Raphina akaribia rekodi ya Messi

Muktasari:
- Huu ulikuwa mchezo wa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Ulaya, mchezo ambao ulifanyika kwenye Uwanja wa Camp Nou, nchini Hispania.
Barcelona, Hispania. Staa wa Barcelona Raphinha amefanikiwa kuvunja rekodi nyingine ya timu hiyo iliyokuwa imeweka na ali yekuwa staa wao Lionel Messi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Inter Milan.
Huu ulikuwa mchezo wa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa Ulaya, mchezo ambao ulifanyika kwenye Uwanja wa Camp Nou, nchini Hispania.

Raphina ambaye amefanikiwa kuonyesha kiwango kizuri akiwa na timu hiyo msimu huu, amekuwa akitajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji ambao wanaweza kuwania tuzo ya Ballon d'Or mwishoni mwa msimu huu kutokana na kiwango cha juu alichokionyesha.
Staa huyo raia wa Brazil mwenye miaka, 28, alikuwa na msaada mkubwa kwa timu hiyo baada ya kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kumalizimisha sare hiyo kwa mabao yaliyofungwa na Lamine Yamal, Ferran Torres na la kujifunga la Yann Sommer, huku Inter ikifunga kupitia kwa Marcus Thuram, Denzel Damfries aliyefunga mawili.
Raphinha ambaye alitoa pasi ya bao lilofungwa na Torres, sasa amefanikiwa kuhusika kwenye mabao 20 katika michuano hiyo msimu huu, likiwa ni bao moja zaidi ya Messi ambaye alihusika kwenye mabao 19 mwaka 2021.

Staa wa zamani wa Man United na Real Madrid, Cristiano Ronaldo, ndiye pekee ambaye ana rekodi ya kuhusika kwenye mabao mengi zaidi kwenye msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa nayo 21, lakini bado Raphina inaonekana kuwa anaweza kufika hapo endapo atafanya vizuri kwenye mchezo wa nusu fainali ya pili au fainali.
Kwa ujumla Raphina msimu huu ameshafunga mabao 30 na kutoa pasi 21 za mabao kwenye mechi zote 51 alizoitumikia Barcelona msimu huu akiwa anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu zaidi.

Akizungumzia mchezo huo, beki wa zamani wa Man United Rio Ferdinand, alisema pamoja na Raphina kufanya mambo makubwa, lakini yeye anaamini kuwa Lamine Yamal anastahili tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwishoni mwa msimu.
"Kwa uhalali wa soka la kisasa, naenda mbali zaidi nikiamiani kuwa Lamine Yamal ni mchezaji wa daraja lingine, kwa kutazama wachezaji wa ligi nyingine tano, huyu ni mchezaji wa kiwango cha juu na anaweza kutwaa tuzo ya Ballon d'or mwishoni mwa msimu huu," alisema Rio.