Kipre Junior arejea Azam akikimbia benchi Uarabuni
Muktasari:
- Katika msimu wa 2023/2024, Kipre Junior aliifungia Azam FC mabao 10 katika mechi 13 za Ligi Kuu ya NBC.
Azam imemrudisha winga Kipre Junior baada ya kumnunua kutoka MC Alger ya Algeri aliyoitumikia kwa misimu miwili iliyopita.
Klabu hiyo imethibitisha usajili wa Kipre Junior mwenye umri wa miaka 26 anayemudu kucheza winga za kulia na kushoto.
“Mchezaji mpya amesajiliwa. Tunayo furaha kuwataarifu kuwa tumemrejesha nyota wetu wa zamani Kipre Junior baada ya kumnunua kutoka klabu ya MC Alger. Karibu nyumbani Kipre Junior,” imeandika Azam FC katika kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Kipre Junior anarudi Azam baada ya kuitumikia kwa misimu miwili MC Alger inayoshiriki Ligi Kuu ya Algeria.
Licha ya kuondoka Azam mwaka 2023 akiwa mchezaji tegemeo, nyota huyo raia wa Ivory Coast alikuwa na wakati mgumu ndano ya MC Alger kutokana na kutopata mara kwa mara nafasi ya kuanza kikosini.
Katika mechi 76 za mashindano tofauti ambazo Kipre Junior ameichezea MC Alger, alianza katika kikosi cha kwanza mara 48 na kuanzia benchi mara 28.
Kabla hajaondoka Azam FC, Kipre alionyesha kiwango bora katika msimu wa 2023/2024 ambao alimaliza akiwa ameifungia timu hiyo mabao 10 katika mechi 13 za Ligi Kuu ya NBC.