Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajumbe CCM tupeni raha, tuondoleeni makada hawa

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza ratiba ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa nafasi ya ubunge lakini natamani wajumbe wanoe vichinjio vyao vizuri ili watusaidie kutuondolea makada wa aina tatu waliotia nia ubunge 2025.

Ninafahamu mchakato huo utakaoanza Juni 28, 2025 utahusisha pia uchukuaji fomu za ujumbe wa Baraza la wawakilishi na madiwani, lakini tunatamani wajumbe wacheke nao vizuri lakini wakitoka ukumbini waseme wajumbe si watu.

Kuna makundi matatu ya makada ambao natamani wajumbe wasiwachekee hata kidogo, kundi la kwanza ni lile linalotumia jina la Rais na viongozi wengi, la pili ni linalotumia udini kutafuta huruma na kundi la tatu ni wanaogawa rushwa.

Kuhusu kundi la kwanza linalotumia majina ya viongozi, hakuna ubishi kuwa makada hao wamejimwambafai sana majimboni kuwa ama wametumwa na Rais Samia, au Waziri mkuu Kassim Majaliwa ama viongozi wa juu wa CCM.

Kuna jimbo moja, mmoja wa makada hao amehifadhi namba kimagumashi kuwa ni ya Rais Samia na anamwambia mwenye namba hiyo ampigie simu, kisha anawaambia baadhi ya wajumbe aliokuwa nao “mnaona? Si nimewaambia?”

Makada wa aina hiyo wapo wengi na wengine ni wanaoshikilia nyadhifa za kuteuliwa na Rais na wanajimwambafai kuwa Rais ndio kamtuma hivyo anamhitaji kwani anataka kumpa nafasi fulani ndani ya baraza la mawaziri lijalo.

Wengine hawaishii kuwaonyesha simu za aina hiyo makatibu wa CCM wa kata au wajumbe wa vikao vya kura za maoni, lakini wanaenda mbali hata kuwaeleza hayo baadhi ya wajumbe wa kamati za siasa za wilaya na mikoa ili kuwavuta kwake.

Bahati nzuri mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amezirahisishia kazi kamati za siasa za wilaya na mikoa kuwa sisi yeye wala Rais wa Zanzibar, Dk Husein Mwinyi wametuma watu huko majimboni ili wakagombee ubunge.

Nikinukuu kile alichokisema, Rais Samia alisema kuna wanaokwenda kwenye majimbo na kusema “nimetumwa nije”, lakini kwa upande mwingine, kuna mtu akienda kwenye jimbo analotaka kugombea, walioko wanasema katumwa aje. “Nataka niwaambie, si mimi, si Rais wa Zanzibar. Hatutatuma watu kuja majimboni. Sisi tuna nafasi zetu kumi kumi, kwa hiyo tukimaliza uchaguzi wale tunaowataka tuna nafasi kumi,”alisema Rais Samia Mei 30,2025 Jijini Dodoma.

“Kwa hiyo mlioko kwenye majimbo mjizatiti na majimbo yenu msifanye woga. Mkiona watu wanasema wametumwa, au wanaojileta na kusema wametumwa na hao wakateni mapema sana. Hatujatuma watu,” alisisitiza Rais Samia.

Ni kupitia mkutano huo mkuu maalum, Rais aliziagiza Kamati za Siasa na mikoa za CCM kutenda haki, anayefaa aambiwe anafaa, asiyefaa aambiwe ana kasoro moja, mbili tatu, nami namuunga mkono mwenyekiti wangu, wasiofaa wachinjwe.

Mgombea anayetumia jina la Rais au la kiongozi mwingine yeyote bila ruhusa yake anatafsiriwa kama kiongozi mlaghai, asiye mwaminifu na mtu wa aina hiyo inaonyesha dhahiri anataka kwenda bungeni kwa maslahi binafsi sio ya umma.

Kwa hiyo kamati za uteuzi na wajumbe wa mikutano ya kura za maoni, noeni vizuri vichinjio vyenu kwani tayari mwenyekiti ameshawapa rungu, hakikisheni mnawapa kinachostahili ili wakome kutumia jina la rais kulaghai wananchi.

Kundi la pili ambalo natamani wajumbe mtupe raha ni kuwanyima kura wale wote wanaotumia udini kutafuta ushawishi katika nyumba za ibada kwamba ooh safari hii ni zamu ya Mkristo au muislamu, kinyume kabisa na Katiba na Sheria za nchi.

Ukisoma Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Tanzania, inazuia kusajiliwa kwa chama chochote cha siasa kinachokusudia kukuza au kupigania maslahi ya imani au kundi lolote la dini, kinachohamasisha ukabila au ubaguzi wa rangi na jinsia ya mtu.

Kwa hiyo, ni wajibu wa wajumbe kutumia kichinjio chao kuwafyeka makada wa CCM ambao tunafahamu baadhi yao wamepita pita kwenye misikiti kuungwa mkono, au hata makanisani na kusema safari hii ni zamu ya mkristo.

Baba wa Taifa, hayati Jullius Nyerere aliwahi kusema kuwa inapotokea kipindi cha uchaguzi (kama tulichonacho) hujitokeza watu ambao wakishindwa kupata ushawishi kwa kutumia sifa bora, hoja na sera hukimbilia kwenye udini. Kutafuta uongozi kwa kutumia dini unagawa watu, kazi ya uongozi ni kuleta umoja, hili lizingatiwe.



na baba wa taifa akasema tukiwakubalia viongozi wa aina hiyo tutagawanyika, na mimi niwasihi wajumbe, kichinjio cha watu wa aina hii mnacho

Mtu anayetumia huruma ya udini kupata ubunge au udiwani hatufai, kwamba anazunguka huko kwenye mashina, matawi na kata na kutafuta wajumbe ambao wanatokana na dini yake ili wampe kura, huyo ni mtu hatari sana kwa Tanzania.

Ukisoma Kanuni ya 25(2) ya Kanuni za Uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya Dola imesema wazi kabisa kuwa ni mwiko kabisa mgombea kutumia au kuhusisha ukabila, udini na rushwa katika shughuli yoyote ya uchaguzi.

Sasa tutawashangaa sana wajumbe mkituletea wagombea wenye vimelea vya udini kwa sababu hiyo peke yake inakwenda kuwagawa wananchi kiimani, na badala yake, mtu achaguliwe kwa sifa zile zilizomo katika Kanuni ya 5(i) hadi (vii).

Kundi la mwisho ambalo wajumbe tunawaomba sana mtuchinjie mapema ni wale walioanza kampeni mapema, wakigawa fedha na zawadi mbalimbali kwa baadhi ya wajumbe wa mikutano ya kura za maoni na wajumbe wa kamati za siasa.

Kada wa CCM anayetafuta uongozi kwa rushwa anaenda kufanya biashara gani ya ubunge hadi atumie hadi Sh500 milioni kugawa fedha na zawadi mbalimbali? Wajumbe chondechonde msikubali kuuza utu wenu kwa vipande vya fedha.

Msikubali kutumika kama karai la zege kwamba baada ya ujenzi, karai huwekwa nyuma ya nyumba kusubiri msimu mwingine wa ujenzi au ‘toilet paper (karatasi za chooni), ambazo hutumika kumsafisha mtu na zenyewe kubaki na uchafu.

Tunafahamu wako makada ambao wamejiweka karibu sana na Jamii katika kipindi hiki, kwenye misiba yumo na akifanya juu chini atajwe na mshereheshaji (MC) kuwa yupo katika shughuli hiyo, pamoja na mahafali na sherehe nyingine.

Lakini ukifungua moyo wake kumbe ameamua kujishusha tu lakini ana kitu anachokilenga na anaweza ku-pretend (kujifanya) hata kwa miaka miwili au mitatu ili jamii imuone ni mtu mwema lakini ukweli kuna kitu anakitafuta.

Tunahitaji mbunge ambaye ataitumia vyema Ibara ile ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake, na sio anayekwenda pale kwa maslahi yake binafsi au kwa lengo la kurejesha fedha.

Mathalan, amefanya nini kuhakikisha anatumia jukwaa la Bunge kuisimamia na kuishauri Serikali katika masuala mazima ya utekaji, kupotea na mauaji ya watu yaliyoshamiri kuanzia 2016 na Bunge halijaonyesha makali yoyote katika hili.

Hatupeleki mbunge ambaye anakwenda kuunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au ambaye atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake.

Leo nayazungumza haya kwa CCM kwa sababu ndio chama kiongozi, lakini natamani haya mambo yatumike pia katika kuwapata wagombea ubunge na udiwani kupitia vyama vingine vya upinzani vinavyoshiriki uchaguzi mkuu.

Kwa hiyo wajumbe na kamati za uchujaji, msiangalie sura ya mgombea, ukwasi alionao, kujuana, dini aliyonayo au kabila analotoka bali chagueni wale tu wenye sifa kama alivyosema Rais Samia, wasio na sifa tupa nje bila kumuonea haya.