Waarabu wawahi mapema mastaa Yanga, Simba

Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu ikiwa na pointi 73 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 72.
Kwa idadi ya pointi ambazo Yanga na Simba kila moja imekusanya kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, timu hizo mbili zimeshajihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Yanga inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 73 na Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 72 hivyo zote zitakuwepo katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mujibu wa kanuni za ligi.
“Uteuzi wa Uwakilishi wowote wa Mashindano yoyote ambao msingi wake unatokana na Ligi Kuu utafuata ubora wa nafasi ya timu husika katika msimamo wa Ligi Kuu. Timu yoyote itakayochaguliwa kucheza mashindano yatakayoandaliwa ama kuidhinishwa na TFF kutokana na nafasi yao katika
Ligi Kuu itawajibika kucheza,” inafafanua kanuni ya 8(xiv).
Lakini wakati wakati mastaa wa Simba na Yanga wakiwa na uhakika na tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, wanapaswa kufahamu kuwa kuna timu 11 vigogo tayari nazo zimeshajihakikishia kushiriki mashindano hayo msimu ujao baada ya kufanya vizuri kwenye Ligi zao.
Vigogo hivyo 11 hapana shaka vitawalazimisha nyota wa Simba na Yanga kufanya kazi ya ziada kupenya kuingia nusu fainali, fainali au kutwaa kabisa ubingwa wa mashindano hayo, ndoto ambayo imekuwa ikiotwa kwa muda mrefu na timu hizo mbili kubwa hapa nchini.
Katika vigogo hivyo 11, kuna timu nane kutoka mataifa yanayozungumza lugha ya Kiarabu ambayo timu zake zimekuwa zikifanya vyema kwenye mashindano hayo na mengine ya klabu Afrika.
Misri imeshapata wawakilishi wawili ambao ni Al Ahly na Pyramids zilizomaliza katika nafasi mbili za juu kwenye ligi yao.
Ahly ndio Mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa wametwaa taji mara 12 na Pyramids FC ndio bingwa wa msimu wa 2024/2025 baada ya kuwachapa Mamelodi Sundowns.

Sudan tayari ishapata wawakilishi wawili ambao ni Al Hilal iliyowahi kucheza fainali ya mashindano hayo mara mbili tofauti na nyingine ni El Merreikh ambayo imewahi kuingia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mara moja.
Tunisia katika msimu ujao itawakilishwa na Mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Esperance na mwakilishi wao mwingine ni Monastir.
Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, RS Berkane wataiwakilisha Morocco ambapo watakuwa sambamba na FAR Rabat ambayo mwaka 1985 iliwahi kuchukua Kombe la Klabu Bingwa Afrika.
Mbali na timu hizo za Kiarabu, Yanga na Simba zitakumbana na vigogo vingine vitatu kutoka Kusini mwa Afrika.
Mabingwa mara moja moja wa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates wamepata tiketi ya kuiwakilisha Afrika Kusini baada ya kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye Ligi Kuu yao.

Timu nyingine ni Petro Luanda ya Angola ambayo msimu wa 2021/2022 ilifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika