MKAPA: Uchafu unavyotishia hadhi na thamani yake

Dar es Salaam. Ukitafuta eneo ambalo kwa kiasi fulani unaweza kusema lina ahueni kwenye Uwanja wa Mkapa ni la taa zinazomulika eneo la kuchezea (pitch) na kwenye majukwaa ndani ya uwanja huo mkubwa nchini.
Mazingira mengine ikiwamo eneo la kuchezea, kapeti la kukimbilia (tartan), viti vya majukwaa, runinga kubwa, nyasi, milango na kwenye vyoo ni aibu, huo ndiyo uhalisia.
Kwenye majukwaa kuna mapengo, viti vingi vimeng’oka, achilia mbali vile vilivyopauka, ukifika kwenye milango, ipo iliyotengeneza kutu, mingine haifungi na mingine imewekewa vitasa ambavyo haviendani na hadhi ya uwanja huo, achilia mbali ile ambayo fremu zake zimeoza.
Ukirudi kwenye eneo la kuchezea (pitch) na maeneo mengine yaliyopandwa nyasi, yameanza kupoteza nuru, rangi ya kijani ya nyasi hizo haipo tena kwa kukosa maji, japo jitihada za kumwagilia zinafanyika kipindi hiki cha kiangazi.
Kapeti la kukimbilia (Tartan) ni janga jingine, kwa lugha nyepesi unaweza kutamka limechoka halifai tena kwani jua kidogo tu linayeyuka na kutengeneza kama gundi au mfano wa tope, hapo bado hujaingia kwenye vyoo, huko ndipo utachoka zaidi.
Uchunguzi wa Spoti Mikiki wa wiki kadhaa kwenye uwanja huo unatosha kuthibitisha ile hadhi ya kuwa moja ya viwanja bora Afrika sasa inapotea.
Kwa wiki kadhaa, gazeti hili limefanya uchunguzi mwingine wa usafi kwenye uwanja huo katika siku ambazo kuna mechi au matukio mengine ya kimichezo na siku za kawaida.
Licha ya baadhi ya maeneo kuwa masafi katika siku za kawaida, harufu kwenye vyoo na mazingira yake ya ndani hayaendani na hadhi ya uwanja huo.
Katika siku za mechi, hali huwa mbaya zaidi, ukiachana na utupaji hovyo wa taka kwa mashabiki, vyooni ni changamoto zaidi, vingine havina maji, yaliyopo kwenye mapipa hayana ustaarabu wa kuyatumia, kopo la kuchotea ni moja na watumiaji ni wengi, vigine havina hata sabuni za kunawia mikono na masinki ni machafu na mabomba yameharibika.
“Baada ya mechi hasa ya Simba na Yanga, mazingira huwa machafu sana, tunatumia siku nne hadi tano kuusafisha, achilia mbali siku nyingine za kawaida,” anasema mmoja wa wafanya usafi ambaye alikuwa na fulana iliyoandikwa Cleaning Master.
“Hii ni kampuni ya usafi, ipo hapa hapa uwanjani, wafanyakazi tuko kama 37, kila siku tunaripoti kazini saa 11 alfajiri hadi saa 10 jioni, tunapangiwa maeneo ya kufanya usafi, siku za kawaida kuna maeneo tunafanya na mengine hatufanyi, itategemea na ilivyopangwa na msimamizi wako,” anasema.
Hata hivyo, alisema mshahara wake ni Sh 100,000, ingawa kuna mpango wa kuongezewa ambao hadi tuazungumza naye wiki iliyopita haukukamilika.
Ukiachana na kumwagilia nyasi, anasema kama hakuna mechi huwa wanasafisha uwanja huo kwa vipande vipande kwenye maeneo maalumu.
“Tunaweza leo kufagia, kufuta vumbi au kudeki, itategemea na namna ulivyopangiwa, inapoisha mechi ndipo tunafanya uwanja wote lakini kwa siku kadhaa hadi kumaliza,” anasema.

Meneja wa uwanja
Kama mpango wa Serikali kuukarabati uwanja huo utatiki, kwa kiasi fulani unaweza kurudi kwenye hadhi yake na hata mpango wa kuwa mwenyeji wa CHAN utazungumzika kwa vitendo.
Katika bajeti ya wizara ya mwaka huu wa fedha, Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohammed Mchengerwa alisema Sh10 bilioni zitakwenda kwenye ukarabati wa viwanja saba, ukiwamo wa Mkapa.
Meneja wa uwanja huo, Salum Mtumbuka anasema, ukarabati utazingatia maeneo ya pitch, tv, mabenchi ya ufundi, majukwaa na kwenye eneo la kukimbilia.
“Tutaondoa yote na kuweka mapya, ingawa pia tumeweka utaratibu wa kupunguza matumizi mengine ya uwanja, ulipojengwa ilikuwa ni mahususi kwa mpira wa miguu na riadha, matukio mengine ya kijamii tutapunguza kufanyika hapa,” anasema.
Kuhusu uharibifu wa mabomba, viti, milango na maeneo mengine ya uwanja huo, Mtumbuka anasema mbali na kuyakarabati, pia elimu ya uzalendo wa matumizi ya uwanja huo inahitajika.
“Kuna watu wakija uwanjani wanang’oa koki wanaenda kuuza, wengine wanafungua nati za viti na vitu vingine, wanakosa ule uzalendo wa kutumia kwa ustaarabu, tunahitaji kuwapa elimu,” anasema.
Anasema hata majukwaa yanapojengwa kwenye eneo la kuchezea yanaharibu eneo hilo, ambalo ukarabati tu wa nyasi si chini ya Sh50 milioni kwa mwaka.
“Hiyo ni kuzikarabati, si kupanda mpya, zinahitaji mbolea, dawa za kutibu fangasi na matunzo mengine na gharama huwa kubwa zaidi kupanda mpya ambazo zinapatikana Afrika Kusini,” anasema.
Japo hakuwa na kiwango kamili cha gharama za kuhudumia uwanja kwa mwezi kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi, Mtumbuka anasema bajeti yake inatoka wizarani, ingawa mameneja wengi waliosimamia uwanja huo waliwahi kulalamikia bajeti kuwa kiduchu.
Kwenye vyoo, anasema uwanja una vyumba 44 na matundu 500, ambayo ni wastani wa mashabiki 120 kutumia tundu moja la choo na watu 1363 kutumia chumba kimoja cha choo, kama vitatumika vyote hasa siku za matukio yanayosababisha uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 waliokaa kwenye viti kujaa.
Kwenye mechi ya Simba na Yanga, mara nyingi uwanja huo hujaa na wengine kulazimika kukaa kwenye ngazi za majukwaa, hivyo kuwa na matumizi makubwa zaidi na kusababisha mazingira kuwa machafu mno vyooni na kwingineko.

Kiafya ikoje?
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi anasema mazingira yanapokuwa machafu siku zote ni hatarishi kwa wanaozunguka eneo hilo.
“Mfano kwenye Uwanja wa Mkapa, unabeba watu 60,000 ukijaa, hivyo ni muhimu sana kuweka hali ya usafi, pia watu wanapokuwa karibu karibu ni rahisi kupata magonjwa yote yanayoambukizwa kupitia hewa, kugusana na hata kuharisha.
“Pia kuugua kifua na kupata magonjwa yanayoambukiza kupitia majimaji, vyoo vikiwa vichafu pia kupata UTI ni rahisi, hivyo usafi unahitajika zaidi,” anasema.
Anasema ukiacha usafi wa mazingira, pia ni muhimu watu kunawa mikono, maji yawepo muda wote uwanjani ili kuwapa nafasi mashabiki kunawa mikono.
Kwa mashabiki ipo hivi
Mmoja wa mashabiki, Anna Samwel anasimulia namna alivyopata UTI, akiamini alipata kwenye uwanja huo kutokana na mazingira ya vyoo vyake.
“Kuna vyoo vingine vya kukaa, kuna muda unaingia maji yameisha na wewe umebanwa, kipi bora udhalilike au ujisaidie hivyo hivyo? Nilifanya hivyo kama mara mbili nikaanza kupata maumivu ya tumbo, kupimwa tayari nina UTI,” anasema.
Shabiki wa Simba, Abdully Fakhi aNAsema changamoto kubwa uwanjani hapo ni mazingira ya vyoo ambavyo vingine wakiwa kwenye mechi huwa vinaziba.
“Usafi ni tatizo, vyoo ni vichafu namiferiji ile ya kusimama upande wa kiume inaziba inajaaa yote na pili ni hakuna ulinzi watu wanaingia vyoo vya kike huku ni wanaume, siku italeta shida,” anasema Fakhi.
Shabiki mwingine wa Yanga, Athuman Abdallah anasema Uwanja wa Mkapa unatakiwa usimamiwe kwa ngazi ya juu kwa sababu unachukua mashabiki wengi na kutumika kimataifa.
“Huu uwanja wanakuja hadi watu kutoka nje ya nchi, kwahiyo kuna vitu ambavyo vinaweza kumalizwa mapema na kuficha aibu hii mapema,” anasema Abdallah.
Kuhusu Uwanja wa Mkapa
Ulijengwa wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa. Awali ulijulikana kama uwanja wa Taifa kabla ya Rais wa awamu ya tano, John Magufuli kuupa jina la Mkapa kwa heshima ya Rais huyo mstaafu, sasa marais hao wote ni marehemu.
Umejengwa na kampuni ya wachina ya Beijing Construction Engineering Group kwa gharama ya Sh60 bilioni na ulifunguliwa rasmi mwaka 2007.