Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bangala anavyosepa na mamilioni Azam FC

Dar es Salaam. Azam FC imeachana na nyota wake raia wa DR Cong, Yannick Litombo Bangala, aliyekuwa amebaki na mkataba wa miezi nane klabuni hapo.

Bangala ambaye alijiunga na Azam, Julai 2023 akitokea Yanga, alisaini mkataba wa miaka miwili uliotakiwa kumuweka Chamazi hadi Julai 30, 2025.

Lakini miezi nane kabla ya kumalizika kwa mkataba wake, Azam FC imeamua kumvunjia mkataba na kumlipa ‘mamilioni’.


ANAOGELEA MAMILIONI

Taarifa kutoka vyanzo vya karibu na mchezaji huyo zinasema Azam FC imemlipa zaidi ya Sh100 milioni za Tanzania kufidia mkataba huo.

"Baada ya mechi ya Tabora, wakala wa Bangala alipigiwa simu na uongozi wa klabu kumwambia wameamua kuachana naye," kilisema chanzo hicho.

Aidha chanzo hicho kikaongeza Azam FC haitaki kushtakiwa Fifa kwa sababu inaharibu jina lao, hivyo wakaomba wayamalize kwa ustaarabu na wao wako tayari kulipa pesa yote mara moja.

"Mshahara wa Bangala ulikuwa Dola 5,000 kwa mwezi, kwa hiyo wamemlipa mshahara wake wote uliobaki wa miezi minane," kilimalizia chanzo chetu.

Kwa maana rahisi ni Bangala alilipwa Dola 40,000, ambazo ni zaidi ya Sh100 milioni.

Kwa hiyo endapo Bangala atapata timu nyingine katika dirisha hili dogo na ikamlipa hela ya kusainia mkataba, maana yake atakuwa milionea kweli kweli.


KWA NINI AMEACHWA?

Kuna taarifa za ndani, aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Youssouf Dabo, aliyetemwa kumpisha Rachid Taoussi alikuwa haridhishwi na Yeison Fuentes, kutokana na kukosa kasi.

Mtu wa ndani kutoka benchi la ufundi la Azam ameongea na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina, anasema tofauti na ilivyokuwa kwa Dabo, kwa kocha Taoussi anamkubali sana Yeison Fuentes kwa maarifa yake ya ulinzi na nidhamu ya nafasi, lakini tatizo lake ni kasi.

Anataka apate beki mwenye kasi zaidi yake na hata Yoro Diaby, ili awe na wigo mpana.

Kwa hiyo muathirika wa hili akawa Bangala ambaye kwa umri wake, inaonekana hana cha kuongeza zaidi.

Hata hivyo, haijajulikana kama beki huyo mwenye kasi atatoka ndani au nje ya nchi na kama atakuja sasa au dirisha kubwa.

Hii ni kwa sababu nafasi ya usajili kwa wachezaji wa kigeni iliyoachwa na Bangala, tayari imechukuliwa na Alassane Diao, ambaye aliondolewa kwenye usajili kwa sababu ya maumivu.

Siku anatambulishwa katika usajili, mkuu wa habari na mawasiliano wa klabu hiyo, Zaka Zakazi, akiongea na redio moja hapa nchini alisema Diao kaja kivingine kama Kombora la Urusi la Oreshnik.

Kweli, mechi yake ya kwanza dhidi ya Fountain Gate, akitokea benchi akafunga bao la pili la klabu yake.

Kwa hiyo endapo Azam itataka kuongeza beki kutoka nje ya nchi basi itabidi mchezaji mwingine tena wa kigeni aondoke au wasubiri hadi dirisha kubwa kuangalia nafasi nyingine.


BANGALA NA AZAM

Azam ilimnunua Bangala kutoka Yanga kwa dau la Sh50 milioni.

Hii ilikuwa biashara ya kushangaza ikizingatiwa klabu hizi mbili zilitoka kwenye mgogoro mkubwa wa uhamisho wa Feisal Salum 'Fei Toto'.

Hata hivyo, haikuwa vigumu kwa Yanga kumuuza Bangala kwa Azam kwani hakuwa kwenye mipango yao na walishapanga kumuacha.

Kwa hiyo kama sio Azam kuja, maana yake ingewalazimu kumvunjia mkataba na kumlipa pesa nyingi, kwa hiyo ujio wa Azam ukawa wa faida kwao.

Alikuwa mhimili mkuu katika safu ya ulinzi ya Azam chini ya kocha Youssouf Dabo katika nusu ya pili ya msimu wa 2023/24 akitengeneza pacha ya ulinzi na ingizo la dirisha dogo, Yeison Fuentes, kutoka Colombia.

Hata hivyo, chini ya Rachid Taoussi, MVP huyo wa msimu wa 2021/22, hakuwa na nafasi mbele ya Mamadou Diaby kutoka Mali.

Tangu Dabo aondoke mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, Bangala ameanza kwenye mechi mbili tu; moja ya ligi kuu, dhidi ya Dodoma Jiji, ambayo alijifunga na nyingine dhidi ya Kombe la CRDB dhidi ya Iringa Sports Club.


ALIANZIA DODOMA, KAMALIZIA DODOMA

Oktoba 3, 2023, Azam FC ilicheza na Dodoma Jiji kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Mechi hii iliyoisha kwa suluhu ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yannick Bangala kuanza katika kikosi cha kwanza.

Alianza katika nafasi ya kiungo akiwa na Sospeter Bajana, lakini hata hivyo hakuimaliza baada ya kuumia na kutoka kipindi cha kwanza tu.

Akajiuguza majeraha yake na kupona kisha kurudi mzigoni, safari hii kama beki wa kati na kushikilia namba hadi mwisho wa msimu.

Hata msimu mpya ulipoanza aliendelea kuwa katika kikosi cha kwanza hadi alipoumia katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya JKT Tanzania na baadaye benchi la ufundi la Azam FC kubadilika.

Kocha mpya Rachid Taoussi, alipokuja akaanza na wachezaji wazima wakati Bangala akijiuguza.

Katika nafasi yake alikuwepo Yoro Diaby, akaenda naye.

Bangala kuja kupona akakuta tayari Diaby ameushikilia nafasi yake, hivyo Bangala kulazimika kusubiri benchi.

Aliendelea kusubiri benchi hadi Desemba Mosi mwaka huu alipoanza dhidi ya Dodoma Jiji, ambao ndiyo mchezo wake wa mwisho wa ligi kuu kabla ya kuvunjiwa mkataba.

Kwa hiyo mechi ya kwanza kuanza ya ligi kuanza ilikuwa dhidi ya Dodoma jiji mjini Dodoma na mechi yake mwisho ya ligi kuanza imekuwa dhidi ya Dodoma Jiji hapo hapo Dodoma.

Kwa heri Yannick Litombo Bangala, mzee wa kazi chafu!