Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lamine Yamal kijana wa miaka 17 anayetikisa dunia ya soka

Muktasari:

  • Mwaka 2024 alikuwa mwanamichezo aliyesakwa zaidi kupitia Google nchini Hispania, na wa pili kwa umaarufu mitandaoni nchini Uingereza.

Barcelona, Hispania. Katika umri wa miaka 17 tu, Lamine Yamal tayari ameandika historia kwenye soka akiibuka kama mmoja wa wachezaji hatari zaidi duniani, akiwa ni miongoni mwa wanasoka wenye mvuto na uwezo wa kipekee. Kijana huyo wa Barcelona ameonesha ukomavu wa ajabu, akifunga mabao muhimu kwa ustadi mkubwa na kuvutia mashabiki duniani kote. Kwa kasi hii, wengi wanaamini kuwa Yamal ni uso mpya wa Barcelona na soka la dunia.

Yamal mwenye umri wa miaka 17 amefikisha mechi 100 kwenye mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Olímpic Lluís Companys tangu alipoanza kuichezea Barcelona Aprili 29. 2023, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Hispania “La Liga” dhidi ya Real betis.

Katika kipindi hicho kigumu cha mikopo, mauzo ya wachezaji na kushindwa kusajili majina mapya kwa ajili ya mashindano ya La Liga, ghafla Barca wakajikuta wamepata kipaji kisicho cha kawaida kutokea La Masia kilichokuja na majina mengine kama Gavi, Pedri, Pau Cubarsí, Fermín López na Alejandro Balde kinachoonekana kuwa na uwezo wa kufikia viwango vya nyota waliovuma chini ya Pep Guardiola mwishoni mwa miaka ya 2000.

Ripoti zinaonesha kuwa Xavi alikuwa na mchango mkubwa kuhakikisha Yamal anabaki Barcelona, hasa baada ya matajiri wa Paris Saint-Germain (PSG), kuvutiwa na uwezo wa kijana huyo mwenye umri wa miaka 15 kwa wakati huo.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Xavi alimuahidi Yamal kuwa angepata nafasi katika kikosi cha kwanza iwapo angesaini mkataba wake wa kwanza na klabu hiyo. Gwiji huyo wa Barcelona alitimiza ahadi yake na kumpa Yamal mechi ya kwanza mwezi Aprili 2023, akiwa na umri wa miaka 15, miezi tisa na siku 16 na hivyo kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuichezea timu hiyo ya wakubwa.

Yamal naye alitimiza sehemu yake ya makubaliano na kutia saini mkataba ambao uliambatana na kipengele cha kuuvunja chenye thamani ya ajabu ya euro bilioni moja.

"Tunapokea ofa za kichaa kwa wachezaji kama Lamine Yamal, lakini tunazikataa bila kusita," alisema rais wa Barcelona, Joan Laporta, mwezi uliopita. "Tunamwamini Lamine na hatuhitaji kumuuza."

Tupuuze umri wake Yamal amepitia miaka miwili ya mafanikio ambayo ni wachache sana wanaweza kuifikia katika maisha yao yote ya soka. Mwaka 2024 alikuwa mwanamichezo aliyesakwa zaidi kupitia Google nchini Hispania, na wa pili kwa umaarufu mitandaoni nchini Uingereza.

Yamal alizaliwa mwaka 2007 kwa wazazi Mounir Nasraoui na Sheila Ebana na akalelewa katika mji wa Mataró, kaskazini mwa Barcelona. Katika mashindano ya Euro 2024, ambayo aling'ara na kutajwa kuwa mchezaji bora chipukizi wa mashindano, Yamal aliendelea kuiheshimu asili yake kwa kusherehekea mabao kwa ishara ya ‘304’ nambari ya msimbo wa posta ya mtaa alikokulia.

Katika msimu wake wa kwanza, alicheza dakika saba pekee za La Liga dhidi ya Real Betis. Lakini msimu uliofuata ulimtambulisha rasmi kwa ulimwengu akawa kipenzi cha mashabiki wa soka duniani kote.

Baada ya kufikisha idadi ya mechi 100 alizoichezea Barcelona, mshambualiaji huyu raia wa Hispania amevunja baadhi ya rekodi akiwa ndiye mchezaji mdogo zaidi ndani ya timu hiyo kufikisha mechi 100 baada ya Messi kufanya hivyo akiwa na miaka 20, Gavi miaka 20, Bojan miaka 19, Pedri miaka 20 pamoja na Ansu Fati miaka 20.

Kwa kuangalia takwimu za moja kwa moja, bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kukua na kufanya vizuri katika soka kwani mechi 49 alizocheza na Blaugrana msimu huu, amefunga mabao 15 na kutoa pasi 24 za mabao.

Lakini jambo la kushangaza zaidi kuhusu kinda huyu ni uwezo wake wa kucheza kwa ubora wa hali ya juu kwenye mechi kubwa.

"Katika mechi kubwa, yeye hujitokeza, na nadhani huwa anafurahia presha hiyo," alisema kocha wake Hansi Flick baada ya mchezo wa kuvutia wa sare ya 3-3 dhidi ya Inter Milan jana.

Kocha huyo Mjerumani alikubaliana na kauli ya kocha mwenzake Simone Inzaghi kuwa winga huyo ni ‘kipaji cha kipekee’, akiongeza: “Ninafurahi sana kuwa na kipaji kama hiki, ambacho kama kweli hutokea kila baada ya miaka 50, basi kimetokea kwa Barcelona.”

Mechi hiyo ya 100 kwa kinda huyo akiwa na jezi ya Barcelona. Katika muda huo, tayari ana mabao 22 na pasi za mabao 27 akiwa amehusika katika mabao 49.

Katika mechi 100 za mwanzo za Messi akiwa Barcelona alipokuwa na umri wa miaka 20 alifunga mabao 41 na pasi za mabao 15, akihusika katika mabao 56.

Ulinganisho wake na Messi umechochewa hata na familia yake mwenyewe kwani mwaka jana, baba yake alidai kwamba mwanaye anaweza kuwa bora zaidi ya mshindi huyo wa Ballon d’Or mara nane, huku mama yake akiwa sehemu ya picha maarufu kwenye kalenda ya hisani akiwa pamoja na Messi, ambapo anaonekana akimwogesha Lamine akiwa bado mchanga na inaelezwa kuwa Messi alimtabiria makubwa.

Wengi wakimuona kama mmoja ya wachezaji bora kuwahi kutokea duniani, hivi karibuni amepuuza kulinganishwa kwake na Messi ambaye alitamba kwa miaka 17 ndani ya timu hiyo.

Akizungumza na Daily Mail, Yamal amesema:

“Sijilinganishi naye, kwa sababu sijilinganishi na mtu yeyote, na hasa kabisa si na Messi,” Yamal aliwaambia waandishi wa habari.Tunafikiria kuhusu kujiboresha kila siku, na kuwa bora zaidi siku inayofuata.

“Hivyo sidhani kama kulinganisha kuna maana, hasa zaidi na Messi. Ninamheshimu bila shaka, kama mchezaji bora wa kihistoria, lakini sijilinganishi naye,” amesema Yamal.

Yamal, akiwa na umri wa miaka 17 tu, tayari amepata ushirikiano wa kibiashara na makampuni makubwa duniani, ikiwa ni pamoja na Beats Electronics, Powerade, Oppo, na Konami, pamoja na mkataba mkubwa na Adidas. Kabla ya Krismasi mwaka jana, kampuni ya Adidas ilitoa mfululizo mpya wa viatu vya F50 na LY304, vilivyokuwa na herufi zake na nambari ya posta ya eneo alikozaliwa, Rocafonda.

Yamal sasa ni mmoja wa watu maarufu zaidi katika soka, akichipukia wakati ambao kama akicheza vibaya hata mechi moja tu, watu mtandaoni wanaweza kumtukana au kumsema vibaya sana. Lakini kama akicheza vizuri sana, anaweza kupewa sifa kubwa hadi kufikiriwa kushinda tuzo kubwa ya Ballon d'Or.