Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha Morocco atoa muelekeo AFCON

Casablanca, Morocco. Kocha wa Morocco, Walid Regragui, ameitaka timu ya taifa kuepuka kujivuna baada ya kufuzu nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), kufuatia ushindi walioupata wakiwa nyumbani wikiendi iliyopita.

Atlas Lions walipata nafasi ya kihistoria ya kufika nusu fainali baada ya kuifunga Cameroon mabao 2-0 katika robo fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah uliojaa mashabiki.

Mabao ya Brahim Diaz na Ismail Saibari, kila mmoja akifunga katika kipindi tofauti cha mchezo, yalihakikisha ushindi wa kukumbukwa huku Morocco ikifikia nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004. Mara ya mwisho Morocco kufika hatua hiyo ilikuwa miaka 22 iliyopita, wakati Regragui bado alikuwa mchezaji.

“Shukrani kwa wachezaji na mashabiki. Tulicheza kana kwamba tuko watu 12 uwanjani, na tulihisi kabisa kuwa nyumbani. Tulicheza kipindi chetu bora cha kwanza tangu Kombe la Dunia au mechi ya kirafiki dhidi ya Brazil,” Regragui aliwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo.

“Ushindi huu unastahili. Tulicheza kwa nguvu kubwa. Wachezaji wetu walitoa kila walichonacho, na wanapobaki makini mambo huenda vizuri. Nimefurahishwa sana na walichokionyesha.”

Aliongeza: “Huu ni ushindi wa kihistoria imepita miaka 22 tangu Wamorocco waione timu yao ya taifa ikifika nusu fainali. Wanastahili. Sasa tunapaswa kubaki wanyenyekevu. Nawapongeza Cameroon na timu yao changa yenye mustakabali mzuri.”

Regragui pia alieleza jinsi alivyowapa hamasa wachezaji wake baada ya mechi ngumu ya hatua ya 16 bora dhidi ya Tanzania, waliyoibuka na ushindi wa bao 1-0 kupitia goli la Diaz dakika ya 64.

“Sikuwa na mpango wa kufanya mabadiliko yoyote kwenye kikosi,” Regragui alieleza. “Tulihitaji kurejesha kujiamini, kuwa chanya na kurekebisha makosa yetu. Tulifanya kazi kwa bidii siku tatu au nne zilizopita.

“Wachezaji walitekeleza tulichopanga. Zaidi ni suala la kisaikolojia. Muhimu zaidi ni kwamba kikosi chetu kimeungana, na tulionyesha hilo dhidi ya Cameroon.”

Akielezea mpango wa mchezo, alisema: “Tulihitaji kushinda mapambano mengi zaidi kuliko dhidi ya Tanzania. Tulipoteza umiliki wa mpira mara nyingi. Tulihitaji kusogea sana na kushinda vita ya kiungo. Bado tuna nafasi ya kuboresha. Tulijibu kama timu kubwa. Tulihitaji kutuma ujumbe.”

“Tunahitaji kubaki wanyenyekevu kwa sababu kila timu inataka kutufunga, na ni lazima tuheshimu wapinzani wote.”

Akizungumzia Diaz, ambaye tayari amefunga mabao matano katika mechi tano za AFCON na anaonekana kuwa mchezaji wa kuamua matokeo kwa Morocco katika toleo la 2025, Regragui alisema:

“Diaz amebadilisha kabisa mtazamo wake. Anakimbia, anapambana, analinda mpira, anatuma ujumbe.

Anafanya kazi kwa ajili ya timu na anatekeleza ninachomtaka. Anaweza kuwa mchezaji bora duniani kama akiamua.”

Kuhusu sababu ya kumtoa dhidi ya Cameroon, alisema: “Diaz hana majeraha. Yuko sawa. Alikuwa amechoka tu, na hilo ni sehemu ya mashindano. Tumekuwa tukiongeza taratibu muda wake wa kucheza kwa sababu hapo awali hakuwa akipata nafasi ya kutosha. Hilo ndilo jambo muhimu zaidi.”

Akizungumzia mechi nyingine ya robo fainali kati ya Algeria na Nigeria, Regragui alisema:

“Ni mataifa mawili makubwa, timu mbili zenye mitindo tofauti. Ikiwa ni Algeria, itakuwa dabi kubwa na sherehe kubwa. Tutafurahi. Timu bora zaidi ndiyo itakayofuzu.”

Kwa upande wa Ismail Saibari alisema lengo la Morocco ni kufika hadi fainali, akiongeza kuwa kikosi hakitapumzika hadi kitimize ndoto hiyo.

“Tayari tumefika nusu fainali, na lengo letu ni kufika fainali. Mashabiki wetu walituunga mkono kwa nguvu na hawakututilia shaka. Sasa tutapumzika, tusubiri kumfahamu mpinzani wetu wa nusu fainali, kisha tuanze maandalizi huku tukirekebisha makosa tuliyofanya awali,” alisema Saibari.

“Tunafanya kazi vizuri kama kikundi ndani ya timu ya taifa ya Morocco, tunafahamiana vizuri, na tunapambana pamoja ili kushinda taji.”

Morocco itakutana na Nigeria katika nusu fainali itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat.