Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fumbo wabunge 19 watakavyorudi bungeni

Muktasari:

  • Awali, wabunge hao walikuwa wakiishambulia Serikali kwa kila jambo ingawa kwa sasa wamekuwa wakiisifia na kuwataja viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wanafanya kazi zilizotukuka.

Dodoma. Hatima ya kurudi bungeni kwa wabunge 19 wa viti maalumu wanaotokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wenye mgogoro na chama chao sasa kujulikana kuanzia Juni 28, 2025.

Wabunge hao akiwemo Halima Mdee wanahitimisha uhai wa Bunge hilo wakiacha historia ya aina yake hususan mvutano baina yao na Chadema.

Mwaka 2020, baada ya uchaguzi mkuu, Chadema kilipinga matokeo ya uchaguzi na kutangaza kutoshiriki mchakato wowote wa kisiasa ndani ya mfumo wa Bunge.

Hata hivyo, wanachama wake walioteuliwa kupitia orodha ya viti maalumu, ikielezwa kuwa pasipo ridhaa ya uongozi wa juu wa chama hicho walikwenda bungeni ambako waliapishwa.

Ilikuwa Novemba 24, 2020 Spika wa wakati huo, Job Ndugai aliwaapisha nje ya ukumbi wa Bunge wabunge hao 19 wa viti maalumu, licha ya kuwapo mzozo kati yao na chama chao.

Waliapishwa nje ya ukumbi wa Bunge kwa kuwa kipindi hicho kilikuwa cha ugonjwa wa Uviko 19.

Ndugai aliwaapisha ikiwa ni baada ya siku 14 kupita tangu wabunge wengine waapishwe ndani ya ukumbi wa Bunge.

Uhai wa Bunge hili la 12 unahitimishwa Juni 27 kwa Rais Samia Suluhu Hassan kulihutubia na kulivunja. Kwa sasa wabunge wanajadili bajeti za wizara mbalimbali na tayari Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake imemalizika.

Inayoendelea kujadiliwa ni ya Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Baadhi yao 19 waliopata fursa ya kuchangia wameshatangaza kwamba katika Bunge la 13 litakaloanza Novemba 2025 watakuwepo, japokuwa kuna usiri kuhusu vyama vipi watapitia.

Hata hivyo, sheria ya uchaguzi inatambua ubunge wa aina mbili, kuchaguliwa ama kuteuliwa na Rais, hivyo wanaochaguliwa ni lazima watokane na vyama vya siasa.

Katika kuonyesha hawatagombea kupitia Chadema, mara kadhaa kumekuwa na kauli kutoka kwa viongozi wa chama hicho cha upinzani wakisema ili kuwasamehe ni lazima waombe msamaha na kutaja jina la aliyewapeleka bungeni kuapishwa.

Wabunge hao 19 kabla ya kuenguliwa Chadema walikuwa na vyeo ambapo Halima Mdee alikuwa Mwenyekiti wa Bawacha, Grace Tendega (Katibu Mkuu wa Bawacha), Nustrat Hanje (Katibu Mkuu wa Bavicha), Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya na Agnesta Lambert.

Wengine ni Jesca Kishoa (Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha -Bara), Hawa Mwaifunga (Makamu Mwenyekiti wa Bawacha- Bara) na Tunza Malapo.

Pia Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Dalili za kukimbia Chadema

Tangu kuanza kwa Mkutano wa 19 wa Bunge mwanzoni mwa mwezi huu, baadhi yao wametoa michango kwa mtindo tofauti na ilivyokuwa awali ambapo wameonekana kupongeza mambo  yaliyofanywa na Serikali, huku wakitaka Watanzania wasimsumbue Rais Samia katika nafasi ya kugombea kiti chake.

Katika michango yao, wamekuwa wakimpongeza Rais Samia na uongozi wa Bunge hususan, Spika Tulia Ackson jinsi walivyosimama kidede kuwatetea kwa kipindi chote cha takriban miaka mitano licha ya kuitwa majina mbalimbali ikiwemo ‘Covid 19.’

Salome Makamba ambaye alijipambanua wakati akichangia hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo alisema haungi mkono kauli mbiu ya No reforms, No election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ ambao ndiyo msimamo wa Chadema.

Makamba alitangaza anaunga mkono kundi la G55 limo ndani ya Chadema linaloundwa na waliokuwa wagombea ubunge mwaka 2020 na watia nia wa nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao ambao wao msimamo wao ni kuendelea kudai mabadiliko, lakini washiriki uchaguzi.

Makamba akizungumza na waandishi nje ya Bunge alisema: "Kurudi bungeni ni lazima, tutakutana hapa Novemba katika Bunge la 13 lakini nitagombea wapi na kwa chama gani hilo liache kwanza."

Makamba pia alimpigia debe Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiwataka wananchi wa Mbeya kufanya kila jambo kuhakikisha anarudi tena bungeni ili aendelee kuhudumu katika nafasi hiyo, akijigamba atarudi naye kwa mara nyingine.

Tofauti na Makamba, Ferister Njau ameweka wazi kwamba anakwenda kugombea Jimbo la Moshi Vijijini ingawa amekuwa na kigugumizi kuhusu chama atakachopitia.

"Nitagombea ubunge kama kawaida, tena nakuhakikishia nitarudi tena bungeni maana kila kitu kipo sawa kwangu," alisema Njau.

Nusrat Hanje kwa upande wake alitangaza kugombea Jimbo la Ikungi na tayari alishaanza kufanya mikusanyo inayoashiria atagombea. Katika kulikoleza hilo,  mbunge wa jimbo hilo, Miraj Mtaturu akimkaribisha kwa mapambano.

Pia mwishoni mwa wiki kwenye mchango wake Hanje alimmwagia sifa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ikungi Michael Kapakapa kwamba alifanya vizuri pia viongozi wa Serikali kuanzia kwa Rais Samia, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wakuu wa na wilaya zote za Mkoa Singida.

"Nasema hivi, mambo yetu sisi watu wa Ikungi mtayashuhudia hapo mbeleni kidogo, nasema tutafanya makubwa mtayashuhudia kwenye kura za Rais kwani mama wa watu hana baya na mtu,” alisema Hanje.

“Kuna sehemu tulikuwa tumekwama, lakini sasa tunakwenda vizuri na mambo mengine yote yatakuwa mazuri wala hakuna namna yoyote tutasimama,” alisema.

Mwingine ni Hawa Mwaifunga ambaye naye ametangaza kuwania Jimbo la Tabora Mjini lakini pia hakusema wala kutaja chama atakachopitia.

Katika mchango wake Stella Fiyao hakusema hadharani kama anakwenda kugombea lakini amekuwa akiipongeza na kuisifia Serikali huku msisitizo mkubwa ukiwekwa kwenye kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan, ili ashinde kwa kishindo uchaguzi wa Oktoba mwaka huu.

Alisema hakuna namna kwamba nchi nzima inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi hivyo ni vema wakaendelea kuwapongeza watu wote, ikiwemo madiwani na watumishi wengine.

Fiyao alimtaja Rais Samia kuwa amelinda heshima ya mwanamke wa Tanzania na kuwafanya wengi kutembea kifua mbele kuliko walivyokuwa wakidhani, lakini akaonyesha mshangao kwa baadhi ya watu wanaopinga kupongezwa kwake wakati akikitaja Chadema kuwa kilianza kutoa pongezi kabla.

“Wote mliona jinsi sisi wabunge 19 tulivyoitwa jina la Covid 19, lakini Rais Samia alipokutana na wanawake wa Chadema Machi 8, 2025 alivyopinga jambo hili akisema jina hilo ni gonjwa, lakini siku hiyo Wanawake wa Chadema walisimama na kumpa tuzo Rais, leo hii watasema nini mbele ya Watanzania kuhusu kiongozi huyu,” alihoji Fiyao.

Aliwataka Watanzania kuendelea kumtia moyo na kueleza ukweli kuwa kiongozi huyo mkuu wa nchi anafanya kazi kubwa na nzuri inayopaswa kukubaliwa na wengi, akisema hakuna namna lazima apewe miaka mingine ya kuongeza.

Fiyao aliwamwagia sifa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wengine ikiwemo Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo na watendaji wengine aliosema wamekuwa na msaada mkubwa katika kusimamia na kutekeleza kazi za Serikali, lakini kutokuwatenga wabunge kwa itikadi za vyama vyao.

Walivyoishi bungeni

Wakati akiwaapisha aliyekuwa Spika  wakati huo, Ndugai alisema angewalinda kuanzia mwanzo hadi mwisho, huku akikemea watu wasiwabeze kwa sababu ni wabunge kama wengine.

Ndugai alitaka watu waache kubeza ubunge wao kwani wapo kihalali kwa mujibu wa Katiba ya nchi na kanuni za kibunge zinamtaka awalinde. Hata alipong'atuka, aliyekuwa Naibu Spika Dk Tulia Ackson aliendeleza msimamo wa mtangulizi wake akisisitiza wasisumbuliwe.

Hata hivyo, Spika Dk Tulia alisema hajapokea barua kutoka Chadema yenye malalamiko kwani angepata huenda angekuwa na maamuzi mengine.

Hata hivyo Chadema kupitia maofisa wao waliwaambia waandishi wa habari kuwa, walishapeleka barua Ofisi ya Spika lakini utekelezaji wake haukuwa na tija kiasi cha kuona kama vile kiti cha Spika kilikuwa kinawapendelea.