Amorim aibua sintofahamu Man United
Muktasari:
- United wanakabiliwa na ratiba ngumu zaidi ambapo itavaana na Burnley, Manchester City kisha kukabiliana na vinara wa ligi, Arsenal.
Manchester, England. Kocha mkuu wa Manchester United, Ruben Amorim, ameashiria kuwepo kwa sintofahamu kati yake na uongozi wa klabu hiyo baada ya kutoa majibu mafupi na yenye tahadhari kali alipoulizwa kuhusu mipango ya usajili wa wachezaji katika dirisha la Januari.
Iwapo kulikuwa na mashaka kuwa kauli zake za awali zilipotoshwa, basi Amorim alizima kabisa utata huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Leeds United Jumapili mchana.
Kocha huyo raia wa Ureno alionekana mwenye hali ya kukunja uso, akidokeza kutoridhika kwake na mwelekeo wa klabu, hasa katika mawasiliano yake na mkurugenzi wa michezo Jason Wilcox.
Amorim amekiri wazi kuwa hatarii kusajili mchezaji yeyote mpya mwezi huu na wala hana mazungumzo yoyote na uongozi kuhusu hilo.
Ingawa United hawajafunga kabisa milango ya kusajili wachezaji, klabu hiyo imesisitiza kuwa haitafanya usajili wa pupa Januari, bali italenga kuharakisha mipango ya usajili iliyopangwa majira ya joto.
Kwa sasa, United wanaendelea kuchunguza uwezekano wa kuimarisha kiungo cha ulinzi, huku wakiwahi kuonyesha nia ya kumsajili Antoine Semenyo kwa dau la pauni milioni 65. Hata hivyo, kuna dalili kuwa watampoteza mshambuliaji huyo wa Bournemouth baada ya kukimbilia kwa wapinzani wao Manchester City.
Awali Amorim alionekana kuunga mkono sera hiyo ya tahadhari, lakini hali ilibadilika ghafla alipoulizwa maswali zaidi kuhusu dirisha la usajili, akitoa majibu mafupi na ya kujikinga.
Baada ya kusema mapema kuwa “hatuna mazungumzo yoyote kwa sasa ya kubadili kikosi”, kocha huyo aliombwa kufafanua kauli yake ya awali kwamba kubadili mfumo kwenda 4-3-3 kungehitaji pesa nyingi, jambo ambalo aliamini halitotokea.
“Sitaki kuzungumzia hilo. Nimejikita tu kwenye mchezo dhidi ya Leeds,” amesema kwa kifupi.
Alipoulizwa kama anajutia kauli hiyo, amejibu:
“Hapana. Sitaki kuzungumzia hilo.”
Je, kulikuwa na mabadiliko katika bajeti ya usajili au Wilcox alikujulisha jambo lolote?
“Sitaki kuzungumzia hilo. Lakini wewe ni mwerevu,” amesema Amorim kwa tabasamu la uficho.
Baadaye aliulizwa iwapo United watalazimika kusajili mchezaji endapo mmoja ataondoka Januari.
“Ukikiangalia kikosi chetu, naona ni vigumu mtu kuondoka lakini hilo wanapaswa kuzungumza na Jason,” amesema.
Ni mara ya kwanza ndani ya miezi 14 ya Amorim Old Trafford kuonekana na dalili za mgawanyiko kati yake na bodi ya klabu. Ingawa hali hiyo haijafikia kiwango cha mgogoro wa Enzo Maresca na Chelsea, bado inazua maswali.
Chanzo chake kinaweza kuwa ni matumaini ya Amorim kuona fedha zilizotengwa kwa Semenyo zikitumika kuimarisha maeneo mengine ya timu, hususani kiungo cha kati, ambacho kimekuwa tatizo kubwa.
Matokeo ya hivi karibuni kipigo dhidi ya Aston Villa, ushindi mwembamba dhidi ya Newcastle na sare ya dhidi ya Wolves yameonyesha wazi ukosefu wa ubunifu, hali iliyochangiwa na majeruhi pamoja na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
United wamewakosa Bruno Fernandes, Bryan Mbeumo na Amad Diallo, ambao Amorim amesema ndio chanzo kikubwa cha ubunifu wa timu.
“Inaweza ionekane kama kisingizio, lakini tulipata mkosi kuwakosa Amad, Bryan na Bruno kwa wakati mmoja,” amesema Amorim.
“Wao ndio wanaunda nafasi nyingi. Ukiwakosa wote kwa pamoja, timu yoyote duniani itapata shida.”
Aliendelea:
“Nani anapiga mipira ya adhabu? Amad, Bryan na Bruno. Ukipoteza wote kwa wakati mmoja, kila kitu kinaathirika.”
Hali ya mambo ilizidi kuwa mbaya baada ya mashabiki wa United kuonyesha kutoridhika kwao kwa kuzomea timu baada ya sare dhidi ya Wolves, pamoja na uamuzi wa Amorim kumtoa Ayden Heaven na kumuingiza beki mwingine, Leny Yoro.
“Naelewa timu kuliko mtu yeyote,” amesema.
“Wakati mwingine mashabiki watakubaliana na maamuzi yako, wakati mwingine hapana. Mimi nafanya ninachoona ni sahihi kulinda timu na kushinda mechi.”
Amorim sasa anahitaji ushindi dhidi ya Leeds ili kutuliza presha inayoongezeka uwanjani na nje ya uwanja. Baada ya hapo, United wanakabiliwa na ratiba ngumu zaidi ambapo itavaana na Burnley, Manchester City kisha kukabiliana na vinara wa ligi, Arsenal.