Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ManCity yaisambaratisha Liverpool kwa staili

Manchester, England. Manchester City imezidi kuweka presha kwa Arsenal kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL) baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 katika mchezo baina yao jana kwenye Uwanja wa Etihad.

Ushindi huo ulioifanya Manchester City kufikisha pointi 64 na kuendelea kukaa katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, haukuwa jambo la kushangaza kuliko kiwango bora kilichoonyeshwa na vijana hao wa Pep Guardiola katika mchezo huo kuanzia dakika ya kwanza hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa na mwamuzi Simon Hooper.

Wenyeji walionekana kutawala katika kila takwimu muhimu za mchezo huo hasa zile za kushambulia na hapana shaka idadi hiyo ya mabao manne ilikuwa malipo sahihi kwa kazi nzuri iliyofanywa na nyota wa Manchester City katika dakika zote 90 za mechi hiyo.

City waliongoza katika umiliki wa mpira wakifanya hivyo wa 68%, wakiwa vinara katika upigaji wa pasi sahihi ambazo zilikuwa 687 huku wageni wao wakiwa nazo 276 tu, wakitamba pia kwa kupiga mashuti mengi yaliyolenga lango ambapo walifanya hivyo mara nane huku Liverpool wakipiga shuti moja tu lakini kana kwamba haitoshi, walifanya jumla ya mashambulizi 73 ya hatari kuelekea langoni mwa wapinzani wao ambao walifanya mashambulizi 27 tu katika mechi nzima.

Na haikushangaza kuona mabingwa hao watetezi wa EPL wakiibuka na ushindi huo mnono licha ya kutanguliwa kwa bao la dakika ya 17 la Mohamed Salah aliyeunganisha pasi ya Diogo Jota, shukrani kwa mabao ya Julian Alvarez, Kevin De Bruyne, Ilkay Gundogan na Jack Grealish.

Dakika 10 tu baada ya Salah kuipatia Liverpool bao la kuongoza, Alvarez aliisawazishia Man City kwa kumalizia vyema krosi ya Grealish kutokea upande wa kushoto na kufanya mechi hiyo kwenda mapumziko ikiwa na matokeo hayo ya sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili kilianza mapema kuwa kigumu kwa Liverpool baada ya De Bruyne kuipatia Manchester City bao la pili dakika moja tu baada ya filimbi ya mapumziko akimalizia pasi ya Mahrez. Pasi hiyo ya bao kwa Kevin De Bruyne ilimfanya Ryad Mahrez kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa Kiafrika aliyepiga pasi nyingi za mwisho katika Ligi Kuu ya England akifanya hivyo mara 55.

Awali Mahrez alikuwa sawa na Mohamed Salah wakishikilia kwa pamoja rekodi hiyo ambapo kila mmoja alikuwa amepiga pasi za mabao 54.

Man City haikuwapa Liverpool nafasi ya kujipanga baada ya bao hilo kwani dakika saba baadaye Gundogan aliwapatia la tatu akimalizia mpira uliookolewa na Trent Alexander-Arnold baada ya shuti la Alvarez.

Grealish aliyeonyesha kiwango cha juu katika mchezo huo, alipigilia msumali wa mwisho katika jeneza la Liverpool katika dakika ya 74 akimalizia pasi ya De Bruyne, na kuihakikishia timu yake ushindi ambao umezidi kufifisha matumaini ya Liverpool kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa EPL ikibakia na pointi zake 42.