Prime
Chanzo cha upinzani Yanga, Azam chafichuka
Julai 27, 2008 Azam FC ilipanda daraja kushiriki ligi kuu. Ilikuwa baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Majimaji ya Songea, kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Siku hiyo hiyo jijini Dar es Salaam, kwenye uwanja wa Taifa, ilitakiwa kuwe na mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba, kuwania nafasi ya tatu ya Kombe la Kagame.
Lakini Yanga hakutokea uwanjani akatoka nduki.
TFF chini ya Leodeger Tenga, ikaifungia Yanga kushiriki mashindano ya kimataifa kwa misimu mitatu.
Viongozi wa Yanga wakalalamika kwamba wanasajili wachezaji wakubwa wa kimataifa ili washindane kimataifa.
Wakifungiwa maana yake wachezaji hao wataishia kucheza mashindano ya ndani tu na akina Azam!
Yaani tusajili wachezaji wakubwa halafu tuishie kucheza na akina Azam, kweli?
Yaani waliitaja Azam kwa udogo na dharau kubwa.
Na hata katika msimu wake wa kwanza, Azam FC ingeweza kushuka daraja.
Ilikuwa Aprili 07, 2009, Yanga ikitoka kuwa bingwa wa ligi kwa kuwafunga Toto Afrika 2-1, huku Azam FC ikipigania maisha katika mchezo huu.
Hadi mapumziko Yanga wakawa wanaongoza 2-0 na kuashiria kwamba Azam FC wanashuka.
Lakini 'comeback' ya hatari ya kipindi cha pili ilitosha kuipa Azam FC alama tatu na kuihakikishia maisha kwenye ligi kuu.
Kipa wa Yanga, Juma Kaseja aliokoa penalti mbili za Azam FC siku hii, hata hivyo, Azam wakapona!
Lakini haikuchukua muda picha ikaanza kubadilika.
Ilikuwa 2010 pale Azam FC ilipomsaini nyota bora zaidi wa Yanga wakati huo, Mrisho Ngassa.
Alikuwa kipenzi cha mashabiki na kuondoka kwake kulivunja nyoyo zao.
Hapo ndipo Yanga walipoanza kujenga hisia hasi kwa Azam na ndio mwanzo wa uhasama huu.
Ikaja mechi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu, msimu wa 2011/12.
Yanga walifungwa 3-1 katika mchezo ambao wachezaji wao wawili; Haruna Niyinzima na Nadir Haroub 'Cannavaro' walioneshwa kadi nyekundu pamoja na Jerry Tegete ambaye alikuwa benchi.
Mchezo huu ni maarufu zaidi kwa wachezaji wa Yanga kumpiga mwamuzi, Israel Nkongo.
Ingia YouTube kisha andika, 'Referee beaten in Tanzania', itakuja video ya tukio hilo.
Mechi hii iliwaharibia sana Yanga ambao walikuwa wanawania ubingwa.
Mchezo uliofuata dhidi ya Coastal Union, walishinda lakini wakanyang'anywa alama kwa kumchezesha Cannavaro ambaye alioneshwa kadi nyekundu.
Msimu ukaharibika mkosi ulioanzia kwenye mechi ya Azam chuki ikaongezeka.
Mrisho Ngassa aliyeanzisha vita hii mwaka 2010, akaja kuongeza ukakasi miaka miwili baadaye mwaka 2012.
Ilikuwa kwenye Kombe la Kagame, 2012, mchezo wa nusu fainali, Azam FC dhidi ya AS Vita.
Wakiwa nyuma 1-0, Azam wakamuingiza Ngassa kutokea benchi akasawazisha na kutengeneza bao la ushindi kwa John Bocco.
Mpira ulipoisha, akapewa jezi ya Yanga na mashabiki wao, akaivaa.
Hii iliashiria kwamba Ngassa bado ana mapenzi na Yanga Azam wakaamua kumuuza.
Yanga wakiamini atarudi kwao, akauzwa kwenda Simba, ikawauma tena.
Wakaiona Azam kama timu ya kuwaumiza hisia zao, kwa kuwanyima kipenzi chao na kumpeleka Simba.
Yaani Azam ni wakala wa Simba katika kuihujumu Yanga, chuki ikaongezeka.
Kuanzia mwaka 2012 hadi 2016, Azam wakawa wapinzani wakuu wa Yanga kwenye mbio za ubingwa hapo ndipo vita ilipokuwa zaidi.
Simba alikuwa dhoofu sana hadi kutajwa kama mtani wa jadi wa Yanga, lakini mpinzani ni Azam.
Msimu wa kwanza, 2012/14, Yanga wakawa bingwa kwa kuwazidi Azam alama sita ambazo ni za mechi baina yao.
Yanga walishinda mechi zote mbili, huku Azam wakilalamika walionewa na waamuzi, chuki ikazidi kukua
Msimu wa 2013/14 Azam FC wakawa mabingwa.
Kuelekea mafanikio hayo, walishinda mechi sita mfululizo za ugenini.
Kocha msaidizi wa Yanga wakati huo, Charles Boniface Mkwassa akalalamika kwamba haiwezekani timu kushinda mechi nyingi namna hiyo ugenini, Azam wachunguzwe.
Kauli hii ikapokelewa na mashabiki wa Yanga na kupiga sana kelele na kuifanya Azam kutajwa zaidi na Yanga, kuliko watani wao Simba, Azam ikazidi kukua.
Uhamisho wa Frank Domayo na Didier Kavumbagu mwaka 2014, uliongeza mafuta kwenye moto huu wa upinzani.
Domayo, kipenzi cha Wanayanga, alisainiwa na Azam FC akiwa kwenye kambi ya tkmu ya taifa.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi, akasema hii haikubaliki na akaunda tume maalumu kuchunguza iliwezekanaje?
Malinzi ambaye zamani alikuwa katibu mkuu wa Yanga, alisahau kama hata Yanga walimsaini Domayo akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa.
Tume yake haikuwa kutoa majibu hadi leo, lakini Yanga waliumia sana na chuki ikaongezeka.
Yanga na Azam waliendelea kushindania ubingwa hadi 2017 pale nyota kadhaa wa Azam walipohamia Simba.
Simba ikaimarika na kutawala ligi, huku Azam na Yanga wakihamishia vuta yao kwenye kuwania nafasi ya pili.
Vita hii ilipiganwa kuanzia 2018 hadi 2021.
Kuanzia 2022, Yanga walijipata na kuwapiku Simba kwenye ubingwa.
Hata hivyo, mwaka huohuo vita ikaibuka tena, sakata la Feisal Salum.
Kipenzi cha Wanayanga, mzee wa byuti byuti, aliamka tu asubuhi na kusema hataki tena kuitumikia Yanga
vita ikawa kubwa, hadi rais wa nchi,Samia Suluhu Hassan, akaingilia kati, Feisal akatua Chamazi mwaka 2023.
Hii iliwauma sana Yanga na kujiapiza kulipa kisasi.
Mwaka 2024, wakamuiba kipenzi cha Azam, Prince Dube, na mzani kubalansi.
Wachezaji wengine waliochochea uhasama wa Yanga na Azam.
1. Salum Abubakary 'Sure Boy '
Alijiunga na Azam FC mwaka 2007 akitokea Friends Rangers ya Manzese.
Ni mmoja wa wachezaji walioipandisha daraja Azam FC.
Lakini historia ya baba yake kuitumikia Yanga ilimfanya ahusishwe nao kwa miaka mingi.
Mwaka 2020 kwa mara ya kwanza akatamka kwamba anataka kuondoka Azam FC.
Tetesi zikasema anataka kwenda Yanga. Hii ikawashtua Azam FC na kukaa naye kujua nini kinamsibu shujaa wao, alama yao.
Wakayamaliza na akaongeza mkataba, akabaki.
Septemba 2021 yeye na waandamizi wenzake wawili, Aggrey Morris na Mudathir Yahya, wakafungiwa na Azam FC kwa utovu wa nidhamu.
Desemba wakafunguliwa lakini yeye akakataa kurudi, Januari 2022 akajiunga na Yanga, neno likatimia!
2. Mudathir Yahya
Alijiunga na akademi ya Azam FC mwaka 2011, baada ya kuonwa kwenye mashindano ya Copa Coca-Cola akiwa na timu ya Mjini Magharibi ya Zanzibar.
Akakaa akademi hadi 2014, alipopandishwa timu kubwa na kudumu nayo hadi 2022.
Tofauti na mwenzake Sure Boy, yeye alikubali kurudi baada ya ile adhabu.
Lakini alikataa kusaini mkataba mpya na kuamua kurudi kwao Zanzibar alikokaa nusu msimu bila timu.
Dirisha dogo la 2022/23 akajiunga na Yanga.
Akiwa Jangwani, akawa na tabia ya kushangilia mabao yake kwa kupiga simu.
Hii ikaleta tafsiri kwa watu kuwa anawatupia kijembe Azam, kwamba aliambiwa atapigiwa simu lakini akatelekezwa.
Japo tafsiri hii haikuwa kweli, lakini iliongeza chachu ya upinzani.
3. Ninju
Ni bwana mdogo mwenye kipaji kikubwa kutoka akademi ya Azam FC.
Alijiunga nayo mwaka 2022 akitokea Zanzibar na akakaa akadeki hadi Januari 2025 akatolewa kwa mkopo kwenda JKU ya Zanzibar ili kupata uzoefu.
Akiwa huko akashiriki Kombe la Muungano na kung'ara.
Timu yake ilifika fainali na kukutana na Yanga, akaubonda mwingi sana, hadi viongozi wa Yanga wakamfuata na kupiga naye picha.
Kumbe haikuishia picha tu, wakamsaini kimya kimya na Julai 2025 wakamtangaza.
Azam FC wakalalamika kwa TFF na Yanga wakakutwa na hatia, wakatakiwa kuwalipa Azam.
Haya yote yakachochea uhasama na kuifanya mechi baina ya Azam FC na Yanga kuwa kubwa kama ilivyokuwa jana.