Man United yaanza ziara Asia

Muktasari:
- Katika ziara yao Asia, Man United watacheza michezo miwili ambayo itahitimishwa kwa mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Hong Kong, Ijumaa, Mei 30 mwaka huu.
Manchester United imesafiri kuelekea Asia kwa ziara ya siku kadhaa kama sehemu ya maandalizi ya msimu ujao, ambapo itacheza michezo miwili ya kirafiki. Ziara hiyo itaanza rasmi Mei 28 na kuhitimishwa Mei 30 mwaka huu ikiwa ni fursa kwa klabu kujiandaa kabla ya msimu mpya kuanza.
Kocha, Ruben Amorim ameondoka na wachezaji 32 kwenye safari hiyo akiwemo nahodha , Bruno Fernandes na Alejandro Garnacho ambao kulikuwa na tetesi kwamba huenda wakaondoka kwenye timu hiyo mwishoni mwa msimu huu.

Bruno Fernandes ambaye kulikuwa na tetesi huenda akajiunga na matajiri wa Saudi Arabia, Al Hilal ambao wamekua wakimfukuzia kwa muda mrefu bila mafanikio, iliaminika msimu huu wanaweza kumnasa kwani kabla ya mchezo wa mwisho wa ligi, nyota huyo raia wa Ureno aliomba kuondoka kwenye timu hiyo.

Kwa upande wa Garnacho ambaye hakuwa sehemu ya kikosi cha Man United kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa, kulikuwa na taarifa huenda nyota huyo raia wa Argentina akaondoka kwenda kutafuta timu nyingine kwani kumekuwa na taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kwamba, Ruben Amorim haridhishwi na kiwango cha mchezaji huyo.
Wachezaji wengine waliosafiri na kikosi hicho ni pamoja na beki, Matthijs de Ligt, Joshua Zirkzee, ambaye amerudi hivi karibuni baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na jeraha la msuli wa paja.
Andre Onana na Luke Shaw, ambao walikosa mechi ya Jumapili, nao wamejumuishwa katika kikosi, lakini beki mkongwe Jonny Evans, Victor Lindelof na Christian Eriksen, hawajasafiri na timu kutokana na changamoto binafsi.
Beki wa Argentina, Lisandro Martinez ambaye alipata majeraha hajasafiri, huku Noussair Mazraoui na Leny Yoro nao pia wakikosa kutokana na majeraha.

Red Devils, watakabiliana na timu ya Asian All Stars huko Kuala Lumpur, Malaysia, Mei 28 kabla ya kusafiri kwenda Hong Kong kwa mechi nyingine siku mbili baadaye.
Mmoja wa wadhamini wa United, Apollo Tyres, amesema kuwa Andre Onana, Harry Maguire na Diogo Dalot watakuwepo Mumbai, India siku ya Alhamisi, Mei 29 kwa tukio maalum la kukutana na mashabiki.
Maandalizi ya msimu ujao kwa United yataanza kwa mechi dhidi ya Leeds United huko Sweden, Julai 19 kabla ya kusafiri kwenda Marekani kushiriki mashindano ya maandalizi ya Ligi Kuu msimu ujao yaani ‘pre-season’ yatakayoanza Julai 26 hadi Agosti 3 mwaka huu kabla kucheza mchezo mwingine dhidiya Fiorentina utakaofanyika katika Uwanja wa Old Trafford Agosti 9.

United ambayo imetoka kushinda mchezo wa mwisho kwenye Ligi Kuu ya England dhidi ya Aston Villa Jumapili iliyopita, ilikuwa na msimu mbaya kwani katika michezo 38 imeshinda mara 11, imepata sare mara tisa na kuruhusu vipigo 18 huku ikimaliza katika nafasi ya 15 ikikusanya jumla ya pointi 42.
United pia wataikosa michuano ya Kimataifa ya Vilabu Ulaya kwa msimu ujao kwani walipoteza mchezo wa fainali katika Kombe la Europa baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Tottenham kwenye Uwanja wa San Mamés, Bilbao, Hispania.