Prime
MZEE WA FACT: Haya ndiyo mabilioni ya Aziz Ki Wydad
Mvp na mfungaji bora wa ligi ya Tanzania msimu wa 2023/24, Stephane Aziz Ki wa Yanga, ameuzwa kwenda klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco inayojiandaa kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia.
Taarifa zinasema dili la uhamisho wa mchezaji huyo limeipatia Yanga kiasi cha dola milioni moja za Marekani (zaidi ya shilingi bilioni mbili za Tanzania).
Kama hii ni ukweli basi Aziz Ki anakuwa mchezaji kutoka ligi ya Tanzania aliyeuzwa kwa pesa nyingi zaidi kihistoria. Lakini achana hilo, pesa atakazopata mchezaji mwenyewe ndiyo sababu ya kuandika makala hii.
Mchezaji huyo aliyekuja nchini mwaka 2022, mkataba wake wa kwanza ulikuwa umalizike mwishoni mwa msimu uliopita lakini akaongeza na kuendelea kusalia Jangwani hadi sasa anapouzwa kwa kiasi hicho cha kufuru.
Atakuwa akilipwa mshahara mnono wa kiasi cha shilingi za Tanzania zaidi ya milioni mia moja kwa mwezi. Amesaini mkataba wa miaka miwili, maana yake kila mwaka atavuna shilingi bilioni moja na ushee kupitia mshahara tu.
Zaidi ya mshahara, Aziz Ki atalipwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu kama pesa ya kusaini mkataba. Kiasi hiki kimegawanywa mara mbili, mwaka wa kwanza atalipwa shilingi milioni mia nane na ushee na mwaka wa pili atalipwa shilingi milioni mia tisa na ushee.
Ni kiasi hiki cha pesa ndicho kilichonisukuma kuandika hiki unachosoma. Dunia nzima imekuwa na mijadala ya kiasi cha pesa ambacho wachezaji mpira wanalipwa na vilabu vyao. Watu wengi wanasema wachezaji wanalipwa pesa ya kufuru na hawalingani na malipo hayo. Kimsingi ni kwamba, acha walipwe kiasi hicho wanacholipwa kwa sababu wanastahili, kama nitakavyoeleza hapa chini.
WABURUDISHAJI
Tunaishi kwenye dunia ambayo kipato chako hutegemea thamani yako kwenye jamii. Thamani ambayo wachezaji kama Aziz Ki wanayo ni kubwa kwa sababu wanaburudisha mashabiki wa vilabu vyao. Kuna watu hutoa hoja kwamba madaktari ni watu muhimu zaidi kwenye jamii kwa sababu wanaokoa maisha yetu kwa hiyo wanastahili kulipwa zaidi ya wanavyolipwa. Ni kweli kabisa kwa sababu kuokoa maisha ni jambo muhimu zaidi ya kuburudisha.
Lakini tofauti ni kwamba mchezaji kama Aziz Ki analeta furaha kwenye sura na nyoyo za mamilioni ya watu kwa wakati mmoja. Endapo daktari mmoja angekuwa anaokoa maisha ya mamilioni ya watu kwa mara moja, jambo ambalo haliwezekani au hutokea kwa nadra, basi angeweza kulipwa pesa nyingi sana.
WANAZALISHA
Wachezaji wanastahili kulipwa mamilioni kwa sababu wanazalisha wao wenyewe hayo mamilioni. Wachezaji wenye mvuto huvipatia pesa nyingi vilabu vyao kwa kuvutia wadhamini na watazamaji kwenye mechi. Pesa wanazozalisha ndizo wanazolipwa na kimsingi wanalipwa kidogo zaidi ya wanavyozalisha.
Timu zenye wachezaji wasio na mvuto au wenye mvuto mdogo, mechi zao hazizalishi pesa nyingi na wao hawalipwi vya kutosha zitatoka wapi hizo pesa? Ndiyo maana soka la wanawake, watoto au hata wale madaktari niliowatolea mfano pale juu, hawalipwi sana kwa sababu hawazalishi pesa nyingi hii ndiyo kanuni ya ubepari.
HAWANA MBADALA
Bila kuzivunjia heshima kazi nyingine muhimu duniani, wachezaji huwa hawana mbadala. Kuna watu wengi sana kila sehemu ambao wanaweza kuwa madaktari, endapo watapatiwa elimu lakini sio kuwa wachezaji. Mchezaji kama Aziz Ki anaweza asipatikane kwa zaidi ya miaka 20 ijayo, hata mkisomesha watoto wangapi kuwaandaa. Hii huwafanya wachezaji kuwa bidhaa adimu na kanuni za biashara zinasema bidhaa ikiwa adimu, thamani yake inapanda.
WAMEJITOA KAFARA
Ili kuwa mchezaji, unatakiwa ujitoe kafara ili ufanikishe ndoto zako. Unatakiwa ubadilishe aina ya maisha yako, ikiwemo kuwaepuka marafiki zako uliokuwa nao. Unatakiwa kuacha aina ya vyakula ulivyovizoea na kuvipenda. Unatakiwa kuzoea kuishi maisha yenye presha kubwa huku ukiandamwa na vyombo vya habari. Nani anataka maisha ya aina hii? Wao wanayaishi maisha hayo ili kufanikisha ndoto zao, ndiyo maana hata malipo yao lazima yawe makubwa.
HITIMISHO
Siko hapa kumsifu Aziz Ki na kiasi anachopata, hapana... Najaribu kufungua kichwa changu na vya wenzangu kama mimi ili kuelewa ni namna gani ilivyo halali kwa wachezaji kulipwa mamilioni. Tanzania kama nchi tunatoka kwenye itikadi za kijamaa na kuingia kwenye ubepari. Tunavyojiimarisha kwenye soka la kulipwa maana yake tunaimarisha ubepari kwenye mpira wetu. Ubepari katika ubora wake unataka mtu alipwe kwa kadri anavyoingiza. Kwa namna Wydad wamemthaminisha Aziz Ki na kuona atakavyovutia biashara yao, anastahili kulipwa atakacholipwa.