Karia achagua bao la Mzize, agomea la Sakho
Muktasari:
- Pape Sakho alikuwa mshindi wa Tuzo ya Bao Bora Afrika 2022 na Clement Mzize ameshinda tuzo hiyo mwaka 2025.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Wallace Karia amesema kuwa amefurahishwa zaidi na bao la Clement Mzize lililoshinda Tuzo ya Bao Bora Afrika mwaka huu kuliko lile la nyota wa zamani wa Simba, Pape Sakho lililoshinda tuzo hiyo mwaka 2022.
Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo Jumamosi, Novemba 29, 2025, Karia amesema kuwa bao la Mzize limemfurahisha zaidi kwa vile mchezaji huyo ni Mtanzania.
“Mbali ya ligi yetu kuwa bora na kuweza kuheshimika lakini kwa mara ya pili, ligi yetu imetoa goli bora. Tumpongeze kijana wetu Mzize na Yanga Afrika kwa kuweza kumlea.
Bao la kwanza lilikuwa la Sakho. Sikulipenda ingawa Nilifurahi. Wakati anapewa tuzo, Bendera ya Sengela ilionekana na safari hii ni kijana wetu Mzize na bendera ya Tanzania ilikuwa pale,” amesema Karia.
Karia amezipongeza klabu nne za Tanzania kwa kuingia hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika.
“Tumeshuhudia, sasa hivi tumekuwa wazoefu wa kutoa timu nne za kuwakilisha Tanzania katika mashindano ya Klabu Afrika. Pointi tulizonazo mbali na hizi tunazotafuta, zinatupa uhakka wa kuingiza timu nne huko mbele.
“Sisi ni ligi ya nne ambayo imetoa timu nne ambazo zimeingia katika hatua ya makundi. Kazi tuliyonayo ni kuingiza timu nyingi kwenye hatua ya robo fainali.
“Kipekee niwapongeze timu za Yanga, Simba, Singida na Azam FC kwa kuweza kututoa kifua mbele. Sitokubali atokee mtu yeyote asababishe hizi timu zisifanye vizuri. Sitomsamehe,” amesema Karia.