Al Ahly yampiga faini mchezaji kisa kukosa penalti

Muktasari:
- Trezeguet alikosa penalti hiyo baada ya kipa wa Inter Miami, Oscar Ustari, kuokoa.
Mshambuliaji wa Al Ahly ya Misri, Mahmoud Hassan maarufu kama Trezeguet, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kukosa mkwaju wa penalti katika mchezo wao dhidi ya Inter Miami katika michuano ya Kombe la Dunia la Kilabu.
Katika mchezo huo uliochezwa Jumapili usiku kwenye Uwanja wa Hard Rock, Marekani, mabingwa hao wa Misri walitoka suluhu na Inter Miami ya Marekani anayochezea Lionel Messi.
Tukio lililozua gumzo kubwa lilitokea dakika tano kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, ambapo Al Ahly walipata penalti baada ya Zizo kuangushwa kwenye eneo la hatari. Hata hivyo, sintofahamu ilizuka baada ya Trezeguet kuchukua jukumu la kupiga penalti hiyo, licha ya kuwepo kwa mpangilio wa timu unaomtaja mshambuliaji, Wissam Abu Ali kama mpigaji wa kwanza wa penalti.
Trezeguet alikosa penalti hiyo baada ya kipa wa Inter Miami, Oscar Ustari, kuokoa kwa ustadi mkubwa. Kwa mujibu wa ripoti kutoka mtandao wa WinWin zinasema kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa Al Ahly, Mohamed Youssef, alichukua hatua ya kumtoza faini Trezeguet kwa mujibu wa kanuni za ndani ya klabu hiyo.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa nyota huyo wa zamani wa Aston Villa amekubali adhabu hiyo na tayari ameomba radhi kwa kocha wake, Jose Riveiro, pamoja na wachezaji wenzake kutokana na kitendo hicho kilichoonekana kama kukaidi maagizo ya benchi la ufundi.
Akizungumza kupitia kituo cha redio na kunukuliwa na tovuti ya Kooora, nyota wa zamani wa Al Ahly, Alaa Maihoub, amesema:
"Haiingii akilini kwa Trezeguet kupiga penalti ilhali tayari kulikuwa na mpangilio wa mchezaji ambaye anastahili kufanya hivyo. Wissam Abu Ali ndiye aliyekuwa kwenye orodha ya kupiga penalti, na kwa kuwa Trezeguet ni mmoja wa wachezaji wakongwe, alipaswa kuheshimu utaratibu huo."
Maihoub ameongeza kuwa anampenda Trezeguet na anaamini bado ana mchango mkubwa kwenye kikosi hicho, lakini amesisitiza kuwa nidhamu ni muhimu kwa mafanikio ya timu yoyote.
Al Ahly imesalia na michezo miwili katika kundi A ambapo Juni 19 itavaana na Palmeiras ya Brazil kisha kucheza mechi ya mwisho Juni 24 dhidi FC Porto ya Ureno.
Katika kundi hilo hakuna timu iliyopata ushindi kwenye michezo ya kwanza ambapo timu zote zina pointi moja huku kila timu ikiwa na nafasi ya kufanya vizuri iwapo itashinda michezo iliyosalia.