Chadema yamvua uanachama Mrema, mwenywe ajibu

Muktasari:
- Mrema amesema yeye ni mwanachama wa Chadema mwenye kadi ya uanachama namba 0111 na anatambulika kwa namba za kadi kwa mujibu wa Kanuni ya 5.1 na 5.2
Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tawi la Bonyokwa likitangaza kumvua uanachama John Mrema, kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ukaidi, mwenyewe amekana kufukuzwa uanachama.
Tuhuma zingine anazodaiwa Mrema aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, sababu nyingine zilizotajwa ni pamoja na dharau dhidi ya mamlaka, kutoheshimu miiko, tamaduni na misingi ya chama.
Taarifa za Mrema kuvuliwa uanachama zimesambaa leo Jumatano Aprili 30, 2025 kupitia barua hiyo iliyoandikwa na Solomini Kagaruki kwa niaba ya Katibu wa tawi la Bonyokwa.
Inadaiwa Mrema alidharu mamlaka ya nidhamu kwa kuibeza barua husika na kuisambaza katika mitandao ya kijamii badala ya kutumia muda kujieleza mbele ya uongozi wa tawi lake.
Kagaruki amesema licha ya Mrema kutakiwa kujieleza, lakini aliendelea kutenda kosa kwa kuendelea kupinga na kudhihaki msimamo na program za chama akifanya hivyo katika mkutano na wanahabari uliofanyika Aprili 22, 2025.
“Uliendelea kushikilia msimamo wako wa kukituhumu chama hadharani huku ukijua kuwa sio utamaduni wa Chadema na wala sio misingi. Baada ya mjadala wa kina kuhusu tuhuma zako, kamati imefikia uamuzi kuwa umepoteza sifa za kuwa mwanachama wa Chadema.”
“Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema 2006 toleo la 2019 ibara 5.4.3 umevuliwa uanachama rasmi ndani ya tawi la Bonyokwa kuanzia tarehe ya barua hii, lakini unayo fursa ya kukata rufaa kwa ngazi ya juu kama hujaridhika na adhabu hii,” amesema Kagaruki kupitia barua hiyo iliyokwenda nakala kwa Katibu Mkuu wa Chadema.
Baada barua hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema Brenda Rupia ameandika katika mtandao wa X kuwa; “Ofisi ya Katibu Mkuu imepokea nakala ya barua hii kutoka kwa uongozi wa tawi la Bonyokwa kuwa John Mrema amefukuzwa uanachama kwa mamlaka ya ibara ya 7.2.11. Barua imepokelewa na imewekwa kwenye jalada.”
Mwananchi imemtafuta Rupia ambaye amekiri kuwa ofisi imepokea barua hiyo ya kufukwazwa uanachama wa Mrema.
Katika taarifa yake kwa umma, Mrema amesema yeye ni mwanachama wa Chadema mwenye kadi ya uanachama namba 0111 na anatambulika kwa namba za kadi kwa mujibu wa Kanuni ya 5.1 na 5.2
“Barua inayosambaa hainihusu mimi kwa sababu haikutaja namba ya uanachama wangu labda kuna mtu tunafanana majina,” amesema Mrema.
Amesema chama hicho ni cha kimtandao, hata kadi yake ya uanachama ambayo inadaiwa amefutwa uanachama haikutajwa.
“Hivyo inawezekana kabisa barua hii hainihusu hata kidogo,”amesisitiza Mrema.
Amesema tawi lake sio Bonyokwa akidai amesajiliwa tawi la Makongo na taarifa hizo zinapatikana kwenye mfumo wa kidigitali wa Chadema.
Amesema kwa mujibu wa kanuni za chama Kanuni ya 5.3. (imeweka utaratibu wa mwanachama kutakiwa kuwasilisha taarifa zake kwa katibu wa tawi pindi anapohama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.
“Hivyo kuishi eneo husika halihalalishi kuwa tayari ni mwanachama wa tawi husika wakati utaratibu wa kanuni husika haujafuatwa na ndio maana sijawahi kushiriki kikao chochote cha tawi la Bonyokwa kwa sababu si tawi langu.
“Tawi la Bonyokwa hawana mamlaka ya kunivua uanachama kwa sababu sio mwanachama wa tawi hilo. Mimi ni mwanachama halali wa Chadema hadi hapo nitakapochukuliwa hatua kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za chama,” amesema Mrema.