Novatus apiga mbili Uturuki chama lake likishinda 3-0

Muktasari:
- Novatus alijiunga na Goztepe Julai 23, 2024 akitokea Shakhtar Donetsk ya Ukraine ambapo tayari amecheza mechi tisa za ligi na kufunga mabao mawili.
Kiungo Mtanzania anayekipiga Goztepe inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki, Novatus Dismas Miroshi, jana aliisaidia timu yake kupata pointi tatu baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Rizespor.
Mchezo huo wa Ligi Kuu ya Uturuki ulipigwa kwenye Uwanja wa Gürsel Aksel ambapo Goztepe ilikuwa nyumbani.
Novatus mwenye uwezo pia wa kucheza beki wa kati na pembeni, alifunga bao la kwanza dakika ya 25 akiunganisha kwa kichwa kona iliyopigwa na David Tijanic ambaye naye alifunga bao la pili dakika ya 71.
Dakika ya 78, Novatus alifunga bao la tatu kwa timu yake huku kwake likiwa la pili akitumia tena kichwa kwa pigo la faulo kutoka kwa David Tijanic.
Ushindi huo umeifanya Goztepe kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uturuki ikifikisha pointi 28 nyuma ya vinara Galatasaray yenye 44 huku nafasi ya pili ikishikwa na Fenerbahce (36) wakati Samsunspor (3) ni ya tatu. Timu zote hizo zimecheza mechi 16.
Novatus alijiunga na Goztepe Julai 23, 2024 akitokea Shakhtar Donetsk ya Ukraine ambapo tayari amecheza mechi tisa za ligi na kufunga mabao mawili.
Mchezo unaofuata Gotsepe itakuwa ugenini dhidi ya vinara wa ligi, Galatasaray utakaochezwa Januari 5, 2025 kwenye Uwanja Rams Park.