Gundogan arejea Man City, apewa jezi ya Alvarez
Muktasari:
- Gundogan, 33, amesaini mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa hao wa Ligi Kuu England.
Manchester, England. Habari ndo hiyo. Manchester City imetangaza rasmi kwamba imemsajili tena kiungo Ilkay Gundogan na kumrudisha kwenye kikosi chao ikiwa umepita msimu mmoja tu tangu alipokwenda kujiunga na Barcelona.
Gundogan, 33, amesaini mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa hao wa Ligi Kuu England.
Mkataba huo wa Etihad una kipengele cha kumwongezea mwaka mmoja zaidi wa kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kama atacheza kwa kiwango bora msimu huu.
Akizungumzia ishu ya kurudi Man City, kiungo huyo Mjerumani alisema: "Miaka yangu saba niliyokuwa Manchester City kilikuwa kipindi bora zaidi kwangu ndani na nje ya uwanja. Nilipevuka hapa kama mchezaji na mwanadamu, nilitengeneza uhusiano mzuri na mashabiki na kupata mafanikio. Kilikuwa kipindi cha kipekee sana katika maisha yangu.
"Kuna nafasi ya kurudi hapa hilo limekuwa na maana kubwa sana kwangu. Kila mtu anafahamu namna ninavyomheshimu Pep – yeye ni kocha bora kabisa duniani na kufanya naye kazi kulinifanya niwe mchezaji bora. Kuwa chini yake unajiona upo kwenye changamoto muda wote na hilo ni jambo ambalo kila mwanasoka wa kulipwa anapenda kukabiliana nalo. Nasubiri kwa hamu kufanya naye tena kazi.
"Na ninachoweza kusema kuhusu wachezaji wenzangu hapa Man City… wao ni wachezaji wa kiwango cha dunia. Nimefurahi kupata nafasi ya kufanya mazoezi na kucheza nao tena. Ukweli nasubiri kwa hamu kubwa kuvaa tena uzi wa Man City kwa ajili ya mechi."
Gundogan amejiunga na Man City kwa uhamisho wa bure akitokea Barcelona ikiwa ni miezi 14 imepita tangu alipoachana na miamba hiyo ya Etihad ambapo amepewa jezi namba 19 iliyokuwa ikivaliwa na Julian Alvarez alijiunga na Atletico Madrid.
Katika ujumbe wake aliowapa mashabiki wa Barcelona, Gundogan alisema: "Wapenzi mashabiki, baada ya mwaka mmoja wa kuwa pamoja ni wakati wa kusema kwaherini. Nilikuja hapa kukabiliana na changamoto mpya na nilikuwa tayari kwa hilo. Nilijitolea kila kitu kwa ajili ya kuipigania klabu katika msimu mgumu na nilikuwa tayari kuwasaidia wachezaji wenzangu kwa ajili ya msimu mpya.
"Sasa naondoka katika hali ngumu sana, lakini kuondoka kwangu kunaisaidia klabu kiuchumi, hivyo inanifanya nisiwe na huzuni sana. Zaidi kilikuwa ni kipindi cha kupanda na kushuka, siku zote nilihitaji sana kuichezea Barcelona na nimefurahi kupata fursa hiyo. Nawatakia kila la heri kwa msimu mpya na hapo baadaye. Mashabiki wanastahili kupata kilichobora kwa timu yao kurudi kwenye ubora. Kwaherini Barca!"
Kabla ya Gundogan kuthibitisha rasmi kurudi Man City, kiungo wa zamani wa Manchester United, Paul Scholes aliitaka timu yake kufanya haraka kwenda kumsajili Mjerumani huyo badala ya Manuel Ugarte.
Man United ipo kwenye mchakamchaka wa kumnasa Ugarte kutoka Paris Saint-Germain na imekuwa ikimfukuzia tangu dirisha lilipofunguliwa, lakini tatizo kubwa lipo kwenye ada ya uhamisho, bado hawajafikia makubaliano.
Na badala yake baada ya Scholes kutambua kwamba Gundogan ameruhusiwa kuondoka Barcelona, alitaka mabosi wa Man United kufanya haraka kwenda kumsajili, lakini mkali huyo alikubali kujiunga na Man City baada ya kukutana na kocha wake wa zamani Guardiola na kupata mlo pamoja.
Scholes alisema: "Gundogan. Najua ni jambo gumu kutokea, lakini ni aina ya wachezaji ambao Man United inawahitaji. Zubimendi… au nitasema Gundogan. Mchezaji anayeweza kutawala kiungo na kuonyesha makali yake kwenye mchezo. Gundogan angefiti vyema kabisa."
Scholes aliongeza: "Sikumwangalia sana Ugarte, nilimwona mara chache sana mwaka jana. Sina uhakika kama kiufundi ana uwezo mkubwa. Anaonekana ni kama Amrabat. Labda anaweza kuwa mzuri kiasi."
Gundogan aliitumikia Man City kwa miaka saba na kucheza mechi 304. Alikuwa nahodha wa kikosi hicho cha Etihad kwa msimu wa 2022-23 kilipoweka rekodi ya kunyakua mataji matatu makubwa ya msimu, Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA.
Kwa ujumla, kiungo huyo ameshinda mataji matano ya Ligi Kuu England akiwa na Man City, Kombe la FA mara mbili, Kombe la Ligi mara nne na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja katika maisha yake kwenye kikosi hicho cha Etihad chini ya kocha Guardiola.