Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miroshi anaondoka bila deni AFCON

Nyota wa Kimataifa wa Tanzania, Novatus Dismas Miroshi anayekipiga kwenye Klabu ya Göztepe inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uturuki ni dhahiri kabisa ameondoka katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 akiwa ni miongoni mwa wachezaji wa Taifa Stars ambao walionyesha kiwango bora katika mashindano hayo yanayoendelea huko Morocco.

Mchezaji huyo mwenye sifa ya kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani ambapo anamudu kucheza kama beki wa kushoto, kiungo mkabaji au mshambuliaji amethibitisha uwezo wake katika michuano ya AFCON ambapo alikuwa akicheza kama kiungo mkabaji lakini hakuishia kuzuia tu bali alionyesha kupandisha mashambulizi pale timu ilipokuwa ikipanda kwenye eneo la wapinzani.


Anavyoondoka bila deni AFCON

Miroshi anarudi Uturuki akiwa hana deni kutokana na kiwango ambacho alikionyesha kwenye mashindano ya AFCON akiwa na Taifa Stars kwani katika mabao matatu ambayo Tanzania iliyapata kwenye hatua ya makundi, nyota huyo alichangia upatikanaji wa mabao mawili kati ya hayo matatu.

Katika mchezo wa kwanza Tanzania ilipokabiliana na Nigeria katika mchezo uliotamatika kwa Stars kupoteza mabao 2-1, ilishuhudiwa katika mchezo huo Super Eagles ikisawazishiwa bao mwanzoni mwa kipindi cha pili lililofungwa na Charles M’Mbombwa dakika ya 50 ambapo alipenyezewa pasi kwa ustadi mkubwa na Miroshi ambayo aliitumia vyema baada ya kuuweka mpira wavuni.

Katika mchezo uliofuata dhidi ya majirani zetu Uganda uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Miroshi hakufanikiwa kutoa pasi ya bao lakini alionyesha kiwango kwa kuzuia na kuanzisha mashambulizi kadhaa ambayo hayakuzaa matunda kwa Stars.

Mchezo wa mwisho wa kundi C ambao uliacha historia kwa Tanzania, pia ilishuhudiwa Miroshi akitoa pasi iliyozaa bao la kusawazisha ambalo lilizamishwa wavuni kwa shuti kali la Feisal Salum ‘Fei Toto’ dhidi ya Tunisia na kuihakikishia Tanzania kutinga katika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia tangu kuanza kwa mashindano hayo.

Nyota huyo anaungana na wachezaji wa Mataifa mengine kama Alex Iwobi, Samuel Chukwueze na Ademola Lookman (Nigeria), Azzedine Ounahi (Morocco), Dango Ouattara (Burkina Faso), Lyle Foster (Afrika Kusini), Hannibal Mejbri (Tunisia), Anis Hadj Moussa (Algeria) pamoja na Christopher Operi    (Ivory Coast) wote wakiwa wametoa pasi mbili za mabao katika hatua ya makundi.

Alivyoibukia Ulaya

Kabla ya kutimkia Ulaya, Miroshi alikuwa anakipiga Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo alizichezea timu za Azam FC na Biashara United Mara kwa vipindi tofauti ambapo aling’aa zaidi alipokuwa akiwatumikia Wanajeshi wa Mpakani, Biahara United Mara ambako alikuwa anacheza kwa mkopo akitokea kwa Matajiri wa Chamazi, Azam FC msimu wa 2019/2020.

Maisha ni safari, kila kitu huwa na muda na wakati wake, ndivyo ambavyo alikuwa akiamini Miroshi (23) ambaye licha ya kupata shavu la kuichezea Maccabi Tel Aviv ya Israel miaka kadhaa iliyopita alikuwa akiamini kuwa anaweza kupiga hatua zaidi.

Akiwa na umri mdogo kwenye kikosi cha vijana cha Azam FC, alikuwa na imani kuwa muda wake ukifika anaweza kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo, baada ya kuonekana kuwa ameiva waajiri wake hao wa zamani waliona kuwa anatosha kwenda Musoma huko Mara kwa ajili ya malisho mapya.

Iliaminika kuwa huko atapata nafasi zaidi ya kukomaa, inawezekana hicho ndio kitu ambacho Novatus alikuwa akikisubiri kwa hamu kwani ndani ya msimu huo aliwashangaza wengi na mwisho wa siku akawa mchezaji bora chipuki, kiasi cha waajiri wake wa zamani, Azam FC kuona kuwa kijana wao sasa anatosha kuwa sehemu ya kikosi chao kwa ajili ya msimu uliofuata wa 2020/21.

Novatus alitangazwa msimu wa 2020/21 kuwa kwenye mipango ya Azam FC na walimuongeza mkataba wa miaka mitatu lakini nafasi aliyopata ya kwenda Israel ndio ilikuwa tiketi yake ya kuanza soka la kimataifa kwani licha ya kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya kwenda kujifunza, akajikuta akipata nafasi ya kuonyesha kipaji chake na hapo ndipo Maccabi Tel Aviv ilipovitiwa naye na kumsajili.

Alipokuwa Israel, Novatus aliwahi kusema kwake jambo la kwanza ilikuwa ni kuingia Ulaya kisha aonyeshe makali yake ili atimize ndoto zake za kucheza ligi kubwa zaidi barani humo,”Najua kuwa hii ni klabu yenye histori kubwa Ulaya, nimeanza kuisikia miaka mingi kutokana na ushiriki wao kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nitaanzia kwenye kikosi cha vijana lakini naamini kuwa nitapandishwa na kuwa sehemu ya kikosi cha wakubwa, nimekuja kupigania ndoto zangu na sio kutembea,” alisema Miroshi.

Haikumchukua muda mrefu Novatus kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Maccabi Tel Aviv lakini kutokana na changamoto ya namba ilibidi atolewe kwa mkopo ili kupata uzoefu zaidi kiushindani kama ilovyokuwa kwa Azam wakati akianza safari yake ya soka nchini.

Hakuwa na noma Novatus kwani alikubali ofa ya timu daraja la kwanza huko Israel, Beitar Tel Aviv Bat Yam, akawa mmoja wa wachezaji muhimu licha ya kuwa umri mdogo ilikuwa panga pangua huwezi kumkosa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo, alicheza michezo 24 msimu uliopita akiwa kwa mkopo. Ubora wa Novatus ambaye amekuwa akifanya vizuri hata upande wa Taifa Stars umemvutia Msenegal, Mbaye Leye ambaye alikuwa kocha wa timu Zulte Waregem ya Ubelgiji.

Novatus alikuwa mchezaji wa tatu wa Kitanzania kucheza kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa miaka ya hivi karibuni wa kwanza ni nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye alitamba akiwa na KRC Genk ambayo aliichezea pia, Kelvin John na Royal Antwerp ambayo alikuwa kwa mkopo.

Kiraka huyo pia alipita kwenye Klabu ya Shakhtar Donetsk ya nchini Ukraine mwaka 2023 lakini pia nyota huyo licha ya kutokuwa na taji la Ligi Kuu Bara, alifanikiwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Ukraine akiwa na Shakhtar Donetsk ikiwa ndio taji lake la kwanza na kuweka rekodi ya kucheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa mchezaji wa pili kufanya hivyo baada ya Samatta.

Safari ya Uturuki imewadia

Baada ya kumaliza majukumu na timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, mchezaji huyo wa Göztepe ya Uturuki atarejea kuendelea na Ligi Kuu nchini humo huku nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza ikiwa bado mikononi mwake kutokana na kiwango alichokionesha kwenye mashindano ya AFCON.

Göztepe inashika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu nchini Uturuki ikiwa imekusanya jumla ya pointi 32 ikishinda mechi mechi tisa, imetoka sare mara tano na kupoteza mara tatu katika mechi 17 ilizocheza sawa na vinara wa ligi Galatasaray wenye pointi 42 huku Fenerbahce ikishika nafasi ya pili kwa pointi 39 wakati nafasi ya tatu ipo Trabzonspor yenye pointi 35.

Göztepe inakibarua cha kuhakikisha inamaliza katika nafasi za juu ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki katika michuano ya Ulaya msimu ujao baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita ilipopoteza mechi mbili kati ya tatu za mwisho ambazo ingepata matokeo mazuri msimu huu ingekuwepo kwenye mashindano ya Ulaya.