Mamelodi yaanza kibabe Kombe la Dunia ikivuna Sh5.3 bilioni

Muktasari:
- Afrika inawakilishwa na timu nne katika Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani ambazo ni Al Ahly, Esperance, Mamelodi Sundowns na Wydad Athletic.
Mamelodi Sundowns imeanza vyema Fainali za Kombe la Dunia la Klabu kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ulsan HD katika Uwanja wa Orlando, matokeo ambayo yamewafanya wawakilishi hao wa Afrika kuvuna Dola2 milioni (Sh5.3 bilioni)
Kiwango hicho cha fedha kinatolewa kwa kila timu inayoibuka na ushindi katika mechi ya hatua ya makundi ya mashindano hayo ambayo yanashirikisha timu 32.
Timu ambayo inapata matokeo ya sare kwenye hatua hiyo ya makundi, inavuna kitita cha Doła 1 milioni (Sh2.6 bilioni).
Katika mchezo huo ambao ulichezwa leo Juni 18, 2025 saa 7:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki, bao pekee la ushindi la Mamelodi Sundowns limefungwa na Iqraam Rayners katika dakika ya 36 akimalizia pasi ya Lucas Ribeiro.
Rayners angeweza kuandika historia ya kufunga mabao matatu (hat trick) katika mechi hiyo lakini mabao yake mawili yalikataliwa kutokana na sababu tofauti baada ya refa kutumia msaada wa teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR).
Alifunga katika dakika ya 29 lakini ikaonekana mpira ulishikwa na mkono na lingine akapachika katika dakika ya 39 halikuhesabiwa kwa vile alionekana ameotea.
Ushindi huo unaifanya Mamelodi Sundowns kuwa timu ya kwanza ya Afrika kupata ushindi katika mashindano hayo baada ya mwanzo ambao haukuwa wa kuridhisha wa Al Ahly na Esperance.
Al Ahly ilianza kwa kutoka sare tasa na Inter Miami na Esperance ilichapwa mabao 2-0 na Flamengo.
Leo wawakilishi wengine wa Afrika kwenye mashindano hayo, Wydad AC watatupa karata yao ya kwanza katika mashindano hayo ambapo watakabiliana na Manchester City.
Mchezo huo utaanza saa 1:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki na utachezwa katika Uwanja wa Lincoln Financial Field jijini Philadelphia.