Prime
Zungu aibua mjadala upya mashangingi ya vigogo, atoa maagizo
Dodoma/Dar. Wakati Serikali ikipata kigugumizi kutekeleza ahadi yake ya kubana matumizi, hususan kwenye matumizi ya magari ya kifahari, Spika Mussa Zungu amesema hilo kwa sasa linapaswa kufanyika kwa vitendo na Bunge litafuatilia utekelezaji wake.
Mara kadhaa, Serikali kupitia mawaziri imekuwa ikitoa kauli ndani na nje ya Bunge kuhusu kupunguza matumizi ya magari ya kifahari, ikiwemo iliyotolewa mwaka 2022 na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Hata hivyo, utekelezaji wa ahadi hiyo ya Dk Mwigulu ambaye sasa ni Waziri Mkuu, umekuwa ukisuasua na magari ya kifahari maarufu kama mashangingi yameendelea kununuliwa na kuitafuna keki ya taifa, huku mijadala ikiendelea kuibuka, nani anaruhusu magari hayo kununuliwa au nani anayeshindwa kuyakomesha.
Zungu akijenga hoja yake kwa takwimu halisi, amelieleza Bunge kuwa mashangingi hayo yanayotumiwa na viongozi wa ngazi mbalimbali yanatafuna mabilioni ya shilingi ambayo yangeweza kutumika maeneo mengine muhimu.
Si spika pekee, hata Mbunge wa Nyasa (CCM), John Nchimbi aliyewahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, hivi karibuni alisema bungeni, kuwa eneo la matumizi ya magari serikalini inatumia fedha nyingi na ni wakati mwafaka iangaliwe upya.
Baadhi ya viongozi wanaotumia magari ya kifahari ni mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu, wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala wa mikoa (RAS) na wilaya (DAS), wakurugenzi wa halmashauri (DED), mameya na makamanda wa polisi.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar wakati akihitimisha Bajeti ya Serikali 2026/27 licha ya kuzungumzia kubana matumizi ya Serikali kwa kudhibiti safari za ndani na nje ya nchi pamoja na kupunguza semina, warsha na makongamano, hakuzungumzia suala la magari.
Alisema mifumo ya ukaguzi wa ndani, udhibiti wa matumizi na usimamizi wa fedha za umma, itaendelea kuimarishwa ili kuzuia upotevu wa rasilimali za Taifa.
Hata hivyo, Waziri wa zamani ambaye kwa sasa ni mbunge akizungumza na Mwananchi, amesema kauli ya Spika Zungu ina mashiko isipokuwa usimamizi katika utekelezaji wa maagizo ya Bunge ndio mgumu.
Mbunge huyo ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe, ameeleza mara nyingi mipango inakuwa mizuri lakini unapofika wakati wa kusimamia utekelezaji wake watu wanajisahaulisha na kuishia kufanya kazi za mazoea.
Kauli ya Zungu
Akizungumza leo Alhamisi Juni 25, 2026 bungeni, Zungu amesema mwaka 2013 Kamati wa Bajeti ilibaini katika kipindi cha miaka mitatu pekee, takribani Sh1.8 trilioni zilikuwa zimetumika kuhudumia magari ya Serikali, bila kujumuisha gharama za manunuzi ya magari hayo.
Kiasi hicho, amesema ni kikubwa kingeweza kujenga mamia ya shule, vituo vya afya, miradi ya maji au kusaidia utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Kauli ya Zungu imekuja wakati Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa tayari ametangaza kuanza kubana matumizi, hasa kwa upande wa mafuta, kwa kupunguza ukubwa wa misafara yake.
Aprili 8, 2026, Rais Samia akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi Ikulu ya Chamwino, Dodoma alisema ni umuhimu taasisi za umma kuanza kuchukua hatua za makusudi kupunguza gharama zisizo za lazima.
“Ndani ya Serikali tuna matumizi makubwa sana ya mafuta, magari ni mengi, safari zetu ni nyingi, niwaombe sana tuanze kupunguza matumizi ya mafuta na ninaanza na ofisi yangu.
“Kuanzia sasa, ninapokwenda popote, maofisa wote nitawaingiza kwenye kibasi kimoja. Msafara utakuwa na eskoti yangu, polisi na gari ya akiba nyuma. Wanaobakia wote wataingia kwenye kibasi ili kupunguza matumizi ya mafuta," alisema Rais Samia.
Mbali na mafuta, moja ya Spika Zungu inagusa magari ‘ya anasa’ kwa ujumla, ambayo amesema hayaendani na uhalisia, kwa kuwa ni moja ya maeneo yanayomaliza fedha nyingi wakati nchi bado ni masikini.
Sasa swali kubwa linaloibuka ni kama taasisi na viongozi wengine wa Serikali wako tayari kufuata mfano huo ili fedha zinazotumika zielekezwe kwenye maeneo yenye tija Zaidi, hasa kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania.
Jambo jingine huenda tatizo si idadi ya magari pekee, bali gharama za kuyatunza, uendeshaji, mafuta, matengenezo, madereva na ununuzi wa magari mapya kila baada ya muda.
Hata hivyo, akijenga hoja yake, Zungu ametolea mfano jinsi matumizi ya magari hayo yanavyotafuna fedha, akitaja namna Kamati ya Bajeti ya mwaka 2013 iliyokuwa chini ya Andrew Chenge ilivyobaini fedha nyingi za kugharamia magari.
Baadhi ya wajumbe waliounda kamati hiyo ni Zungu (Spika), Beatrice Shelukindo, Christina Lisu, Dk Mwigulu (Waziri Mkuu), Luhaga Mpina, Hamad Rashid na James Mbatia.
Zungu amesema fedha zinazookolewa kutokana na kupunguza matumizi ya magari na misafara zinaweza kuelekezwa katika kuboresha huduma za jamii na kuongeza upatikanaji wa dawa hospitalini.
Pia, zinaweza kujenga madarasa, kuimarisha upatikanaji wa maji safi na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
Kutokana na hilo, Zungu amewataka viongozi wa Serikali kuiga mfano wa Rais Samia kubana matumizi kwenye magari, akisema yeye pia atakuwa ataku wa mtu wa pili baada ya mkuu huyo wa nchi.
“Rais Samia ameonyesha mfano wa kupunguza misafara yake, ninyi wengine mnasubiri nini? Kuanzia sasa mtaona gari nitakayotumia mimi itabadirika siyo ile mliyozoea,” amesema Zungu na kuongeza:
“Hatuwezi kuendelea na matumizi ya magari ya anasa wakati nchi yetu bado ni masikini, matumizi ya Serikali yapungue na kama Rais mwenyewe ameonyesha mfano kwa nini nyie,” ameeleza.
Zungu amemkumbusha Waziri Mkuu Nchemba kuwa, alipokuwa Waziri wa Fedha, bajeti yake ya kwanza alitangaza suala la kubana matumizi lakini akahoji mpango huo uliiishia wapi.
Amesema kamati hiyo ilibaini fedha zilizotumika kuhudumia magari ya Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu katika matunzo, ununuzi wa mafuta na matengenezo pekee zilikuwa Sh1.8 bilioni.
Akichanganua, amesema mwaka 2008/2009 Serikali ilitumia Sh685 bilioni, mwaka 2009/2010 (Sh530 bilioni) na mwaka 2010/2011 zilitumika Sh537 bilioni.
Sera ibadilike
Akizungumzia hilo, Mtaalamu wa uchumi, Charles Matekele kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma amesema taarifa mbalimbali zinaonyesha kwenye taasisi za Serikali kuna asilimia kubwa ya matumizi ya dizeli na petroli katika shughuli za kila siku.
Matekele amesema kubana matumizi kungekuwa na maana zaidi iwapo watahama kutoka kwenye matumizi ya dizeli na petroli kwenda katika nishati safi ya gesi na magari ya umeme.
“Matumizi ya dizeli na petroli ni makubwa kwa taasisi za Serikali, wakihama na kuingia kwenye gesi na umeme, kutakuwa na ahueni kubwa ya kupungua kwa matumizi na kuokoa fedha,” amesema Matekele.
Mbali na hilo, Matekele amesema Serikali inapaswa kubadilisha sera itakayowezesha watendaji wa mijini kutumia magari ya gharama kubwa tofauti na wale waliopo katika halmashauri za vijijini ambako kuna changamoto miundombinu ya barabara.
“Dhana ya kubana matumizi iendane na mabadiliko ya sera kuanzia magari yanayotumika, ingawa ni vigumu lakini lazima tumeze, hata kwa wakuu wa idara tatu kutumia gari moja ili nchi ijitegemee na kupunguza matumizi na fedha zitakazookolewa zitatumika katika shughuli nyingine za maendeleo,” amesema Matekele.
Mmoja wa madereva wa Serikali jina limehifadhiwa amesema ili kubana matumizi ni Serikali kuweka utaratibu wa kutonunua magari ya kifahari ambayo yana gharama kubwa.
“Kupunguza matumizi ya magari si katika kuendesha, matengenezo au kulihudumia, bali katika manunuzi, Prado unanunua kwa Sh150 milioni, Land Cruiser V8 unanunua kwa Sh500 milioni.
“Binafsi sioni utofauti wa gharama za uendeshaji wa Prado au V8, zote zipo sawa hata ukienda ‘services’ gharama zake hazipishani. Hata kukiwa na safari ya umbali Fulani ukiweka mafuta ya Sh200,000 wote mnafika,” ameeleza.
Kwa mujibu wa dereva huyo, kinachokula mafuta katika magari ya Serikali ni mwendokasi wa baadhi ya madereva, jambo ambalo ni gumu kulidhibiti kutokana na presha za mabosi wao.
“Mfano kikao kikiishi, mkitoka tu nje unaambiwa changamsha mwendo. Sasa ukikimbiza gari lazima mafuta yaende mengi, tofauti ukienda katika mwendo wa kawaida,” amesema dereva huyo.
Dereva mwingine amesema magari ya Serikali hasa Land Cruiser VXR 300 yana gharama kubwa na yanatakiwa kunyenyekewa kama mtoto mdogo.
“Ikitokea umevunja chuma au kitu chochote kwenye gari inakuwa shida, mfano taa moja unaweza ukaambiwa Sh6 milioni au Sh8 milioni. Hata breki zake zinauzwa Sh300, 000 wakati magari ya kawaida Sh45,000 unapata,” amesema.
Ili kuendana na zana ya kubana matumizi, dereva huyo anaungana na mwenzake akiitaka Serikali kupunguza ununuzi wa magari ya namna hiyo na si vinginevyo.
“Shida inakuja utampandisha waziri kwenye Land Cruiser hardtop’ je itawezekana? Hakuna atakayekuelewa, ila magari yana gharama kubwa,” amesema.
Ianzie kwa wabunge
Aprili 2, 2026, akichangia mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2026/27, mbunge wa Nyasa, John Nchimbi alisema Iangaliwe aina ya magari yanayotumika na kazi anazozifanya mtumishi. Utakuta mtumishi yeye ni mkurugenzi tena hapa hapa Dodoma na kazi zake hazimlazimu kutoka nje ya mkoa lakini anatumia gari la Sh480 milioni,” alisema.
“Kwa nini anatumia gari la gharama hiyo wakati haendi mbali? Serikali inatumia magari aina ya V8 zaidi ya 400, wakati kuna wengine hawakupaswa kuyatumia hayo,” amesema.
Nchimbi amefafanua kuwa hata hao wanaotumia V8 sasa hivi kuna tatizo la mafuta, lakini madereva wa magari wanayawasha kuanzia asubuhi hadi jioni yakisubiri viongozi.
“Unajiuliza hawa wanajua kama haya mafuta yananunuliwa kwa dola? Lakini ni gharama ya Serikali, mtu anangurumisha gari kuanzia asubuhi hadi mchana akimsubiri bosi wake ili lisipate joto,” amesema.
Mbunge huyo, amesema kama wabunge wanataka kudhibiti matumizi ya Serikali lazima yaanzie kwa viongozi wakiwemo wabunge hasa kwa magari wanayoyatumia.
Amesisitiza ni wakati muafaka kwa kuwekwa utaratibu wa udhibiti wa matumizi kuanzia mtu mmoja mmoja hadi serikalini ili kubana matumizi yatakayowezesha kuokoa fedha zitakazorudi kwa wananchi kupeleka maendeleo.
Ahadi ya Mwigulu 2022
Mwaka 2022 akisoma bajeti ya Wziara ya Fedha, Dk Mwigulu alisema sera ya Serikali kuelekea mwaka wa fedha 2022/23 itakuwa kubana na kuondoa matumizi yasiyokuwa na ulazima.
Dk Mwigulu alifafanua ili kutimiza azma hiyo, Serikali inatarajia kudhibiti ununuzi na matumizi ya magari kwa kuzingatia Waraka wa Rais Namba 1 wa mwaka 1998 kuhusu hatua za kubana matumizi ya Serikali.
“Pia, waraka mkuu wa utumishi wa umma namba 2 wa mwaka 2021, ni kuhusu utaratibu wa kutumia magari, aina za staili ya magari kwa viongozi wa umma ili kubana matumizi,” alisema.
“Baadhi ya maeneo yenye gharama kubwa sana kwa Serikali ni ununuzi wa magari, vipuri, mafuta, uendeshaji na matengenezo. Tumepanga kuchukua hatua za muda mfupi na mrefu ili matumizi ya Serikali na utumishi wa umma yaakisi ugumu wa maisha wanaopitia wananchi,” alisema Dk Mwigulu.
Mwaka huohuo, waziri huyo fedha alisema: “Kwa sasa, Serikali ina magari zaidi ya 15,742, pikipiki 14,047 na mitambo 373 na inatumia zaidi ya Sh558 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa magari, mafuta ya uendeshaji, vipuri na matengenezo ambapo kwa sasa ni zaidi ya Sh 500bilioni,” alisema.
Katika kukazia hilo, Dk Mwigulu alisema Serikali itaondoa utaratibu uliozoeleka wa dereva anapitishwa chini, bosi anapanda ndege hadi Mwanza au Mbeya kutoka Dar es Salaam na kurudi hivyo hivyo.
“Zaidi ya Sh500 bilioni zitaokolewa na kuelekezwa kwenye ununuzi wa dawa muhimu hospitalini na kutekeleza miradi ya maendeleo. Tumezidi kupenda ubosi, magari 17 makubwa kwa kila mtu Serikalini, wakati katika nchi yetu kuna watu wanapata shida ya mlo mmoja,” alieleza Dk Mwigulu.
Bunge linasimamia Serikali
Katika hatua nyingine, Zungu amezungumzia kauli ya baadhi ya wanaopinga kwamba Bunge la 13 ni la chama kimoja kwamba haliwezi kusimamia masilahi ya wananchi akasema si kweli kwani wakati wote wamekuwa wakipigania masilahi hayo na ndiyo maana mambo mengi yaliyopendekezwa na Serikali yalikataliwa.
Ametaja baadhi ya maeneo ambayo Bunge liliigomea Serikali ambayo yanagusa watu wa chini ikiwemo pendekezo la nyongeza ya tozo kwenye pikipiki, kuongezwa muda kwa wafanyabiashara kabla ya kuanza kulipa kodi na ulinzi wa viwanda vya ndani kwa kuongeza ushuru kwenye bidhaa zinazoingizwa nchini zenye ushindani na viwanda.