Ilichosema TEC kushambuliwa kwa Padri Kitima

Muktasari:
- Baraza hilo limesema hadi sasa linapata ushirikiano kutoka kwa Serikali na vyombo vya usalama katika tukio hilo.
Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limetaka hatua za haraka kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika na shambulizi dhidi ya Katibu Mkuu wa baraza hilo, Padri Charles Kitima.
Baraza hilo limesema hadi sasa linapata ushirikiano kutoka kwa Serikali na vyombo vya usalama.
TEC imekuja na wito huo, siku moja baada ya taarifa ya kushambuliwa Padri Kitima tukio lililotokea usiku wa jana katika eneo la makazi na makao makuu ya baraza hilo, Kurasini, Temeke jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema linamshikia mtu mmoja mkazi wa Kurasini, Rauli Mahabi kuhusiana na tukio hilo na kwamba mahojiano na uchunguzi zaidi unaendelea ili kuchukua hatua kali na haraka dhidi ya waliohusika.
Taarifa ya TEC iliyotolewa leo, Alhamisi Mei 1, 2025 na kusainiwa na Makamu wa Rais wa baraza hilo, Askofu Euswebius Nzigilwa imeeleza Padri Kitima alipata majeraha na amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Baraza hilo, limetoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka, kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika katika kupanga na kufanya uhalifu huo.
"Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huu wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria," imeeleza taarifa hiyo.
TEC imetaka uchunguzi wa tukio hilo ufanyike kwa haraka na taarifa zilitolewe kwa uwazi, bila upotoshaji wowote ili kurudisha imani na matumaini kwa watu.
Katika taarifa hiyo, TEC imeeleza hadi sasa inapata ushirikiano kutoka serikalini na kwa vyombo vya usalama.
"Pia tunawashukuru watu binafsi, taasisi za ndani na za kimataifa zinazoendelea kulaani na kutupa pole kwa tukio hili baya na la aibu kwa Taifa letu," amesema.
Baraza hilo limewataka waumini waendelee kumuombea neema ya uponyaji Padri Kitima, pia kuliombea Taifa amani na umoja.
Aidha, limewasihi kuwa na subira na uvumilivu wakati matokeo ya uchunguzi wa vyombo vinavyohusika yakisubiriwa.
"Tunawashukuru wote waliomsaidia na kumfikisha Padri Kitima hospitalini mapema pia madaktari na wauguzi wanaomhudumia mpaka sasa." imeeleza.