Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Lock ya fingerprint’ kwenye simu inavyoweza kukusababishia haya…

Muktasari:

  • Moja ya changamoto za kutumia mfumo wa alama za vidole (fingerprint) katika simu ni uwezekano wa mtu asiyehusika kupata ufikiaji wa kifaa chako bila ridhaa yako, hasa ukiwa umelala au hujitambui ambapo anaweza kuchukua kidole chako na kukiweka kwenye kihisi cha alama za vidole ili kufungua simu kwa urahisi, tofauti na nenosiri au PIN ambayo huhitaji mtumiaji kuingiza kwa hiari.



Dar es Salaam. Licha ya teknolojia ya utambuzi wa alama za vidole ‘fingerprint’ kuendelea kuwa sehemu muhimu ya simu za kisasa ikiwapa watumiaji njia rahisi na ya haraka ya kufungua vifaa vyao bila kutumia nenosiri, kwa namna moja au nyingine inaweza isiwe bora kwenye faragha au uhusiano wa kimapenzi kwa wenza wasio waaminifu.

Pamoja na manufaa yake katika usalama wa taarifa, matumizi ya teknolojia hiyo yamekuwa na mjadala kuhusu athari zake ambapo katika miaka ya karibuni, watengenezaji wa simu wamekuwa wakiboresha mifumo yake ili kuongeza usalama wa taarifa za watumiaji.

Ikumbukwe tofauti na nenosiri ambalo linaweza kusahaulika au kuibiwa, alama za vidole ni za kipekee kwa kila mtu na ni vigumu kuigwa.

Tafiti, machapisho na wataalamu wa usalama wa mtandao wanasema matumizi ya fingerprint hupunguza hatari ya watu wasiostahili kupata taarifa binafsi zilizohifadhiwa kwenye simu, ikiwemo picha, ujumbe, taarifa za benki na nyaraka muhimu.

Faida nyingine ni urahisi wa matumizi. Mtumiaji huhitaji kugusa tu sehemu maalumu ya simu ili kuifungua badala ya kuandika nambari au nenosiri kila wakati. Hali hiyo huongeza kasi ya matumizi na kuboresha uzoefu wa mtumiaji.

Aidha, baadhi ya programu za kifedha na benki hutumia fingerprint kuthibitisha miamala, jambo linaloongeza ulinzi dhidi ya utapeli na wizi wa kidijitali.


Hasara zake

Katika usalama wa taarifa zako fingerprint inaweza isiwe bora hasa inapokuja suala la kutolewa kinguvu kutoka kwa watu wanaotaka taarifa zako, mwenza asiye mwaminifu kuona taarifa zako hasa pale unapokuwa umelala hivyo kuleta migogoro.

“Niliwahi kugombana na mpenzi wangu hadi tukatengana baada ya kuona nina uhusiano na mwanamke mwingine. Aliona nilipokuwa nimelala akachukua simu akagusisha kidole ikafunguka akaona madudu yote,” anasema kijana mmoja kutoka Dar es Salaam aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Anasema kuanzia hapo haamini tena na hatumii badala yake amekuwa akiweka neno la siri.

Upo utafiti wa mwaka 2024 wenye kichwa cha habari ‘Privacy or Transparency? Negotiated Smartphone Access as a Signifier of Trust in Romantic Relationships’ uliochapishwa kwenye majarida mbalimbali ya masuala ya kifamilia,  uliochunguza namna wanandoa na wapenzi wanavyoshirikiana ufikiaji wa simu zao.

Watafiti waligundua wanandoa wengi huruhusiana kufungua simu za wenzao, lakini huwa na mipaka ya matumizi ya ruhusa hiyo. Utafiti huo ulionyesha suala la kufikia simu ya mwenza linahusishwa moja kwa moja na imani, uwazi na faragha.

Jambo la kuvutia ni kwamba watafiti waligundua hakuna makubaliano ya pamoja kuhusu kiwango sahihi cha uwazi katika mahusiano. Kwa baadhi ya watu, kumpa mwenza fingerprint ya simu ni ishara ya kuaminiana, wakati kwa wengine ni uvamizi wa faragha. Kilichoonekana kukubalika zaidi ni kwamba ufikiaji huo uwe wa hiari na wa makubaliano ya pande zote.

Hata hivyo, baadhi ya watu huona kutokuwa na fingerprint ya mwenza wao kwenye simu kama ishara ya kuficha siri, hali inayoweza kuzua migogoro hata pale ambapo hakuna tatizo halisi.

Hata hivyo, endapo taarifa za alama za vidole zitaibiwa kupitia mbinu za hali ya juu za udukuzi, mtumiaji hawezi kubadilisha alama zake za vidole kama ilivyo kwa nenosiri. Hivyo, madhara yanaweza kuwa ya muda mrefu.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la Symmetry mwaka 2019 ulieleza mfumo wa fingerprint una kiwango kikubwa cha usahihi katika utambuzi wa mtumiaji na ndiyo sababu umetumika sana kwenye simu, benki na mifumo mingine ya kidijitali.

Ingawa hakuna mfumo wa fingerprint wenye usalama wa asilimia 100, na changamoto kama udukuzi wa taarifa za biometriki na matumizi ya alama bandia bado zipo.

Utafiti mwingine wa mwaka 2024 wa Science direct ulionesha watu wengi wanaamini fingerprint ni njia salama na rahisi ya kulinda simu zao, lakini bado wana wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya taarifa zao za biometriki na uvunjifu wa faragha.

Kwa ujumla, fingerprint imeleta mapinduzi katika usalama wa simu na kurahisisha matumizi ya teknolojia za kidijitali. Hata hivyo watumiaji wanapaswa kuzingatia mipaka ya faragha, kutumia mbinu nyingine za ziada za usalama na kufanya maamuzi ya busara wanaposhirikisha wengine ufikiaji wa vifaa vyao.