Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HISIA ZANGU: ‘Merry Christmas’ mchungaji wa Dube na Ateba

Muktasari:

  • Inawezekana hakuna mabadiliko mengi nyuma ya pazia. Au inawezekana mabadiliko yapo na inatupasa kuendelea kuchunguza. Kwanza kabisa tujiulize ni kwanini picha za Dube na Ateba zimefika katika mitandao.

Usione kitu cha kawaida. Inachekesha kidogo. Nilipotazama picha za staa wa Yanga, Prince Dube na staa wa Simba, Leonel Ateba wakiombewa kwa mchungaji katika nyakati tofauti nilifikiria mbali. Nilifikiria mpira wetu ulikotoka na ulipo.

Inawezekana hakuna mabadiliko mengi nyuma ya pazia. Au inawezekana mabadiliko yapo na inatupasa kuendelea kuchunguza. Kwanza kabisa tujiulize ni kwanini picha za Dube na Ateba zimefika katika mitandao.

Kuna wachezaji wengi wanaosali na kuswali. Labda hatuoni tu picha zao lakini nawajua wachezaji wengi ambao wanasali. Wapo wengi. Kuhusu Dube na Ateba kilicholeta tofauti ni kwamba picha zao zilipojitokeza katika mitandao ya jamii watu wakaamua kushirikisha suala la ushirikana.

Kwamba wote wawili hapa katikati wamekuwa na viwango vibovu kwahiyo wameenda kuombewa kwa mchungaji ili warudishe viwango vyao. Hii ndio tafsiri ya haraka haraka. Sasa kuna suala la kufikiria hapa. Kuna wanaokwenda katika nyumba za ibada wakiamini kwamba wanafanyiwa vitendo vichafu na wenzao. Na kuna wanaokwenda kwa ajili ya kujiimarisha katika kazi zao na kufanya vema.

Kwa mujibu maneno ya mitaani ambayo yanatokana na mambo tuliyozoea katika mpira wetu ni kama vile Dube na Ateba walikwenda kwa mchungaji kutokana na viwango vyao kushuka kutokana na imani za kishirikana. Huwa inachekesha tunapofikiria hivi lakini hatuna cha kuwafanya wale wote wanaofikiria hivi.

Kuna maisha ya wenzetu halafu kuna maisha yetu. Maisha ya wenzetu wangeamini kwamba Dube ana tatizo la kisaikolojia. Kwamba kucheza Yanga kumemfanya akawa na presha kubwa kwa sababu ni timu kubwa. Kwamba labda alihitaji muda wa kumudu presha ya kucheza katika timu yenye mashabiki wengi kama Yanga baada ya kucheza katika timu ambayo haikuwa na presha kubwa kama Azam.

Kwa Ateba ungeweza kuona kwamba labda alihitaji muda wa kuendana na kasi ya soka la Tanzania. Wengine pia tulikuwa tunamuangalia kwa jicho la kuwa na unene fulani ambao alihitaji kuupunguza kuendana na soka letu.

Haya yote kuanzia ya Dube hadi ya Ateba hayakuwahi kuzingatiwa. Majibu yalionekana kuwa rahisi tu kwamba wachezaji walikuwa wamefanyiwa mambo ya Kiswahili. Kwa Dube ilizungumzwa zaidi kwa sababu watu walikuwa wanafahamu ubora wake tangu akiwa Azam.

Kichekesho kikawa kwamba kuna waliodai kwamba alikotoka, wakimaanisha Azam, hakuwa ameondoka vizuri kwahiyo labda kuna vinyongo vimetupwa chini ya bahari ya Hindi. Wengine wakadai labda katika timu yake ya sasa kuna mambo ya Kiswahili amefanyiwa.

Vyovyote ilivyo kilichonifurahisha kidogo ni kwamba pamoja na yote haya majibu ya hawa washambuliaji yalikuwa ni kwenda kwa mchungaji. Zamani katika mambo kama haya wachezaji walikuwa wanakwenda kwa mganga. Sijui kama Dube na Ateba hawajapelekwa huko lakini tunachojua sisi ni kwamba wameibukia kwa mchungaji.

Labda tunapiga hatua kuachana na imani za kishirikina na sasa maombi yanataka kuchukua nafasi. Labda ni mwanzo mpya. inanikumbusha namna ambavyo zamani tuliamini kwamba dawa ya jeuri ni kiburi. Kwamba namna ya kuondoa ushirikina uliofanyiwa ni kwenda kwa mganga.

Kulikuwa na wizi wa viatu vya mchezaji ambaye unacheza naye namba moja tu. lakini pia unakuta kuna jezi ya mchezaji ambaye unacheza naye nafasi moja. Unapeleka kwa mganga kwa siri vinaenda kufanyiwa mambo mabaya kisha unarudisha kimya kimya na mwenzako anaanza kuharibikiwa mambo yake.

Sisi wengine hatuamini katika mambo haya na tumejikita katika imani ya Mungu pamoja na kuamini katika sayansi ya mpira. Kwamba kwa mchezaji kama Dube baada ya kukosa mabao ya wazi kwa muda mrefu labda alihitaji bao moja tu la kurudisha uwezo wake wa kujiamini na kurudi katika njia.

Kwa wenzetu kule kama mshambuliaji ni tegemeo na ikatokea akawa katika nuksi kama ya Dube huwa anapewa hata penalti na wenzake ili afunge. Mpigaji wa penalti wa kila siku aliyechaguliwa na kocha anaamua tu kumpa penalti Dube ili walau afunge apate nguvu ya kujiamini.

Kitu kingine kilichonichekesha katika janga zima ni namna ambavyo suala la ushirikiana linahusishwa zaidi na wachezaji mmoja mmoja. Siku hizi zile shutuma za kwamba timu haina mganga anayeeleweka zimekuwa zikipungua kila uchao. Nafasi yake imebebwa zaidi na suala la hujuma.

Siku hizi timu kubwa ikifungwa sana wanahisi kwamba wanahujumiwa na watani wao. Timu kubwa ikicheza ovyo inaaminika kwamba inatokana na wachezaji wake kupewa mlungula na watani wao ili wachezaji wacheze kiwango cha chini.

Ni nadra sana kusikia sababu mpya kama hii ya majuzi ambayo waliangushiwa wachezaji wa Yanga kwamba wamekuwa wakiendekeza starehe kupita kiasi. Huwa inatokea mara chache. Hata hivyo, mchezaji mmoja mmoja siku hizi wamekuwa wakijitokeza hadharani na kuamini wamerogwa.