Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliokuwa wabunge wapiga jaramba kurudi bungeni

Muktasari:

  • Oktoba 2025, Tanzania itafanya uchaguzi wa madiwani, wabunge na urais huku idadi kubwa ya waliokuwa wabunge 2015-2020 wakiwemo waliowahi kuwa mawaziri na naibu mawaziri wakijiweka sawa kuingia kwenye mbio za kurejea bungeni.

Dar/mikoani. Joto la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba linazidi kupanda ndani ya majimbo huku waliokuwa wabunge kwa kipindi cha mwaka 2015-2020 wakitajwa kupiga jaramba kurejea.

Kwenye kundi hilo wapo walikuwa mawaziri na naibu mawaziri wameonyesha nia ya kuingia katika uchaguzi mkuu ujao kuchuana na wenzao walioingia mwaka 2020 ambao wamebakisha siku 23 kumaliza utumishi wao.

Kinyang’anyiro kimeongeza joto hususan ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ikizingatiwa baadhi ya wagombea ni waliokuwa wakitetea nafasi hizo mwaka 2020 lakini walienguliwa na vikao vya uteuzi baada ya kushinda kura za maoni na walioshika nafasi za pili, tatu hadi nne wakaokota dodo kwenye mpera.

Baadhi ya makada kwa miaka mitano hawakuwa mbali na majimbo yao wakishiriki shughuli mbalimbali za kijamii kama misimba, sherehe na harambee kwenye nyumba za ibada kwa maana makanisani na misikitini.

Aidha, baadhi yao wamekuwa hawachezi mbali na ziara karibu zote za viongozi waandamizi wa CCM za kukagua utekelezaji wa ilani.

Ingawa wamekuwa hawapewi fursa ya kuzungumza kwenye mikutano hiyo, lakini uwepo wao ni mkakati tosha wa kuijipitisha machoni mwa viongozi na wanachama ambao hukusanyika kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo husika na inapotokea kuna michango ya kukichangia chama wamekuwa wakishiriki.

Baadhi ya wabunge hao, kwa sasa ni wakuu wa mikoa na wilaya mbalimbali nchini, suala amballo makada waliozungumza na Mwananchi wamesema linaongeza joto.

“Kuna mtiti mkubwa unakuja huu uchaguzi. Hao waliokatwa kipindi kile licha ya kuongoza kura za maoni wanarudi tena kwa nguvu. Pia kuna wale wa upinzani walikuwa na nguvu, lakini unajua uchaguzi ulivyokuwa,” alieleza kada wa CCM.

Mmoja wa vigogo waandamizi wa CCM aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutokutajwa jina anasema: “Mchuano utakuwa mkali sana mwaka huu, hii inatokana na kile kilichotokea mwaka 2020 kwenye uteuzi, wengi waliokuwa wamepita kwenye kura za maoni na kutoswa.”


Hali ilivyo majimboni

Hakuna kada hata mmoja wa CCM ambaye alikuwa yuko tayari kuthibitisha au kukanusha kuwa ataingia katika kinyang’anyiro hicho wakisema kanuni zinawabana hadi Bunge litakapovunjwa Juni 28, 2025 ndio watasema kitu.

“Tulieni. Mbona mna haraka? Haraka haraka haina Baraka naweza nikaongea hapa ndio mahasimu wangu wakapata kitu cha kupeleka maadili,” alieleza mmoja wa walioenguliwa na vikao vya CCM, ambaye anatajwa anarudi katika moja ya majimbo.

Mkoa wa Tanga ni moja ya mikoa ambayo makada wake waliathiriwa na majina kukatwa na chama kuwateua wengine walioshika nafasi kuanzia ya pili, ambao vyanzo kutoka ndani ya chama vinawataja kuwa wanataka kurejea.

Ingawa hakuna aliyekiri kuwa na mipango hiyo kwa sasa, kuwa miongoni mwa wanaotajwa ni Adadi Rajabu wa Muheza aliyeshinda kura za maoni, lakini nafasi akapewa Hamisi Mwenjuma ‘Mwana FA’.

Wengine wanaotajwa ni Mary Chatanda, mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa CCM (UWT), ambaye hata hivyo amesema hana mpango wa kugombea ubunge Korogwe Mjini kwa kuwa ameridhika na nafasi aliyonayo.

Wanatajwa pia Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba kuwa anataka kurejea Kigoma Kaskazini jimbo ambalo aliliongozwa mwaka 2015-2020 huku waziri wa zamani wa nishati na madini, William Ngeleja akidaiwa kupiga jaramba kurejea Sengerema kuvaana na Hamisi Tabasamu.

Pia, waziri wa zamani Kilimo, Dk Charles Tizeba yeye anatajwa kutaka kurejea Buchosa kwa Eric Shigongo huku mchuano mwingine unatarajiwa Shinyanga Mjini ambapo aliyewahi kuwa naibu waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele anatajwa kujipanga.

Licha ya kuongoza kura za maoni jina lake halikurejea badala yake Patrobas Katambi, naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) akateuliwa.

Duru za siasa zinamtaja pia waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kuwa anataka kujitosa tena Singida Kaskazini huku Iddi Azzan akitajwa tajwa kwenye korido za Jimbo la Kinondoni ambalo kwa sasa lipo chini ya Abbas Tarimba.

Orodha haikuishia hapo, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari naye anatajwa kutaka kurejea tena Arumeru Mashariki, Mkoa wa Arusha. Nassari alihudumu jimbo hilo akiwa Chadema lakini baadaye alihamia CCM.

Waziri mwingine wa zamani wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige yeye anatajwa tajwa kutaka kurejea tena Msalala huku aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Andrew Chenge akitatwa kutaka kutia mguu Bariadi Mjini.

Katika kura za maoni Chenge aliongoza lakini aliteuliwa Mathew Kundo ambaye vyanzo vinasema huenda akahamia jimbo jipya la Bariadi Vijijini.

Wengine wanaotajwa ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda kuwa anataka kurejea Mbinga Mjini huku Naibu waziri wa zamani wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri akitajwa kurudi Siha.

Viunga vya siasa vya Mwibara vinamtaja Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kuwa miongoni mwa wanaotaka kugombea tena huku Dk Raphael Chegeni akielezwa analimezea tena mate Jimbi la Busega.

Huko Mchinga kunaelezwa kuwa aliyekuwa mbunge 2015-2020, Hassan Bobali kupitia CUF analinyemelea tena, akitaka kuvaana na Mama Salma, mke wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Mwingine anayetajwa ni Dk Stephen Kebwe kuwa anainda tena Serengeti huku aliyekuwa Simanjiro, James Ole Millya ambaye hivi sasa ni mbunge wa Afrika Mashariki, akitajwa kuingia kwenye kinyanganyiro cha nafasi hiyo.

Ole Millya alimuangusha mbunge wa sasa Ole Sendeka mwaka 2015 na kisha naye akaangushwa na Ole Sendeka mwaka 2020.

Wengine wanaotajwa tajwa kuwa wanafaa ni aliyekuwa mbunge wa Babati Vijijini, Vrajilal Jituson kuwa huenda akavaana na mbunge anayemaliza muda wake, Daniel Sillo.

Mbali na hao wa CCM, wapo waliokuwa wabunge wa upinzani ambao nao wanapiga jaramba. Mathalani Zitto Kabwe tayari amechukua fomu Kigoma Mjini kuomba ridhaa chama chake cha ACT-Wazalendo kimpitishe awanie tena.

Zitto aliongoza jimbo hilo mwaka 2015-2020 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alishindwa na Kulumbe Ng'enda wa CCM.

Chadema ambacho mpaka sasa kinaendelea na msimamo wake wa No reforms no election, lakini walokuwa wabunge wake wanatajwa kuwa mguu sawa kwenye majimbo iwapo chama hicho kitabadili msimamo.

Waliokuwa wabunge na majimbo yao kwenye mabano ni, Frank Mwakajoka (Tunduma), Pascal Haonga (Mbozi), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (Mbeya Mjini) na John Heche (Tarime Vijijini), Joseph Haule maarufu Profesa Jay (Mikumi), Godbelss Lema (Arusha), Ezekia Wenje (Nyamagama) na Susan Kiwanga (Mulimba) ambaye ametimkia Chaumma na ameweka wazi kuwa anagombea tena.

"Jina langu linatajwa na watu wengi kule Mlimba na baadhi ya wana Mlimba wameniomba nirudi tena jimboni ili wanipe ridhaa ya kwenda kuwasemea bungeni, mimi ni nani mpaka nikatae ombi hili la wananchi,” amesema Kiwanga.

Wengine ni, Halima Mdee (Kawe), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) waliofukuzwa uanachama Chadema na hatima yao kwenye majimbo inategemea maamuzi yao baada ya Bunge kuvunjwa.


Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba na Janeth Joseph (Moshi), Joseph Lyimo (Manyara), Rajabu Athman (Tanga), Hawa Mathias (Mbeya), Hamida Shariff (Morogoro), Beldina Nyakeke (Mara) na Seif Jumanne (Njombe)