Mambo saba Taifa Stars ikiaga mashindano Morocco
Muktasari:
- Mwaka huu mambo yamekuwa tofauti kabisa baada ya Stars kuonyesha uimara katika mashindano haya kwani licha ya kufungwa kila mchezo na yenyewe imefunga isipokuwa mchezo wa leo
Rabat, Morocco. Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeaga rasmi mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 yanayoendelea kutimua vumbi nchini Morocco katika hatua ya mtoano ambayo ilifanikiwa kufuzu baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwa takwimu nzuri.
Katika mchezo wa leo uliokuwa unapigwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdallah, Rabat, imeshuhudiwa Stars ikishindwa kufurukuta mbele ya wenyeji wa mashindano hayo Morocco baada ya kuruhusu kipigo cha bao 1-0.
Stars ilimaliza kwa kukusanya jumla ya pointi mbili katika kundi C huku wastani mzuri wa mabao ya kufunga ukiisogeza mbele katika hatua ya 16 na kuandika rekodi ya kufanya hivyo kwa mara ya kwanza katika historia.
Waamuzi na manahodha wa timu za taifa ya Morocco na Taifa Stars wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya mchezo wa mtoano leo Jumapili, Januari 4, 2026. Picha na Mtandao
Dakika 45 za kwanza
Kipindi cha kwanza Stars haikuanza kinyonge baada ya kutengeneza nafasi kubwa ya wazi ambayo ilishindwa kutumiwa vyema na Simon Msuva ambaye aliupiga mpira kwa kichwa ulioshindwa kuingia wavuni
Wenyeji wa mashindano waliondoka kwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa wameinamisha vichwa chini baada ya kudhibitiwa na Stars.
Tanzania iliondoka ikiwa imepiga mashuti mawili tu kwenye lango la Morocco huku kukiwa hakuna hata shuti lililolenga langa sawa na Morocco waliopiga mashuti matano bila kulenga lango la Stars.
Mshambuliaji wa Taifa Stars, Salum Mwalimu akimtoka beki wa Morocco. Picha na Mtandao
Dakika 45 za pili
Katika kipindi cha pili, Morocco ilianza kwa kasi ikitafuta bao la uongozi huku Stars ikiwa nyuma kuzuia mashambulizi ya mpinzani wao.
Licha ya kuonekana kuzidiwa na mashambulizi Stars haikushindwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambapo dakika ya 55 Feisal Salum 'Fei Toto' alikosa bao la wazi baada ya kipa wa Morocco, Yassine Bono kutema shuti kali lililopigwa na Mohamed Hussein kisha Seleman Mwalimu kuutenga kwa Feisal ambaye alishindwa kuingiza mpira wavuni ukipaa juu ya lango.
Mshambuliaji wa Morocco, Brahim Diaz (namba 10) akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao dhidi ya Taifa Stars katika mechi ya mtoano AFCON 2025.
Bao la Diaz
Uzoefu na uwezo wa mchezaji binafsi umekuwa nguvu kubwa kwenye mashindano haya baada ya Brahim Diaz kuifungia Morocco bao lililowavusha kwenda robo fainali ambapo alitumia ustadi mkubwa kuingizia mpira wavuni.
Nyota huyu anayekipiga kwenye Klabu ya Real Madrid ya Hispania alithibitisha ubora wake baada ya kuuweka mpira wavuni kwa kutumia nafasi ndogo iliyokuwa imeachwa pembeni ya lango na golikipa, Hussain Masalanga sehemu ambayo haikuzaniwa kabisa mpira kupita kwa urahisi.
Namna alivyoupitisha mpira kwenda wavuni alithibitisha ubora wa kuwa mchezaji mkubwa na mwenye uwezo wa kuibeba timu katika wakati mgumu kama ule.
Hata baada ya kuwa nyuma kwa bao moja, vijana wa Miguel Gamondi bado hawakukata tamaa kwani waliendelea kufanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Morocco lakini hayakufanikiwa kuzaa matunda.
Baeki wa Taifa Stars, Bakar Nondo akijaribu kumtoka beki a Morocoo, Noussair Mazraoui. Picha na Mtandao
Mbinu za kocha
Tangu mchezo wa kwanza dhidi ya Nigeria, kocha Miguel Gamondi aliwaruhusu wachezaji wake kucheza mpira kuliko kukaa nyuma kuzuia mashambulizi ya mpinzani.
Aina hiyo ya mchezo imewafanya wachezaji wa Stars kucheza kwa kujiamini zaidi bila kuwa na presha na ndiyo maana hata ilivyoruhusu bao bado ilionekana kuwa imara kufanya mashambulizi kadhaa huku ikiendelea kujilinda.
Kawaida timu inapokuwa imekaa nyuma kujilinda ndivyo inavyomruhusu mpinzani kufanya mashambulizi mengi kwenye lango tofauti na kucheza mpira wa kufunguka kwa kuwaheshimu wapinzani bila presha, jambo ambalo Stars imelifanya katika mechi za makundi kwani uchezaji wa aina hiyo unamjenga mchezaji kujiamini na kupunguza presha ya mchezo.
Ushindani umeonekana
Karibu wachezaji wote wa kikosi cha kwanza cha Tanzania wana uzoefu wa kucheza mechi kubwa za Kimataifa walioupata kupitia Klabu zao wanazozichezea kushiriki michuano hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa imewapa uzoefu wa kushindana uwanjani.
Nyota kama Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto, Tshabalala, Feisal, Dickson Job na Shomari Kapombe tayari wanaouzoefu wa kukabiriana na wapinzani wakubwa kutokana na ushiriki wao wa mara kwa mara katika michuano ya Kimataifa wakiwa na Klabu pamoja na timu ya taifa.
Vilevile wapo nyota wengine wa Kimataifa ambao wanakipiga kwenye ligi mbalimbali kama Novatus Miroshi, Simon Msuva, Charles M’Mbombwa, Mbwana Samatta, Haji Mnoga, na Alphonce Msanga ambao wameonyesha uzoefu wa kucheza kwa ushindani ulioisaidia Stars kuonyesha kiwango katika mashindano ya mwaka huu.
Beki wa kushoto wa Taifa Stars, Mohammed Hussein akikokota mpira wakati wa mechi ya mtoano AFCON dhidi ya Morocco. Picha na Mtandao
Uzoefu wa Mashindano
Haya ni mashindano ya AFCON kwa mara ya nne ambayo Taifa Stars imeshiriki kwa kipindi cha hivi karibuni ukiachana na yale iliyoshiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1980 kule Nigeria.
Ukiangalia uchezaji katika mashindano ya mwaka huu ni dhahiri kabisa kunaonekana tofauti ya uchezaji wa mashindano yaliyopita ya AFCON ambayo Stars ilikuwa ikiambulia kucheza mechi za hatua ya makundi pekee.
Katika mechi za hatua ya makundi kwenye mashindano ya mwaka huu, Stars imeonyesha kuwa na uzoefu kiasi fulani kwani tuliona hata katika mechi dhidi ya timu kubwa kama Nigeria bado Tanzania ilionyesha ushupavu licha ya kuruhusu kipigo cha mabao 2-1.
Katika kulithibitisha hilo, Taifa Stars ilionyesha tena ukomavu baada ya kutoka nyuma na kusawazisha bao dhidi ya Tunisia ambayo ina wachezaji bora kulinganisha na Tanzania.
Hata katika mechi ya leo Stars haijaondoka kinyonge kwani imewaachia maswali magumu wenyeji hao katika hatua inayofuata. Kiwango ilichoonesha Tanzania kinatoa matumaini ya kuja kufika hatua za mbali katika mashindano yanayofuata yatakayoandaliwa kwa pamoja na Kenya, Uganda na Tanzania.
Mshambuliaji wa Morocco, Brahim Diaz akizungumza jambo na Kiungo wa Taifa Satrs, Feisal Salum mara baada ya mchezo uliomalizika kwa Stars kupoteza bao 1-0 na kuondoshwa kwenye michuano ya AFCON 2025. Picha na Mtandao
Takwimu za jumla
Katika mashindano ya mwaka huu yamekuwa tofauti kwa Stars kwani hadi inatoka kwenye mashindano haikuonyesha unyonge katika mechi zao zote.
Katika mashindano ya mwaka 2019 yaliyofanyika nchini Misri, Stars ilifungwa jumla ya mabao manane huku yenyewe ikifunga mawili wakati katika mashindano ya mwaka 2023 yaliyofanyika nchini Ivory Coast, Tanzania iliruhusu mabao manne huku yenyewe ikipachika bao moja.
Mwaka huu mambo yamekuwa tofauti kabisa baada ya Stars kuonyesha uimara katika mashindano haya kwani licha ya kufungwa kila mchezo na yenyewe imefunga isipokuwa mchezo wa leo ambapo imeruhusu jumla ya mabao matano huku yenyewe ikipachika matatu wavuni jambo ambalo liliisaidia kupenya katika hatua ya mtoano ikiishinda Angola ambayo nayo ilimaliza kwa pointi mbili huku ikiwa imefunga mabao mawili pekee.