Tuiombee Taifa Stars
Muktasari:
- Hilo litakuwa ni pambano la tisa kwa Tanzania kuumana na Morocco tangu 2010 kupitia mechi za michuano mbalimbali, huku rekodi zikiwabeba wenyeji, kwani katika mechi nane za awali wameshinda saba, huku ni mara moja tu kwa Stars kutoka na ushindi mbele ya wapinzani wao hao.
Mechi ya kikubwa! Ndio, kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat itapigwa mechi ya kukata na shoka kati ya wenyeji Morocco na Tanzania.
Hii ni mechi inayozikutanisha timu zenye ubora na viwango vinavyotofautiana kama ilivyokuwa katika vita ya mkubwa na mdogo, kutokana na ubora na mafanikio ya timu zote mbili, lakini jambo pekee kwa Watanzania wengi ni kuweka maombi mbele.
Kwa kuangalia takwimu za ubora kisoka na hata wachezaji mmoja mmoja, ni wazi Morocco wapo juu maradufu kuliko wale wa Taifa Stars ya Tanzania. Kama hujui ni kwamba Morocco ndio nchi inayoongoza kwa ubora wa soka Afrika kulingana na orodha ya viwango vya soka vya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), vilivyotolewa Desemba 22, mwaka jana, ikishika nafasi ya 11 duniani, ikitofautiana nusu pointi na Croatia iliyopo ndani ya 10 Bora.
Katika orodha hiyo Tanzania inashika nafasi ya 112 duniani ilihali kwa Afrika ni ya 27 kati ya nchi 53. Lakini, kwa vile soka siku zote huwa na maajabu yake baadhi ya mashabiki na wapenzi wa soka nchini wanaitumainia timu yao kama Daudi alivyomsapraizi Goliati kwa kumpiga na jiwe akitumia kombeo na kuwakomboa wana wa Israel enzi hizo.
Hata hivyo, ukija katika uhalisi mechi ya leo ni ngumu na Tanzania inapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa ili kukabiliana na wenyeji watakaoongezewa nguvu na mashabiki wanaosifika kwa kujaza na kuanikiza uwanjani kwa vaibu la kutisha ambalo kwa wasiozoea wanaweza kupoteza umakini wa kupambana na timu hiyo.
Hilo litakuwa ni pambano la tisa kwa Tanzania kuumana na Morocco tangu 2010 kupitia mechi za michuano mbalimbali, huku rekodi zikiwabeba wenyeji, kwani katika mechi nane za awali wameshinda saba, huku ni mara moja tu kwa Stars kutoka na ushindi mbele ya wapinzani wao hao.
Mara ya mwisho Stars kuifunga Morocco ilikuwa Machi 24, 2013 katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 kwa kuichapa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo aliyekuwa mshambuliaji wa Morocco, Marouane Chamakh, aligoma kubadilishana jezi na Mbwana Samatta aliyewatungua mabao mawili siku hiyo.
Katika mechi ya leo wachezaji watatu waliokuwa katika timu iliyoidhalilisha Morocco, Shomari Kapombe, Simon Msuva na Samatta wapo katika kikosi cha sasa cha Gamondi ili kusaka tiketi ya robo fainali kwa mara ya kwanza katika michuano ya Afcon baada ya awali kufanya hivyo katika CHAN 2024.
Katika hatua ya makundi ya Afcon 2023, Tanzania ilifungwa mabao 3-0, lakini pia zimekutana katika mechi za kuwania fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico na mara zote Stars imepasuka nje ndani kwa mabao 2-0 na katika robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 ililala pia kwa bao 1-0.
Kwa kuangalia namna rekodi zilivyo na aina ya vikosi vilivyopo katika fainali hizo za Afcon 2025, ni wazi turufu inawaangukia wenyeji, ingawa soka huwa na matokeo ya kikatili na ndicho wanachotegemea Watanzania kwa Stars.
Hapa kuna shughuli pevu
Katika mechi ya leo, Stars itakuwa na kazi kubwa ya kuwazuia nyota wa Morocco ambao wanacheza soka la kasi na kutumia akili mipira iliyokufa, na pia kuwatia presha mabeki wa timu pinzani, hivyo kama Ibrahim Bacca, Bakar Mwamnyeto na Dickson Job watatumika kama ilivyokuwa katika mechi dhidi ya Tunisia wanapaswa kujipanga.
Kuna uwezekano mkubwa kocha Miguel Gamondi akafanya mabadiliko madogo katika kikosi kulinganisha na kile kilichocheza mechi ya mwisho dhidi ya Tunisia ikiwamo eneo la golini kwa Zuberi Foba kurudi akipishana na Hussein Masalanga, japo Alphonce Mabula na Dismas Novaus wanaweza kucheza eneo la kiungo.
Eneo la ushambuliaji kuna uwezekano wa Seleman Mwalimu 'Gomez', Feisal Salum na Simon Msuva wakaanza ili kuipa kashikashi beki ya Morocco iliyoruhusu bao moja katika mechi tatu zilizopita za makundi na yenyewe kufunga saba, ilihali Stars imeruhusu mabao manne na kufunga matatu.
Presha kubwa katika mechi hiyo itakuwa zaidi kwa Morocco ambao hesabu zao ni kutinga fainali na kubeba taji ambalo wanalisaka tangu walipotwaa mara ya mwisho 1976 na kulikosa katika fainali za 2004 mbele za waliokuwa wenyeji, Tunisia.
Lakini, pamoja na kuwa moja ya timu zilizofunga mabao mengi na kufungwa bao moja, bado timu hiyo imekuwa ikikosolewa na wadau wa soka wa nchi hiyo wakiponda mbinu za kocha Walid Regragui.
Pia, watashuka uwanjani wakiumizwa na mbinu za Gamondi ambaye ameifanya Stars kuwa timu ngumu kufungika akitumia mfumo wa 5-4-1 aliowawekea Watunisia katika mechi ya mwisho na kuwafanya washindwe kucheza kwa uhuru na kulazimishwa dakika 90 kuisha kwa sare ya 1-1.
Ukuta wa Stars ambao umeruhusu mabao manne katika mechi tatu za makundi utakuwa na kazi ya kuwadhibiti mastaa wawili hatari wa Morocco, mshambuliaji Ayoub El Kaabi anayekipiga Olympiacos Piraeus na kiungo Brahim Diaz wa Real Madrid ambao kila mmoja amefunga mabao matatu katika mechi tatu za makundi.
Stars iliyofunga mabao matatu katika mechi za makundi kupitia Charles M'Mombwa, Simon Msuva aliyekwamisha kwa penalti na kiungo Feisal Salum itakuwa na kazi ngumu kuipenya safu ya Morocco iliyoruhusu bao moja kupitia mechi tatu ilizocheza pale ilipotoka sare ya 1-1 na Mali.
Hata hivyo, pamoja na ukubwa wa Morocco na kuwa wenyeji, bado Stars inawapa matumaini Watanzania kwa kusema watashuka uwanjani kwa nia moja ya kutafuta matokeo mazuri na wachezaji wanasema "waacha kipigwe tu."
Simon Msuva kinara wa mabao akiwa na 25 akilingana na Mrisho Ngassa kupitia mechi 101 amenukuliwa mapema akisema kwamba wanaiheshimu Morocco kwa ubora ilionao, lakini watashuka uwanjani kwa nia ya kupambana ili kupata matokeo kwa vile soka ni mchezo wa maajabu na wenye matokeo ya kustaajabisha.
"Tuna mtihani mkubwa mbele yetu, lakini tutaenda kupambana ili kuleta heshima kwa Tanzania. Muhimu kila Mtanzania atuombee kwa mechi ya Jumapili (leo)," alisema Msuva, kauli iliyoungwa mkono pia na nahodha Mbwana Samatta sambamba na kocha Gamondi.
Kocha huyo alisema anajisikia fahari kuifikisha Tanzania hatua hiyo licha ya kwamba wanajua wana mechi ngumu mbele ya Morocco, lakini ameandaa kikosi kupambana bila presha mbele ya wapinzani wao.
Njia ni hii
Kama itatokea Stars ikibahatika kupenya mbele ya Morocco na kutinga robo fainali bado itakuwa na kibarua kigumu, kwani itacheza na mshindi kati ya Afrika Kusini au Cameroon, Januari 9, na hata hapo ikitoboa itakuwa na kigingi kingine nusu fainali itakapocheza na mshindi kati ya Algeria dhidi ya DR Congo na yule wa Nigeria dhidi ya Msumbiji.
Waamuzi wa mechi
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limemteua mwamuzi kutoka Mali, Boubou Traore kuamua pambano hilo ikiwa ni mwendelezo wa utamaduni wa kuwapanga waamuzi wa Kiafrika wenye uzoefu kusimamia mechi muhimu za mtoano.
Traore, aliyezaliwa Machi 3, 1989 na kupewa beji ya Fifa 2014, ndiye aliyesimamia mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Februari, mwaka juzi, kati ya Yanga na CR Belouizdad na wenyeji vijana wa Jangwani kushinda kwa mabao 4-0 yaliyowawezesha kutinga robo fainali.
Rekodi zinaonyesha mwamuzi huyo amechezesha mechi 25 za klabu Afrika, huku katika michezo hiyo wenyeji wameshinda 17, ilhali wageni wakishinda sita na mbili zikiisha kwa sare. Pia anasifika kwa kumwaga kadi kama njugu kwani kupitia mechi hizo ametoa za njano 86 na nne nyekundu kuonyesha kuwa hana utani uwanjani.
Katika michuano ya Afcon 2025 alisimamia shoo ya Nigeria na Tunisia, na Super Eagles iliibuka mshindi wa mabao 3-2 na kuwa ya kwanza kutinga hatua ya 16 Bora kutoka Kundi C lililokuwa pia na Tanzania na Uganda.
Mwamuzi huyo atasaidiwa na Modibo Samake kutoka Mali na Jonathan Koffi Ahonto wa Togo, huku Jean-Jacques Ndala Ngambo atakuwa mezani na mwamuzi kutoka Senegal, Issa Sy, atasimamia kama mwamuzi msaidizi wa video (VAR).
Traore ni mwamuzi mwenye uzoefu mkubwa kutoka Mali ambaye amekuwa akishiriki mara kwa mara katika mashindano ya CAF ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na yale ya awali ya Afcon. Kwa kumteua kusimamia mechi hiyo, CAF inaonyesha imani kubwa iiyonayo katika uwezo wake wa kuchezesha mechi kubwa na muhimu Afrika. Tayari amekuwa na majukumu mengi katika Afcon hii, kwani licha ya Nigeria na Tunisia, pia alikuwa mwamuzi wa nne kati ya Angola dhidi ya Misri iliyoisha kwa suluhu.
Mechi nyingine za leo
Baada ya mechi hiyo ya saa 1:00 usiku leo, ifikapo saa 4:00 kwenye Uwanja wa Al Medina Afrika Kusini itakuwa na kibarua dhidi ya Cameroon. Hilo litakuwa ni pambano la sita kwa timu hizo kukutana tangu 1996, kwani awali zilishakutana mara tano ikiwamo mechi mbili za kirafiki na tatu za michuano ya Afrika ambapo Wasauzi walishinda mara mbili huku nyingine zikiisha kwa sare zikiwamo za mwisho za makundi ya kuwania kufuzu fainali za Afcon 2018.
Hii ni kuonyesha pambano hilo la 16 Bora halitabiriki kirahisi, kwani kila timu ina nafasi japo Cameroon ya msimu huu inaonekana kuwa imara zaidi kulinganisha na Afrika Kusini.
Fedha ipo
Hatua ya Stars kutinga 16 Bora ya Afcon 2025 imeihakikisha kuvuna Dola 800,000 (zaidi ya Sh1.9 bilioni mbali na kupokea Sh300 milioni kama zawadi ya kila bao ikianzia mechi dhidi ya Uganda ilipotoka sare ya 1-1 na kuongezwa hadi Sh200 milioni ilipoumana na Tunisia na kutoka pia sare ya 1-1.
Kwa mujibu wa zawadi za fedha za Afcon 2025 bingwa atazoa Dola 10 milioni, huku atakayekuwa wa pili atabeba Dola 4 milioni na zitakazoishia nusu fainali zitapewa Dola 2.5 milioni, ilhali zitakazofika robo fainali zitakunja Dola 1.3 milioni na zilizotinga 16 Bora kila moja itabeba Dola 800,000.
Kwa zilizomaliza nafasi ya tatu na nne katika hatua ya makundi kila moja imeambulia kati ya Dola 700,000 na 500,000 mtawalia.