Singida BS yambadilishia majukumu Gamondi
Kocha wa muda wa Taifa Stars na Mkurugenzi wa Ufundi wa Singida BS, Miguel Gamondi. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Gamondi amefanikiwa kuiongoza Stars kuweka rekodi ya kucheza hatua ya mtoano ya AFCON kwa mara ya kwanza katika historia.
Dar es Salaam. Kutoka kuwa kocha mkuu wa Singida Black Stars hadi kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi ambacho ndio cheo kipya cha Miguel Gamondi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi wa Singida BS, leo Jumatatu, Januari 5, 2025 umetangaza mabadiliko katika klabu yao ambapo kocha mkuu wa timu hiyo atakuwa David Ouma.
Ouma atasaidiwa na makocha wasaidizi Mousa Nd’aw na Muhibu Kanu.
Gamondi amebadilishiwa majukumu na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu, nafasi itakayompa dhamana ya kusimamia mipango ya kiufundi na maendeleo ya jumla ya timu.
Aidha, Singida BS imemrejesha Ramadhani Nsanzurwimo kama Mshauri wa Ufundi wa klabu, huku Kocha Othman Najar akiendelea kushiriki katika benchi la ufundi kulingana na majukumu aliyopangiwa na uongozi.
Uongozi wa klabu hiyo umeeleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuongeza ufanisi katika eneo la ufundi na kuweka mazingira bora ya ushindani.
Singida BS imeongeza kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida katika soka la kisasa na yanalenga kuijenga timu kwa misingi ya muda mrefu ili kushindana kikamilifu katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Hata hivyo, Singida imesema haina pingamizi lolote kwa mamlaka endapo Gamondi atateuliwa kuwa kocha wa kudumu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Kwa sasa Gamondi ni kocha wa muda wa Taifa Stars ambapo alikabidhiwa majukumu ya kuinoa Novemba 4, 2025 katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa mafanikio makubwa akiweka rekodi ya kuiongoza Stars kufuzu katika hatua ya mtoano kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania.
Kabla ya Gamondi kutambulishwa, Taifa Stars ilikuwa imecheza mechi sita mfululizo za mashindano na kirafiki bila kupata ushindi huku ikifunga bao moja tu ilipokuwa chini ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’.
Katika mashindano ya AFCON yanayoendelea kutimua vumbi nchini Morocco, Stars ilifanikiwa kutinga hatua ya 16 bora baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye kundi C ikibebwa na takwimu za mabao ya kufunga baada ya kupachika jumla ya mabao matatu huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne ikiishinda Angola ambayo ilikuwa imefunga mabao mawili.
Hata hivyo, Stars imetupwa nje ya mashindano hayo jana Januari 4, 2026 baada ya kupoteza bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo, Morocco.
Tangu Gamondi akabidhiwe Stars imekuwa na mabadiliko makubwa na kuonyesha kiwango bora katika michuano ya AFCON.