FIFA yaiandama Argentina kwa ujumbe wa kisiasa baada ya kuiondoa England
Muktasari:
- Argentina inakabiliwa na faini kutoka FIFA baada ya wachezaji wake kuonyesha bango la kudai Visiwa vya Falklands kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya England, huku Lionel Messi akiongoza ushindi huo kwa kutoa pasi mbili za mabao zilizoifikisha timu yake fainali.
Timu ya Taifa ya Argentina huenda ikakabiliwa na faini kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) baada ya wachezaji wake kuonyesha bango lenye ujumbe wa kisiasa mara baada ya kuiondoa England kwa ushindi wa mabao 2-1 katika nusu fainali ya Kombe la Dunia iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz, Atlanta, Marekani.
Baada ya filimbi ya mwisho, wachezaji wa Argentina walikusanyika katikati ya uwanja wakiwa na bango lililoandikwa "Las Malvinas son Argentinas", yaani "Visiwa vya Falklands ni vya Argentina." Hatua hiyo imeibua mjadala mkubwa kutokana na mgogoro wa muda mrefu wa umiliki wa visiwa hivyo kati ya Argentina na Uingereza.
Miongoni mwa wachezaji walioonekana wakilishika bango hilo ni nahodha wa Tottenham Hotspur, Cristian Romero, kiungo Giovani Lo Celso pamoja na beki wa Manchester United, Lisandro Martinez.
Aidha, kiungo Leandro Paredes alisema katika mahojiano baada ya mchezo kuwa, "Falklands zitabaki kuwa za Argentina milele."
FIFA inaweza kuchukua hatua
FIFA imekuwa ikipiga marufuku mabango na bendera zenye ujumbe wa kisiasa ndani ya viwanja vya mashindano yake, ikiwamo zile zinazohusu mgogoro wa Visiwa vya Falklands.
Mwaka 2014, Argentina ilitozwa faini ya pauni 20,000 baada ya wachezaji wake kubeba bango lenye ujumbe huohuo kabla ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Slovenia.
Chanzo cha mgogoro
Visiwa vya Falklands, vinavyojulikana nchini Argentina kama Las Malvinas, ni eneo la ng'ambo la Uingereza lililopo katika Bahari ya Atlantiki Kusini, takribani maili 300 kutoka pwani ya mashariki ya Argentina.
Argentina imekuwa ikidai umiliki wa visiwa hivyo kwa muda mrefu, hali iliyosababisha vita kati ya nchi hizo mbili mwaka 1982 baada ya majeshi ya Argentina kuvamia na kuteka visiwa hivyo.
Vita hivyo vilidumu kwa siku 74 kabla ya Uingereza kurejesha udhibiti wa visiwa hivyo.
Kauli za viongozi wa Argentina zazidisha mvutano
Kabla na baada ya mchezo huo, viongozi waandamizi wa Argentina walitoa kauli zilizoongeza mvutano kati ya mataifa hayo mawili.
Makamu wa Rais wa Argentina, Victoria Villarruel, aliandika katika mtandao wa X kuwa pambano dhidi ya England "halikuwa mechi nyingine tu."
Akiambatanisha video iliyoonekana kuwa ya wanajeshi wa Argentina, alisema, “visiwa vya Malvinas ni vya Argentina. Walikataza kuingiza mabango uwanjani, lakini wamesahau kuwa tunavibeba ndani ya damu na mioyo yetu."
Katika ujumbe mwingine kabla ya mchezo huo, Villarruel aliwaita Waingereza "maharamia wanyang'anyi" akisema, “kesho tunacheza dhidi ya maharamia walioteka ardhi yetu. Huu si mchezo wa kawaida. Siwezi kuwa wa kisiasa wala mwenye hisia za baridi; dhidi ya Waingereza siku zote kuna jambo kubwa zaidi."
Rais wa Argentina, Javier Milei, naye alisisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kudai umiliki wa visiwa hivyo.
"Tunafanya kila linalowezekana kibinadamu kurejesha Visiwa vya Falklands mikononi mwa Argentina. Suala la mamlaka ya visiwa hivyo haliwezi kujadiliwa, lakini lazima lifanywe kwa busara na kwa akili,” alisema Milei.
Imendikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao