Prime
Nataka ‘niamini’ kuna kada CCM atamwachia mpinzani Jimbo

Nataka niamini, na naumiza kichwa sana kuuaminisha ubongo wangu kuwa kuna wagombea fulani fulani wa vyama vya upinzani, kwamba makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), watawapa bure majimbo hayo hata kama hawajashinda.
Haisemwi rasmi bali inasemwa kama minong’ono kuwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025, yapo majimbo ambayo Serikali ya CCM itayatenga kwa ajili ya wagombea wa upinzani, ili kuonesha dunia kuwa kuna Demokrasia.
Ni kweli zipo nchi Afrika zinaweza kutengeneza maigizo ya aina hiyo, ila sio Tanzania. Ninachoamini haitakaa itokee CCM imekubaliwa na wananchi halafu ikawaambia tunawapa huyu wa upinzani ndio awe Mbunge au Diwani wenu.
Kwa uzoefu wangu, kinachoweza kutokea ni kwamba mgombea wa upinzani ameshinda kihalali kabisa, CCM wakakubali atangazwe kwa kuwa hakuna namna, kwa hiyo hao wanaojidanganya watapata ushindi wa mbeleko, sio CCM hii.
Kwamba dhana hii ndio ambayo imechochea vuguvugu la baadhi ya waliokuwa watia nia nafasi za ubunge na udiwani 2020 na waliokuwa wamejipanga kuwania nafasi hizo uchaguzi mkuu 2025, kupitia Chadema kuhamama chama hicho.
Nataka niamini kwamba CCM kimegeuka malaika na kuachana na matendo yote yaliyotokea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na 2024 na uchaguzi mkuu 2020, na kwamba sasa itatoa majimbo na kata bwerere kwa baadhi ya wapinzani.
Kwamba CCM hii ambayo ilizoa majimbo 262 kati ya 264 uchaguzi mkuu 2020 na CCM hii hii iliyoshinda vijiji 12,271 kati na nafasi 12,280 na kushinda nafasi 63,843 za vitongoji kati ya 63,886 uchaguzi 2024, iko tayari kugawana nafasi na upinzani.
Halafu mwanasiasa mahiri kabisa, unakubalije kuingia kwenye mkenge huu bila kujitafakari na kutambua kuwa vya bure vina gharama?, halafu ni lini CCM imejitokeza hadharani ikasema safari itagawa viti bure kwa upinzani?Lini?.
Kwamba purukushani zote hizi zinazoendelea katika majimbo mbalimbali ya Tanzania Bara kwa makada wa CCM kujipitisha, kutia nia na wengine hata kugawa rushwa, ili waongoze kura za maoni, kwamba watakubali kuachia majimbo.
Mnawafahamu wajumbe nyie?, Yaani kada wa CCM amefurukuta kuanzia sasa hadi anaongoza kura za maoni, amekwepa mishale kadhaa wa kadhaa halafu eti kuna makada wa upinzani wanajiaminisha watagawiwa tu bure majimbo yao.
Ukisoma Katiba ya CCM ya mwaka 1977 ibara ya 5 kuhusu madhumuni ya kuanzishwa kwake inasema ni pamoja na kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ili kuunda na kushika Dola, upinzani mnapewaje viti vya bure?
Mathalani, kwamba eti huko nje kuna mtiti wa wananchi na wanataka mgombea aliyeshinda ndiye atangazwe mshindi, bila kujali ni CCM, ACT-Wazalendo, CUF au NCCR-Mageuzi, halafu msimamizi anamtangaza mgombea wa Chaumma.
Kama ingekuwa ni hivyo kama radio mbao zinavyoeleza, basi kutakuwa hakuna haja ya kuwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo majukumu yake yanapatikana katika kifungu cha 10 cha sheria ya INEC ya mwaka 2024.
Kinachotakiwa katika nchi yetu si kikundi fulani au chama fulani kiwe na nguvu ya kuishawishi INEC imtangaze mshindi hata kama hajashinda, bali tuwe na mifumo ya kisheria inayotoa hakikisho la uchaguzi huru, wa haki na unaominika.
Mifumo yetu isiruhusu wagombea kuenguliwa eti kwa sababu tu msimamizi anaandika “hajui kusoma na kuandika”, bali mgombea aenguliwe kwa sababu za msingi kama vile sio raia wa Tanzania, ni mgonjwa wa akili au amegushi elimu.
Mifumo hiyo isibague, ni lazima sheria iwe ni msumeno ikate mbele na nyuma, kwamba uenguaji usiwe kwa upande mmoja tu wa wagombea wa upinzani, kama ni makosa ya kuandika tarehe au eneo basi aambiwe ayarekebishe kwanza.
Ukisoma Ibara ya 67 ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imeeleza ni kasoro gani mgombea akiwa nazo hatachaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge na ziko nane, kwa hiyo ni ushamba kumwengua mgombea nje ya sababu hizo.
Tunataka vyombo vyetu vya Dola kama Jeshi la Polisi wawe watizamaji na wasiwe wachezaji katika chaguzi zetu, wao watekeleze jukumu lao la ulinzi na usalama wa raia na mali zao, masuala ya uchaguzi waviachie vyama, wagombea na INEC.
Mambo ya kuenguana bila sababu za msingi na za kisheria kama zilivyo kwenye Katiba yetu ni ushamba na ndio yanasababisha tunapata viongozi ambao hawana uhalali wa kisiasa (political legitimacy) kwa vile hawakutokana na watu.
Ni lazima sheria zetu zitoe uwanja sawa katika mchakato mzima wa uchaguzi, kuanzia uandikishaji wapiga kura, uteuzi wa wagombea, kampeni za uchaguzi,upigaji kura na utangazaji wa matokeo na isiwe fadhila, hapana.
Hatutaki ule usemi wa Joseph Stalin kwamba “It’s not who votes that counts; it’s who counts the votes” kwamba ushindi haupatikani kupitia sanduku la kura, bali ushindi unapatikana kutokana na nani anayehesabu kura na kutangaza matokeo.
Katiba yetu Ibara ya 13(1) inasema wazi kuwa ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote, kuweka sharti lolote ambalo ni la ubaguzi na kwamba na inasema watu wote ni sawa mbele ya sheria na wana haki sawa.
Ukisoma Ibara ya 3 ya katiba yetu inasema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, kwa hiyo kama ndivyo, si dhambi kwa mgombea wa chama chochote cha siasa akichaguliwa na wananchi.
Lakini ukisoma Ibara ya 8(1) inasema wananchi ndio watakuwa msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi, sasa hao wanaoota kupata ushindi wa mezani tunapaswa kuwakataa.
Kwa hiyo watanzania tunapaswa kuwang’ong’a wanasiasa ambao wanahama vyama vyao eti kwa sababu tu wameahidiwa kupewa ushindi wa mezani na CCM (jambo ambalo si kweli), kila mmoja acheze mechi zake ashinde au ashindwe.
Yale mambo sita ambayo mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Tundu Lissu aliyasema yarekebishwe ili chama hicho kiweze kushiriki uchaguzi mkuu 2025 ni muhimu sana yakarekebishwa hata kama chama hicho hakishiriki uchaguzi.
Moja kusiwe na kuenguana kusikozingatia Katiba wala sheria, watoto walioandikishwa wasiruhusiwe kupiga kura, vyama vya upinzani visifanyiwe figisu kwenye kampeni na mawakala wasiwekewe urasimu na kuondolewa vituoni.
Lakini uchaguzi usiwe ndio sehemu ya kumwaga damu za watanzania maana wimbi hili la utekaji linatia hofu kama tutabaki salama kutoka sasa hadi mshindi wa kiti cha urais, washindi wa ubunge na udiwani watakapotangazwa na INEC.
Mambo ya kuteka nyara wagombea wakati wanarudisha fomu au kuwapora fomu wagombea wanaokubalika na kuteka na kutesa wananchi wanaounga mkono wagombea wa upinzani ni mambo ambayo hatutaki yajirudie uchaguzi huu.
Kwa hiyo, baadhi ya waliohama vyama kwa sababu tu wameahidiwa kupewa ushindi mezani, tuwakatae kwa sababu Tanzania haijafikia hatua ya kugawa ushindi mezani, bali madaraka ni lazima yatoke kwa wananchi na si vinginevyo.
Ndio maana nimetangulia kusema nataka ‘niamini’ kwamba kuna kada wa CCM atamwachia mpinzani atangazwe hata kama ameshinda, kwa hiyo namuomba Mungu anipe uhai niweze kushuhudia haya maajabu uchaguzi mkuu 2025.
Ila wakitendwa huko, tusisikie kelele zao, wapige kimya kwa sababu watakuwa wameyataka wenyewe na wale waliokubali kuingia katika uchaguzi huu kwa sheria za sasa za uchaguzi, nao tusiwasikie wakilia uchaguzi haukuwa huru na haki.
0656600900