Mechi ya sura mbili
Muktasari:
- Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge amesema kuwa anaamini mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa.
Azam inaikaribisha Yanga leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 usiku katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC ambao matokeo yake yatakuwa na sura mbili tofauti.
Jambo la kwanza ni mbio za ubingwa wa ligi ambapo kama Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 35 ikipata ushindi leo, itafanya pengo la pointi baina yake na Azam FC kufikia 11 jambo ambalo hapana shaka litazidi kuipunguzia Yanga upinzani katika mbio za ubingwa.
Lakini kama Azam FC yenye pointi 27 itapata ushindi, itapunguza pengo la pointi kati yake na Yanga kubakia pointi tano, jambo ambalo angalau litaendelea kuweka hai matumaini yake ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Jambo la pili ambalo litatazamwa baada ya matokeo hayo ni kisasi ambacho Azam FC itakuwa na hamu ya kulipa kwa Yanga baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo zilizopita baina yao, mojawapo ikiwa ni ya Kombe la Mapinduzi.
Kwa upande wa Yanga, hapana shaka wanaingia wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu uliopita, matokeo ambayo yaliwafanya washindwe kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza idadi kubwa ya mechi ambapo kabla ya kukutana ilikuwa haijapoteza michezo 18.
Kumbukumbu ya mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo mbili, inaonyesha Yanga ni mbabe ambapo imepata ushindi mara sita, Azam FC ikishinda michezo minne na zimetoka sare mara moja.
Katika mchezo wa leo, Azam FC hapana shaka itaingia ikimtegemea zaidi Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye hadi sasa ndiye mchezaji aliyehusika na idadi kubwa ya mabao katika Ligi Kuu ya NBC akifanya hivyo mara 10 ambapo amefunga mabao sita na kupiga pasi nne za mwisho.
Yanga wao jina ambalo wanategemea zaidi leo liwape furaha ni mshambuliaji Laurindo Dilson 'Depu' ambaye amehusika na mabao saba hadi sasa, akifunga sita na kupiga pasi moja ya mwisho.
Ni mchezo unaokutanisha wachezaji sita ambao kwa nyakati tofauti wamezichezea timu hizo zote mbili.
Katika kikosi cha Azam FC, yupo Feisal Salum 'Fei Toto' aliyewahi kuitumikia Yanga kabla ya kuhamia katika kikosi chake.
Wachezaji wa Yanga ambao walipita katika nyakati tofauti ndani ya Azam FC ni Mohamed Hussein, Prince Dube, Mudathir Yahya, Farid Mussa na Salum Abubakar 'Sure Boy'.
Hata hivyo, ni Mohamed Hussein, Prince Dube na Mudathir Yahya ambao wamekuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha Yanga kwani Sure Boy na Faridi Mussa wamekuwa wakisotea benchi.
Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kuwa mchezo huo ni mgumu lakini wamejiandaa kushinda.
"Kuhusu mechi, tunakabiliana na Azam miongoni mwa timu imara katika ligi na walikuwa na kiwango bora katika mashindano ya Klabu Afrika. Itakuwa ni fursa nzuri kucheza katika uwanja mzuri wenye eneo zuri la kuchezea.
"Wachezaji wapo katika hali nzuri na kiwango chao cha kujiamini kipo juu tayari kwa mchezo wa kesho (leo)," alisema Goncalves.
Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge amesema kuwa anaamini mechi hiyo itakuwa na ushindani mkubwa.
"Tuna furaha kucheza mechi zenye ushindani. Naamini utakuwa mchezo mzuri na sisi tuna furaha kucheza michezo kama hii," alisema Ibenge.