Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Ubingwa Ligi Kuu Bara umefichwa hapa

Dar es Salaam. Kariakoo Dabi iliyopangwa kuchezwa Juni 15, mwaka huu, inaweza kuamua timu gani kati ya Yanga na Simba ina nafasi kubwa ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kufuatia hivi sasa timu hizo kutofautiana pointi moja pekee huku zikibakiza mechi tatu. Yanga inazo 73 kileleni, inafuatia Simba yenye 72, zote zikishuka dimbani mara 27.

Katika mechi hizo tatu zenye pointi tisa zilizoshikilia ubingwa, ratiba inaonyesha Yanga itacheza mbili nyumbani dhidi ya Simba na Dodoma Jiji, moja ugenini ikienda kukabiliana na Tanzania Prisons, timu iliyopo kwenye hatari ya kucheza mechi za mtoano 'play off' kuepuka kushuka daraja.

Kwa upande wa Simba, itacheza mbili ugenini dhidi ya Yanga na KenGold iliyoshuka daraja mapema, kisha moja nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, nayo imeshuka daraja.

Ratiba hiyo inaonekana kuibeba zaidi Simba kwani hivi sasa kuna mgomo wa Yanga kutokubali kwenda kucheza mechi ya dabi ikiwa na kauli yao kwamba: "Hatuchezi."

Mchezo huo wa dabi uliopangwa kuchezwa Juni 15 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni, Yanga inasisitiza haichezi kufuatia kutoridhishwa na uamuzi wa kuahirishwa ule wa kwanza uliotakiwa kufanyika Machi 8, 2025.

Kuahirishwa kwa mchezo huo ambapo Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilianisha sababu mbalimbali za uamuzi wake juu ya hilo ikiwemo madai ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi uwanja wa mechi siku moja kabla. Yanga ikaenda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) jijini Lausanne,Uswisi kupeleka malalamiko yake kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo, lakini CAS iliirudisha katika mamlaka za soka za ndani huku Yanga ikiibuka kwa kusema haina imani nayo hivyo imeamua kutocheza mechi hiyo.

Endapo Yanga itashikilia msimamo huo huku ratiba ikiendelea kama ilivypangwa, kanuni za ligi zinabainisha adhabu kwa timu itakayoshindwa kufika uwanjani kwa mechi moja bila ya sababu za msingi ni kukatwa pointi 15 na faini.

Hiyo itamaanisha kwamba Simba itapewa pointi tatu na mabao matatu, huku Yanga ikikabiliwa na adhabu ya kupokwa pointi 15 ambazo moja kwa moja itafanya kupoteza nafasi ya kubeba ubingwa kwani itakuwa nazo 58 na Simba 75 zikibaki mechi mbili. Yanga ikishinda mechi hizo mbili zitakazobaki, itamaliza na pointi 64 kwenye nafasi ya pili.

Kama mchezo huo utafanyika, basi matokeo yatatoa picha ya timu itakayokwenda kubeba ubingwa. Ikiwa sare, Yanga itakuwa na pointi 74 na Simba 73. Mbio zitabaki kwenye mechi mbili ambapo moja nyumbani na nyingine ugenini.

Simba itakwenda ugenini kukabiliana na KenGold kisha kumalizia nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, timu hizo zote zimeshuka daraja na rekodi zinaonyesha duru la kwanza Simba ilishinda zote. Iliichapa KenGold 2-0, ikaikanda Kagera 5-2.

Yanga itaifuata Tanzania Prisons na kumalizia nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji. Duru la kwanza, Yanga iliichapa Tanzania Prisons 4-0, pia ushindi kama huo dhidi ya Dodoma Jiji.

Akizungumzia mchezo huo wa Juni 15 ambao umekuwa na pande mbili za wanaocheza na hawachezi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Steven Mguto, alisema: "Tumeshapanga tarehe, basi tusubiri."

Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, inapambana kutetea ubingwa iliouchukua kwa misimu mitatu mfululizo, huku ikisaka rekodi ya Simba ya misimu ya karibuni ilipochukua taji hilo mara nne mfululizo kuanzia 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021. Ingawa Yanga imewahi kuwa timu ya kwanza kuchukua mara tano mfululizo 1968, 1969, 1970, 1971 na 1972, Simba ikalipa 1976, 1977, 1978, 1979 na 1980.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alisema: "Tunakwenda kwenye Kalenda ya FIFA, tutakuwa na mapumziko, tukirejea tutajiandaa na mechi tatu zilizobaki.

"Kwa mechi zilizobaki, tunapaswa kuwa makini kwani kila moja ina umuhimu wake, tutakuwa na muda mwingi wa kujiandaa tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzo. Tunataka kushinda kila mechi, hivyo tutacheza kama fainali."

Hivi karibuni, Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi, alisema wao wamebakiza mechi mbili za ligi ambazo watazicheza vizuri kuhakikisha wanamaliza salama.

"Lengo letu kuu ni moja tu, kushinda kila mechi ambayo ipo mbele yetu. Tunahitaji kuwa mabingwa msimu huu, hilo lipo wazi,” alisema Hamdi.