Prime
Fadlu atoa muelekeo mpya Simba

Dar es Salaam. Kocha wa Simba SC, Fadlu Davids, amesema sasa wanakwenda kujiandaa dhidi ya dabi ya Kariakoo.
Simba ilipitia mlolongo mgumu wa mechi tatu kuanzia Mei 25 hadi Mei 31. Ilianza kwa kucheza fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco, mchezo uliochezwa Zanzibar na kuisha kwa sare ya 1-1. Matokeo hayo yaliifanya Simba ipoteze taji hilo kwa jumla ya mabao 3-1, baada ya kuchapwa 2-0 katika mechi ya kwanza mjini Berkane.
Siku tatu baadaye, Mei 28, Wekundu wa Msimbazi walirudi dimbani kucheza mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida Black Stars na kushinda kwa bao 1-0. Ushindi huo ulishusha presha kwa mashabiki, lakini uchovu uliendelea kuwaangukia wachezaji.
Mei 31, Simba ilikutana tena na Singida BS lakini safari hii ikiwa katika nusu fainali ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa huko Babati, Manyara, na kuambulia kipigo cha mabao 3-1 kilichowaondoa rasmi kwenye ndoto ya kutwaa taji hilo.
Akizungumza na Mwananchi, Fadlu alisema wanakwenda mapumziko na wakirejea wanaanza maandalizi ya dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga.
"Tulicheza mechi yetu ya tatu ndani ya siku sita. Ilikuwa ni ratiba ngumu mno kwa wachezaji wetu. Fainali ya CAF ilituchosha kimwili na kiakili, kisha ndani ya muda mfupi tukacheza mechi ya ligi kabla ya nyingine ya nusu,"
"Hakika kipindi cha kwanza dhidi ya Singida BS kwenye FA kilituumiza. Mabao yale mawili ya mwanzo ndiyo yalibadili mchezo mzima."
Akitazama mbele, Fadlu ameweka matumaini yake katika mapumziko ya FIFA, ambapo baadhi ya nyota wake kama vile, Ally Salim, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Abdulrazack Hamza, Valentino Mashaka na Kibu Denis wameitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Hata hivyo, kocha huyo raia wa Afrika Kusini anaamini wachezaji waliobaki watarejea na nguvu mpya, huku wale walioko kwenye timu za taifa wakitunzwa vyema kabla ya kurejea kwa maandalizi ya dabi.
"Tuna zaidi ya wachezaji saba walioko kwenye timu za taifa, lakini kwa wale waliobaki, tutatumia muda huu kuwapa mapumziko, kuwajenga upya kimwili na kiakili."
"Tunajua umuhimu wa mechi dhidi ya Yanga. Hii ni Dabi ya heshima, Dabi ya historia, na tutakuwa tayari. Tumecheza mechi kubwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, na sasa tupo tayari kuonyesha kuwa Simba bado ni Simba."
Mechi ya watani wa jadi kati ya Simba dhidi ya Yanga inatarajiwa kuchezwa Juni 15 baada ya mapumziko ya FIFA, huku mashabiki wakisubiri kuona kama Simba itaweza kurejesha heshima baada ya kukosa kombe la Shirikisho Afrika na kuondolewa kwenye FA.
"Tuna muda sasa wa kurekebisha makosa, kuboresha kasi yetu na kurejesha kasi ya ushambuliaji. Mashabiki wetu wanahitaji kuona Simba inayopambana, inayotaka ushindi, na hiyo ndiyo tutakayoipeleka Derby," aliongeza.
Simba yenye pointi 72 na Yanga ikiwa na 73 zimepishana pointi moja tu kwenye msimamo wa ligi hivyo matokeo ya mechi hiyo ya Kariakoo Dabi yanatarajiwa kuamua vita ya ubingwa msimu huu zikiwa zimesalia raundi tatu tu kabla ya msimu kutamatika.
Hata hivyo, Yanga bado imeshikilia msimamo kuwa haitacheza mchezo huo wa dabi hadi mamlaka za soka nchini zitakapoeleza kwanini mchezo huo uliokuwa umepangwa kupigwa Machi 8 haukuchezeka.
Siku moja kabla ya mechi Simba iliandika barua kuwa haitacheza mchezo huo baada ya kuzuiwa na wanaodaiwa kuwa walinzi wa Yanga kuingia Uwanja wa Mkapa kufanya mazoezi ya mwisho na baadaye Bodi ya Ligi ilitangaza kuuahirisha mchezo huo.