Kocha aifungukia Nigeria
Kocha mkuu wa Msumbiji, Chiquinho Conde, ameonesha imani kubwa na uwezo wa timu yake kuelekea mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Nigeria, huku akikubali wazi kuwa Super Eagles ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda mechi ya leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Fez.
“Tumeonesha kwamba tuna timu imara na yenye uwezo,” amesema Conde.
“Dhidi ya Ivory Coast na Cameroon tulikosea mambo madogo, lakini sasa ni hatua ya kufa au kupona. Nigeria ni timu bora, lakini tunapaswa kuikabili mechi hii kwa unyenyekevu, utulivu na uwajibikaji mkubwa. Tumefika hatua hii kwa heshima, sasa tutaonesha kile tunachoweza kufanya.”
Msumbiji ilihakikisha inafuzu hatua ya mtoano baada ya kampeni ngumu ya hatua ya makundi dhidi ya wapinzani wenye nguvu.
Mambas ilianza michuano kwa kipigo chembamba dhidi ya Ivory Coast, kabla ya kupata ushindi wa kihistoria dhidi ya Gabon na kuandika ushindi wao wa kwanza kabisa katika historia ya AFCON.
Msumbiji ilihitimisha hatua ya makundi kwa kipigo kingine cha ushindani mkubwa dhidi ya Cameroon, lakini matokeo hayo yaliwatosha kupata nafasi ya kuingia miongoni mwa timu 16 bora kupitia kapu la mshindwa bora lililowabeba pia Tanzania, Benin na Sudan.
Leo itakuwa na kibarua dhidi ya Nigeria, mabingwa wa Afrika mara tatu, wanalenga kuendeleza mwanzo wao mzuri katika AFCON 2025 katika pambano litakalopigwa kuanzia saa 4:00 usiku.
Super Eagles imeshinda mechi zao zote hadi sasa katika mashindano haya, jambo linaloimarisha sifa yao kama moja ya timu hatari zaidi kwenye michuano hiyo.
Hii itakuwa mara ya pili kwa timu hizi kukutana katika AFCON, kwani mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2010 katika mechi ya mwisho ya makundi na Nigeria ilishinda 3–0 kupotia kwa Peter Odemwingie alifunga mabao mawili dakika ya 45 na 47, huku Obafemi Martins akiongeza bao la tatu dakika ya 86.
Rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara tano katika mashindano yote na Nigeria haijawahi kupoteza kwani imeshinda nne na mechi moja kuisha kwa sare, huku ikivuna mabao sita dhidi ya mawili ya wapinzani wao hao.
Mechi nyingine ya leo itapigwa mapema saa 1:00 usiku kwa mabingwa wa kihistoria, Misri itakayovaana na Benin kwenye Uwanja Adrar uliopo mji wa Agadir, likiwa ni pambano la tano kwa timu hizo kukutana katika michuano mbalimbali tangu mwaka 2004, huku katika mechi nne za awali Misri ikishinda mechi tatu na moja ikiisha kwa sare.