoja na vipindi vya kiroho alivyoshiriki, wakisema maisha yake yalikuwa ushuhuda unaowapa wengi matumaini kuwa inawezekana kubadilika na kuanza upya.
Wengi wameeleza kuwa urithi mkubwa aliouacha Mchungaji Sylvanus Msuya haukuwa tu katika mahubiri yake, bali pia katika maisha aliyoyaishi, yaliyodhihirisha nguvu ya malezi, elimu na imani katika kubadilisha hatima ya mwanadamu.
Wakati familia na kanisa wakiendelea na maandalizi ya mazishi, waumini wameendelea kuomboleza wakishikilia maneno yaliyotolewa na viongozi wa kanisa.
Walichokisema wachungaji
Baadhi ya Wachungaji wa Dayosisi ya Mwanga wasema kifo cha Mchungaji Msuya ni pigo kwa kanisa hilo kwa kuwa alikuwa ni mchungaji kijana aliyekuwa na ushawishi wa kipekee kwa vijana wenzake.
Mchungaji wa Usharika wa Mamba, Ugweno, Anituja Msuya amesema wamepoteza mchungaji ambaye alikuwa na uthubutu, mwenye upendo, muwazi na ambaye alikuwa hapindishi jambo.
"Ni kijana mchungaji ambaye alikuwa bado hajatimiza ndoto yake aliyoitaka maana huu ndio mwaka wake wa pili wa kutumika. Tutamkumbuka kwa upendo wake na uthubutu wake. Hata kama jambo ni gumu yeye alithubutu kulitenda," amesema Mchungaji huyo.
"Alikuwa ni mkweli na alikuwa hapindishi jambo, alikuwa ni muwazi. Tutamkumbuka kwa ucheshi wake, uwazi wake, uthubutu wake na upendo wa dhati aliokuwa nao kwa wengine."
Naye Mchungaji wa Usharika mteule wa Kifaru, Charles Tenga amesema ameondoka katika kipindi ambacho walimtegemea kwa mengi kutokana na vipaji alivyokuwa navyo.
"Ni mchungaji kijana ambaye alikuwa na vipaji vingi ambapo baada ya kuondoka na kwenda Dar es Salaam tulitegemea angerudi haraka na kuendelea na huduma kama kawaida lakini tukasikia amepata shida ya kuugua ghafla na kupelekwa hospitalini. Wakati tunaendelea kuuliza anaendeleaje tukapata taarifa ya msiba," amesema Mchungaji Tenga.
"Tutamkumbuka sana katika masuala yake ya uimbaji, mhamasishaji mzuri katika dayosisi yetu maana tulikuwa tumeshamuweka tena katika kitengo cha utunzaji wa taarifa mbalimbali kutokana na fani yake, ambayo alikuwa ameisomea. Tutamkumbuka sana."