Prime
Aziz Ki na mtihani wa watu tisa Wydad

Muktasari:
- Raia wa Morocco mwenye umri wa miaka 25, msimu huu amecheza mechi 16 za ligi, hana bao wala asisti akiwa na asilimia 23 za kuanza kikosini. Yupo Wydad tangu Agosti 2023. Nafasi nyingine anayocheza mbali na ile ya winga ya kulia ambayo ndiyo yake, pia anamudu kutumika winga wa kushoto na mshambuliaji wa pili.
Achana na ishu ya kuisaidia timu kushinda makombe ambayo hiyo inamuhusu mchezaji yeyote akisajiliwa, lakini kuna jambo kubwa ambalo Stephane Aziz KI anakabiliana nalo ndani ya klabu ya Wydad Athletic ya Morocco ambayo anajiunga nayo akitokea Yanga.
Azi KI ameondoka Yanga baada ya kuitumikia timu hiyo kwa muda wa misimu mitatu tangu alipotua Julai 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambapo mkataba ulimalizika.
Pale Yanga, Aziz KI bado alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja, hivyo klabu hiyo imenufaika na mauzo ya nyota huyo raia wa Burkina Faso mwenye umri wa miaka 29 akitumia zaidi mguu wa kushoto.
Kuna mambo mazito Aziz KI ameyafanya akiwa na Yanga ndani ya misimu mitatu ambayo sio rahisi kusahaulika mpaka anaondoka, lakini sasa anakabiliwa na ukurasa mpya wa kuanzisha maisha ndani ya Wydad.
Wakati anaitumikia Yanga alipohusika katika mabao 86 kwenye mechi 114 za michuano yote akifunga 54 na kutoa asisti 32, huku kati ya hayo mabao 39 ni ya Ligi Kuu, yakiwamo 21 yaliyompa tuzo ya Mfungaji Bora msimu uliopita, Aziz Ki anapaswa kukaza msuli kuingia kikosi cha kwanza pale Wydad.
Ndani ya Yanga, Aziz KI alikuwa sehemu ya wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza, lakini huko anapokwenda kuna ushindani mkubwa kufuatia nyota tisa wanaocheza nafasi zote anazozimudu.
Inafahamika wazi kwamba Aziz KI ndani ya Yanga hata timu ya taifa ya Burkina Faso nafasi anayotumika zaidi ni kiungo mshambuliaji, lakini ana uwezo wa kucheza winga zote mbili kushoto na kulia, pia mshambuliaji wa pili kwa maana ya namba kumi.
Imeshuhudiwa kabla ya Aziz KI kutua Wydad, Mtanzania Seleman Mwalimu alitangulia kikosini hapo Januari mwaka huu ambapo hadi ligi inatamatika Mei 11, 2025, alicheza mechi tatu pekee kwa dakika 36 pekee kufuatia kujumuishwa kikosini mara sita, akiishia benchi mara tatu, huku akilia na ufinyu wa nafasi uliochangiwa na ushindani wa namba.
Mwalimu aliwahi kunukuliwa akizungumzia ishu ya kukosa nafasi kubwa ya kucheza akisema: “Nafurahia maisha ndani ya nchi hii, changamoto ya kukosa namba inaniongeza nguvu ya kupambana. Nashukuru nimekuwa nikipata walau dakika chache za kucheza, hizo ninazozipata zinanipa nguvu ya kuonyesha kitu ili kulishawishi benchi liendelee kuniamini.”
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Mwalimu, Aziz KI ambaye amezitesa timu nyingi katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa wakati anavaa jezi ya Yanga, anakwenda kuyaanza maisha mapya Wydad ikiwa chini ya Mohamed Amine Benhachem aliyechukua mikoba ya Rulani Mokwena ambaye hivi karibuni taarifa ilitoka wamefikia makubaliana ya kuachana.
Benhachem nafasi yake kikosini hapo ni Mkurugenzi wa Michezo, lakini amepewa kwa muda kuiongoza timu hiyo inayojiandaa kushiriki Kombe la Dunia la Klabu nchini Marekani kuanzia Juni 14 hadi Julai 13 mwaka huu huku Wydad ikipangwa Kundi G kuzikabili Manchester City, Juventus na Al Ain.
Katika kikosi cha Wydad, kuna nyota tisa ambao Aziz KI ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha anacheza na kuendeleza makali yake kama ilivyokuwa mitaa ya Jangwani.
HAMZA SAKHI
Umri wake miaka 28 akiwa ni raia wa Morocco na Ufaransa, tayari amecheza hapo kwa msimu mmoja ambao ni huu alipojiunga na timu hiyo akitokea AC Ajaccio ya Ufaransa. Nafasi yake halisi ni kiungo mshambuliaji, pia ana uwezo wa kucheza kiungo wa kati na winga wa kulia. Katika ligi msimu huu amecheza mechi 25, amefunga mabao mawili na asisti mbili akiwa na asilimi 67 za kuanza kikosini.
ARTHUR WENDERROSCKY
Ni Mbrazili mwenye umri wa miaka 20 ambaye nafasi yake halisi ni kiungo mshambuliaji, ametua kikosini hapo msimu huu akitokea Fluminense ya kwao, akifanikiwa kucheza mechi 14 za ligi akitoa asisti tatu, hana bao. Nafasi nyingine anayomudu ni kiungo wa kati. Ana asilimia 21 za kuanza kikosini.
PEDRINHO
Mbrazili mwingine katika kikosi hiki akiwa na miaka 21, naye ametua msimu huu akitokea Corinthians ya kwao, amecheza mechi nane za ligi, hana bao wala asisti. Mbali na nafasi ya kiungo mshambuliaji ambayo kiasili ni yake, pia anaweza kucheza winga ya kulia na mshambuliaji wa pili. Kutokana na takwimu za mechi alizocheza, ana asilimia saba za kuanza kikosini.
ISMAIL MOUTARAJI
Raia huyu wa Morocco mwenye miaka 25, yupo hapo tangu Julai 2022. Msimu huu amecheza mechi 23 za ligi akifunga mabao matatu na asisti nne. Ana asilimia 50 za kuanza kikosini. Nafasi nyingine anayoimudu mbali na kiungo mshambuliaji ni kiungo wa kati na mkabaji.
MOUAD ENZO
Naye ni raia wa Morocco, ana umri wa miaka 24. Msimu huu amecheza mechi tisa akiwa na asisti moja, hana bao akiwa na asilimia tatu pekee za kuanza. Ametua hapo msimu huu akitokea Fath Casablanca ya Morocco ambapo nafasi yake uwanjani ni kiungo mshambuliaji.
MOHAMED RAYHI
Umri wake ni miaka 30 akiwa na uraia wa Uholanzi na Morocco. Katika mechi 26 za ligi alizocheza kati ya 30, amefunga mabao 11, hana asisti. Ana asilimia 57 za kuanza kikosini. Mbali na winga ya kushoto ambayo ni nafasi yake, pia anaweza kucheza winga wa kulia na kiungo mshambuliaji. Ametua msimu huu akitokea Al-Jabalain ya Saudi Arabia.
SAIFEDDINE BOUHRA
Raia wa Morocco mwenye umri wa miaka 25, msimu huu amecheza mechi 16 za ligi, hana bao wala asisti akiwa na asilimia 23 za kuanza kikosini. Yupo Wydad tangu Agosti 2023. Nafasi nyingine anayocheza mbali na ile ya winga ya kulia ambayo ndiyo yake, pia anamudu kutumika winga wa kushoto na mshambuliaji wa pili.
WALID NASSI
Akiwa na uraia wa Morocco na Ufaransa, nyota huyu mwenye umri wa miaka 24 msimu huu kwenye ligi amecheza mechi 18 akifunga mabao mawili na asisti moja akiwa na asilimia 30 za kuanza kikosini. Ametua Wydad Agosti 2024 akitokea Dijon ya Ufaransa. Nafasi yake halisi ni winga wa kulia ingawa hata kushoto anaweza kucheza, pia anamudu kutumika kama mshambuliaji wa pili.
ZAKARIA FATIHI
Umri ni miaka 26 akiwa na uraia wa Morocco ambapo ametua kikosini hapo Januari 2025 akitokea SCC Mohammédia ya Morocco. Amecheza mechi 23 akifunga mabao mawili na asisti moja. Ana asilimia 60 za kuanza kikosini. Kati ya nyota wote wa eneo hilo, mwamba huyu ana uwezo wa kutumia miguu yote kwa ufasaha akicheza winga zote mbili na mshambuliaji wa kati ingawa nafasi yake halisi ni winga wa kulia.