Miujiza pekee kuinusuru Tanzania Prisons Ligi Kuu
Muktasari:
- Tanzania Prisons inakabiliwa na kibarua kigumu cha kupindua matokeo ya kichapo cha mabao 4-0 iliyopata katika mechi ya kwanza dhidi ya Polisi Tanzania ugenini.
Dakika 90 zimesalia kuamua hatma ya Tanzania Prisons kubaki katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ukweli unaonekana kuwa mchungu kwa timu hiyo ya jijini Mbeya.
Kesho Alhamisi, Julai 16, Tanzania Prisons itaingia kwenye Uwanja wa Sokoine kuikaribisha Polisi Tanzania katika mchezo wa marudiano wa mtoano wa kuwania nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu wa 2026/27, ikikabiliwa na kazi ngumu ya kupindua matokeo.
Baada ya kuchapwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Ushirika, Moshi, Tanzania Prisons sasa inalazimika kushinda kwa tofauti ya mabao matano ili kubadilisha matokeo na kujihakikishia kubaki Ligi Kuu.
Lakini hizo zinaweza kuwa hesabu ngumu ambazo kwa kiwango ilichoonyesha kwenye mchezo wa kwanza, zinaonekana kuwa mbali na uhalisia.
Kinachotia hofu si matokeo pekee, bali namna timu ilivyoshindwa kuhimili presha ya mchezo. Ilianza kuruhusu bao la penalti katika dakika ya 15, kabla ya kupoteza umakini zaidi kipindi cha pili ambapo iliruhusu mabao matatu kwa urahisi.
Licha ya Haruna Chanongo kugongesha mwamba dakika ya 27, nafasi ambayo ingeweza kubadilisha sura ya mchezo, Tanzania Prisons bado ilionekana kushindwa kurejea mchezoni, huku safu ya ulinzi ikifanya makosa yaliyoigharimu.
Kwa upande mwingine, Polisi Tanzania ilionyesha utulivu mkubwa, nidhamu ya kiuchezaji na uwezo wa kutumia makosa ya wapinzani wake. Mabao yaliyofungwa na Juhudi Philemon, Tariq Seif, Tatizo Shem na Emmanuel Mpuka yameiweka timu hiyo mlangoni kurejea Ligi Kuu, ikiwa inahitaji kulinda tu faida kubwa iliyopata katika mchezo wa kwanza.
Changamoto nyingine kwa Tanzania Prisons ni kwamba kadri muda utakavyokwenda bila kupata mabao ya mapema, ndivyo presha itakavyoongezeka. Hali hiyo inaweza kuwafanya wachezaji waathirike kisaikolojia na kuzima matumaini ya kubaki Ligi Kuu.
Ingawa soka limewahi kushuhudia timu zikipindua matokeo, hali ya Tanzania Prisons kwa sasa inaonyesha kuwa inahitaji zaidi ya uwezo wa kawaida ili kubadili matokeo hayo. Mechi ya kesho si ya kutafuta ushindi pekee, bali ni ya kupigania uhai wa klabu katika Ligi Kuu.
Iwapo Polisi Tanzania itafanikiwa kulinda faida ya mabao manne iliyonayo, Tanzania Prisons itaaga rasmi Ligi Kuu Bara na kushuka Championship, huku Polisi Tanzania ikirejea kwenye Ligi Kuu baada ya kusubiri kwa miaka mitatu tangu iliposhuka daraja msimu wa 2022-2023.